mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Monday, July 25, 2016

Mtandao wa haki za binadamu walia na Jeshi la Polisi



Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umelitaka Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuwafikisha mahakamani wanachama wake wanne linaowashikilia kwa siku 12 sasa. 

Mtandao huo umedai kuwa watu saba wilayani Longido wanatuhumiwa kutoa taarifa kwa mwanahabari wa Sweden, Susana Nurduland ambaye anafuatilia kwa karibu migogoro ya ardhi wilayani humo. 

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema uendeshaji wa madai hayo umegubikwa na upendeleo wa wazi jambo lililo kinyume na matakwa ya sheria za nchi kwa watuhumiwa wa makosa ya jinai. 

“Hadi sasa watetezi wanne wamenyimwa dhamana wakati wengine wenye nafasi za kisiasa wamepewa. Hii si sawa,” alisema Olengurumwa. 

Aliwataja walionyimwa dhamana kuwa ni Samwel Nangiria, Supuk Olemaoi, Clinton Kairung na Yohana Mako wakati walioachiwa ni mbunge wa zamani wa Ngorongoro, Mathew ole Timan, Diwani wa Ololosokwani, Yanick Ndina Timan na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundoros, Joshua Makko. 

Alieleza kuwa watetezi hao wamenyang’anywa vitendea kazi vyao pamoja na vifaa vya mawasiliano zikiwamo simu za mkononi na kompyuta mpakato. 

Wakili wa Kujitegemea wa kampuni ya Law Guards Advocates, Jebra Kambole alisema hiyo ni kinyume na sheria zinazosimamia haki za binadamu nchini. 

“Kumshikilia mtu muda mrefu bila dhamana pamoja na kunyimwa uwakilishi ni kinyume na Katiba ya nchi. Ni kinyume na Azimio la Umoja wa Mataifa la Watetezi wa Haki za Binadamu la mwaka 1998,” alisema Kambole baada ya kueleza kuwa watuhumiwa hao wamenyimwa haki ya kuwatumia mawakili. 

Licha ya ombi hilo kwa Polisi, mwanachama wa mtandao huo, Rose Sarwatt alimuomba Jaji Mkuu kuingilia kati suala hilo ili kuhakikisha haki inatendekea. 

Aliziomba asasi za kimataifa kukemea na kuishauri Serikali juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea huko Loliondo. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jeshi lake linasimamia na kutekeleza sheria za nchi na halichagui wa kumkamata kama amefanya kosa la jinai.

 “Lazima ukamatwe labda uwe na kinga. Hata mimi, japo kazi yangu ni kukamata lakini nikifanya jinai nitakamwa tu,” alisema na kubainisha kuwa taratibu zinaendelea kuzingatiwa na zikimalizika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.

Askofu Gwajima amjibu Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba aliyemuita muongo



Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemjibu katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba aliyemtuhumu kuwa ni mwongo akisema leseni yake ni ya kuendesha magari makubwa na siyo vibajaji na maguta. 

Akihubiri katika kanisa lake jana, Gwajima bila kutaja jina la Makamba, alisema: “Siwezi kushughulika na vigari vidogovidogo nyie mnanifahamu, mimi nina leseni ya kuendesha semi trailer …nadhani mmenielewa,” alisema huku waumini wake wakimshangilia. 

Juzi, Makamba aliwaeleza wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kuwa Askofu Gwajima ni kiongozi wa dini lakini ni muongo na kuwa uongo wake unawaudhi hata waumini wake ambao ni wanachama wa chama hicho. 

Alisema Gwajima amekuwa akisema uongo kuwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete hataki kuachia madaraka ya uenyekiti wa chama hicho, kitu ambacho Rais huyo mstaafu alikanusha akisema ni yeye alikwenda kumshawishi Dk John Magufuli kuchukua nafasi hiyo kabla ya muda wa uliopangwa kikatiba. 

Katika mahubiri hayo, Gwajima pia alisema mafunzo aliyoyapata tangu akiwa mdogo ni kuogopa kugombana na watu wa aina tatu, walevi, wazee na wagonjwa. 

“Baba yangu alinifundisha nisigombane na walevi, wazee na wagonjwa kwani ukimpiga kidogo mtu wa aina hiyo anaweza kufa,” alisema Gwajima. 

