mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Monday, July 25, 2016

Mtandao wa haki za binadamu walia na Jeshi la Polisi



Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umelitaka Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuwafikisha mahakamani wanachama wake wanne linaowashikilia kwa siku 12 sasa. 

Mtandao huo umedai kuwa watu saba wilayani Longido wanatuhumiwa kutoa taarifa kwa mwanahabari wa Sweden, Susana Nurduland ambaye anafuatilia kwa karibu migogoro ya ardhi wilayani humo. 

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema uendeshaji wa madai hayo umegubikwa na upendeleo wa wazi jambo lililo kinyume na matakwa ya sheria za nchi kwa watuhumiwa wa makosa ya jinai. 

“Hadi sasa watetezi wanne wamenyimwa dhamana wakati wengine wenye nafasi za kisiasa wamepewa. Hii si sawa,” alisema Olengurumwa. 

Aliwataja walionyimwa dhamana kuwa ni Samwel Nangiria, Supuk Olemaoi, Clinton Kairung na Yohana Mako wakati walioachiwa ni mbunge wa zamani wa Ngorongoro, Mathew ole Timan, Diwani wa Ololosokwani, Yanick Ndina Timan na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundoros, Joshua Makko. 

Alieleza kuwa watetezi hao wamenyang’anywa vitendea kazi vyao pamoja na vifaa vya mawasiliano zikiwamo simu za mkononi na kompyuta mpakato. 

Wakili wa Kujitegemea wa kampuni ya Law Guards Advocates, Jebra Kambole alisema hiyo ni kinyume na sheria zinazosimamia haki za binadamu nchini. 

“Kumshikilia mtu muda mrefu bila dhamana pamoja na kunyimwa uwakilishi ni kinyume na Katiba ya nchi. Ni kinyume na Azimio la Umoja wa Mataifa la Watetezi wa Haki za Binadamu la mwaka 1998,” alisema Kambole baada ya kueleza kuwa watuhumiwa hao wamenyimwa haki ya kuwatumia mawakili. 

Licha ya ombi hilo kwa Polisi, mwanachama wa mtandao huo, Rose Sarwatt alimuomba Jaji Mkuu kuingilia kati suala hilo ili kuhakikisha haki inatendekea. 

Aliziomba asasi za kimataifa kukemea na kuishauri Serikali juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea huko Loliondo. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jeshi lake linasimamia na kutekeleza sheria za nchi na halichagui wa kumkamata kama amefanya kosa la jinai.

 “Lazima ukamatwe labda uwe na kinga. Hata mimi, japo kazi yangu ni kukamata lakini nikifanya jinai nitakamwa tu,” alisema na kubainisha kuwa taratibu zinaendelea kuzingatiwa na zikimalizika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.

Askofu Gwajima amjibu Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba aliyemuita muongo



Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemjibu katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba aliyemtuhumu kuwa ni mwongo akisema leseni yake ni ya kuendesha magari makubwa na siyo vibajaji na maguta. 

Akihubiri katika kanisa lake jana, Gwajima bila kutaja jina la Makamba, alisema: “Siwezi kushughulika na vigari vidogovidogo nyie mnanifahamu, mimi nina leseni ya kuendesha semi trailer …nadhani mmenielewa,” alisema huku waumini wake wakimshangilia. 

Juzi, Makamba aliwaeleza wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kuwa Askofu Gwajima ni kiongozi wa dini lakini ni muongo na kuwa uongo wake unawaudhi hata waumini wake ambao ni wanachama wa chama hicho. 

Alisema Gwajima amekuwa akisema uongo kuwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete hataki kuachia madaraka ya uenyekiti wa chama hicho, kitu ambacho Rais huyo mstaafu alikanusha akisema ni yeye alikwenda kumshawishi Dk John Magufuli kuchukua nafasi hiyo kabla ya muda wa uliopangwa kikatiba. 

Katika mahubiri hayo, Gwajima pia alisema mafunzo aliyoyapata tangu akiwa mdogo ni kuogopa kugombana na watu wa aina tatu, walevi, wazee na wagonjwa. 

“Baba yangu alinifundisha nisigombane na walevi, wazee na wagonjwa kwani ukimpiga kidogo mtu wa aina hiyo anaweza kufa,” alisema Gwajima. 

“Hata nyie waumini wangu nawaomba msigombane na watu wa aina hiyo kwani mnaweza kupata matatizo,” alisema. 

Kiongozi huyo aliongoza mamia ya waumini wake kumuombea Rais Magufuli kwa kushinda uenyekiti wa CCM akisema kofia hizo mbili zimempa meno ya kung’ata na zitamwongezea kasi ya kutatua matatizo ya wanyonge nchini.

Rais Magufuli juzi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM baada ya kupata kura zote 2,398 alizopigiwa na wajumbe wa mkutano huo. 

Kutokana na ushindi huo, Gwajima alisema Magufuli amepewa meno ya `kung’ata’ kila upande tofauti na alipokuwa na kofia moja ya urais. 

Alisema kwa muda mfupi aliokaa madarakani, elimu ya msingi na sekondari zimeanza kutolewa bure kitendo ambacho maskini na wanyonge wa nchi hii wameanza kuuona mwanga. 

Alisema ataendelea kumwombea Magufuli kwa sababu kazi anazozifanya zinawanufaisha wanyonge na maskini ambao kwa muda mrefu walipuuzwa katika nchi yao.

“Kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti ni zawadi kwetu Watanzania, tuendelee kumwombea kila siku ili aendelee kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi,” alisema. 

Alisema nafasi hiyo mpya itamwezesha kupambana na rushwa tatizo ambalo ameonyesha kuwa `atalivalia njuga’ hata ndani ya chama hicho. 

Mbali na Rais Magufuli, Gwajima aliwaombea pia Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri na Spika wa Bunge kwamba Mungu awalinde ili wamsaidie Rais kutekeleza majukumu yake. 

Kwa mwezi mzima, Askofu Gwajima amekuwa akitafutwa na Polisi baada ya kusambaa kwa sauti inayosikika kama yake ikitaka Rais mstaafu Kikwete afikishwe mahakamani kwa makosa yote yaliyofanyika katika utawala wake. 

Katika mkanda huo, sauti hiyo inadai baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka Magufuli asipewe uenyekiti ambao umekuwa ukishikiliwa na Kikwete. 

Baada ya sauti hiyo, Gwajima aliondoka nchini kwenda Japan lakini Polisi waliendelea kumsaka hadi Julai 12 walipomkamata katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), aliporejea. Alihojiwa na kuachiwa siku hiyohiyo.

Rais Magufuli mgeni rasmi Sherehe za Mashujaa Dodoma



AMIRI Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Kitaifa, yatakayofanyika mjini Dodoma leo.

Hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa maadhimisho hayo kufanyika nje ya Jiji la Dar es Salaam, tangu Tanzania ipate Uhuru wake mwaka 1961. 

Pia, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuongoza maadhimisho hayo tangu alipochaguliwa Oktoba mwaka jana.

"Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yatafanyika kitaifa mkoani Dodoma katika Uwanja wa Mashujaa siku ya Jumatatu (leo) Julai 25, 2016 kuanzia saa 1 kamili asubuhi hadi saa 4:30 asubuhi. 

“Mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli," alisema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, jana.

Alisema anaishukuru serikali kwa kuupatia mkoa huo, ambao ni Makao Makuu ya nchi, heshima ya kipekee katika historia ya nchi ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kitaifa.

Rugimbana alitaja shughuli zitakazofanyika siku hiyo kuwa ni gwaride la maombolezo litakaloshirikisha vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na Magereza.

Kutakuwa pia na upigaji mizinga na uwekaji wa silaha za asili na shada la maua kwenye mnara, kama ishara ya kumbukumbu kwa mashujaa. Shughuli nyingine ni utoaji wa dua na sala, utakaofanywa na viongozi wa madhehebu ya dini.

Rugimbana aliwataka wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwenye Viwanja vya Mashujaa kushiriki kwenye maadhimisho hayo. Alisema hadi jana, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya shughuli hiyo yalikuwa yamekamilika.

Rais wa Zanzibar Dr Shein Afuata Nyayo za Magufuli...Aanza Tumbua Tumbua Majibu Uchungu


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, amefuta uteuzi wa Naibu Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Hafidh Ussi Haji huku akimteua Khadija Shamte Mzee, kuchukua nafasi hiyo.

Pia, taarifa ya Ikulu inaonyesha Dk Shein, amemteua Amour Hamil Bakari kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar kuchukua nafasi ya Abdi Khamis Faki ambaye anastaafu kwa mujibu wa sheria.

Vilevile, Dk Shein amemteua Umi Aley kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Magazeti ya Serikali; Said Bakar Jecha na Sebtuu Mohammed Nassor wameteuliwa kuwa Makamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wakati Ali Saleh Mwinyikai ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji Zanzibar.Wengine walioteuliwa ni Maryam Hamdan kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu na Utamaduni, wakati Maryam Abdulla Yussuf ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani Zanzibar na Profesa Ali Seif Mshimba, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Viwango Zanzibar. Uteuzi huo unaanza Julai 25.

Diwani Moshi Akwepa Risasi Sita, Apambana na Majambazi Mwanzo Mwisho....


Hii ni kama filamu lakini ndio ukweli, Diwani wa Kata ya Kiborlon Manispaa ya Moshi, Frank Kagoma (Chadema) ameonyesha ujasiri wa hali ya juu alipopambana na majambazi waliokuwa na silaha za moto.

Alinusurika kuuawa baada ya majambazi hao waliokuwa na bunduki na bastola, kumfyatulia risasi sita alipokuwa akiwafukuza ambazo hata hivyo, hazikumpata.

Tukio hilo ambalo lilionekana kama sinema, lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya majambazi hayo kuvamia duka la jumla la kuuza mitumba linalomilikiwa na Menti Mbowe na kupora Sh10 milioni.

Katika tukio hilo lililotokea saa tano asubuhi eneo la Kiborlon, majambazi hayo walimjeruhi kichwani mfanyabiashara huyo anayemiliki pia mabasi ya Machame Safaris. Hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri.

Henry Kilewo:Dar es Salaam ipo Chini ya Chadema/Ukawa, Ndio Maana Analazimisha Serikali Kuhamia Dodoma


Nimesikia Mwenyekiti Mpya wa CCM Taifa ambaye alikuwa anagombea pekee ambaye pia alitangazwa na NEC kuwa Rais akisema atahamishia serikali yake Mkoani Dodoma kutoka Dar es salaam..
Ni kweli ni lazima serikali ihamie Dodoma kwakuwa Dar es salaam ipo chini ya Chadema/Ukawa na siyo CCM ndiyo maana analazimisha ihamie Dodoma.. Mkuu unasubiri nini? Ihamishie kesho maana Dar es salaam imewakataa ccm peleka sehemu ambayo Nec wamewatangaza...

Naelewa kuwa serikali kuhamia Dodoma ilikuwa ni adhima ya Mwl.Nyerere ila lilipouzwa kwakuwa Dar es salaam lilikuwa shamba la Bibi ila kwasasa kwakuwa Dar es salaam imeikataa CCM ni lazima Serikali ihamie Dodoma kama ambavyo imekuwa matakwa ya wengi na kupuuzwa... Tunakwenda kuichukua Dodoma 2020 na ndiyo mwisho wenu.....
Henry Kilewo
Katibu Greater Dsm (Chadema)

Vikongwe wawili wauawa kwa tuhuma za uchawi


Vikongwe wawili mke na mumewe wa Kitongoji cha Nyag’holongo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameuawa kwa kutumia silaha za jadi na watu wasiojulikana wakituhumiwa kuwa ni wachawi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Isack Msengi alisema tukio hilo lilitokea Julai 22 saa tatu usiku nyumbani kwao.

Aliwataja wanandoa hao kuwa ni Machene Magina (80) na Mkewe Genke Bundara (75) ambao waliuawa na wananchi wakiwatuhumu kwa uchawi.

Msengi alisema watu watano wanashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea. Diwani wa Kata ya Nanda, Jumamosi Mathias alisema kundi la watu ambalo halijulikani lilivamia nyumbani kwa familia hiyo wakati wakijiandaa kulala na kufanya ukatili huo.

Mathias alisema akiwa nyumbani kwake, alisikia kelele za watu wakisema; “Tumechoshwa na hawa wachawi. Kwa kuwa hawa wazee ni majirani zangu, nilianza kuhangaika ili kuona jinsi ya kudhibiti maafa hayo,” alisema Mathias.

 Hata hivyo, alisema kabla ya kutoa taarifa polisi, watu hao waliivamia nyumba hiyo na kufanya mauaji hayo ya kinyama kwa vikongwe hao.

Alilaani kitendo kilichofanywa na watu hao kuwa ni cha kikatili dhidi ya wazee kwani tangu aishi nao kijijini hapo hakuwahi kusikia tuhuma za uchawi dhidi yao.

Mathias alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwahisi wazee kuwa ni wachawi na kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawathamini na kuwalinda kwani wazee ni hazina ya Taifa.