“Hata nyie waumini wangu nawaomba msigombane na watu wa aina hiyo kwani mnaweza kupata matatizo,” alisema. 

Kiongozi huyo aliongoza mamia ya waumini wake kumuombea Rais Magufuli kwa kushinda uenyekiti wa CCM akisema kofia hizo mbili zimempa meno ya kung’ata na zitamwongezea kasi ya kutatua matatizo ya wanyonge nchini.

Rais Magufuli juzi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM baada ya kupata kura zote 2,398 alizopigiwa na wajumbe wa mkutano huo. 

Kutokana na ushindi huo, Gwajima alisema Magufuli amepewa meno ya `kung’ata’ kila upande tofauti na alipokuwa na kofia moja ya urais. 

Alisema kwa muda mfupi aliokaa madarakani, elimu ya msingi na sekondari zimeanza kutolewa bure kitendo ambacho maskini na wanyonge wa nchi hii wameanza kuuona mwanga. 

Alisema ataendelea kumwombea Magufuli kwa sababu kazi anazozifanya zinawanufaisha wanyonge na maskini ambao kwa muda mrefu walipuuzwa katika nchi yao.

“Kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti ni zawadi kwetu Watanzania, tuendelee kumwombea kila siku ili aendelee kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi,” alisema. 

Alisema nafasi hiyo mpya itamwezesha kupambana na rushwa tatizo ambalo ameonyesha kuwa `atalivalia njuga’ hata ndani ya chama hicho. 

Mbali na Rais Magufuli, Gwajima aliwaombea pia Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri na Spika wa Bunge kwamba Mungu awalinde ili wamsaidie Rais kutekeleza majukumu yake. 

Kwa mwezi mzima, Askofu Gwajima amekuwa akitafutwa na Polisi baada ya kusambaa kwa sauti inayosikika kama yake ikitaka Rais mstaafu Kikwete afikishwe mahakamani kwa makosa yote yaliyofanyika katika utawala wake. 

Katika mkanda huo, sauti hiyo inadai baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka Magufuli asipewe uenyekiti ambao umekuwa ukishikiliwa na Kikwete. 

Baada ya sauti hiyo, Gwajima aliondoka nchini kwenda Japan lakini Polisi waliendelea kumsaka hadi Julai 12 walipomkamata katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), aliporejea. Alihojiwa na kuachiwa siku hiyohiyo.

Rais Magufuli mgeni rasmi Sherehe za Mashujaa Dodoma



AMIRI Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Kitaifa, yatakayofanyika mjini Dodoma leo.

Hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa maadhimisho hayo kufanyika nje ya Jiji la Dar es Salaam, tangu Tanzania ipate Uhuru wake mwaka 1961. 

Pia, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuongoza maadhimisho hayo tangu alipochaguliwa Oktoba mwaka jana.

"Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yatafanyika kitaifa mkoani Dodoma katika Uwanja wa Mashujaa siku ya Jumatatu (leo) Julai 25, 2016 kuanzia saa 1 kamili asubuhi hadi saa 4:30 asubuhi. 

“Mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli," alisema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, jana.

Alisema anaishukuru serikali kwa kuupatia mkoa huo, ambao ni Makao Makuu ya nchi, heshima ya kipekee katika historia ya nchi ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kitaifa.

Rugimbana alitaja shughuli zitakazofanyika siku hiyo kuwa ni gwaride la maombolezo litakaloshirikisha vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na Magereza.

Kutakuwa pia na upigaji mizinga na uwekaji wa silaha za asili na shada la maua kwenye mnara, kama ishara ya kumbukumbu kwa mashujaa. Shughuli nyingine ni utoaji wa dua na sala, utakaofanywa na viongozi wa madhehebu ya dini.

Rugimbana aliwataka wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwenye Viwanja vya Mashujaa kushiriki kwenye maadhimisho hayo. Alisema hadi jana, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya shughuli hiyo yalikuwa yamekamilika.

Rais wa Zanzibar Dr Shein Afuata Nyayo za Magufuli...Aanza Tumbua Tumbua Majibu Uchungu


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, amefuta uteuzi wa Naibu Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Hafidh Ussi Haji huku akimteua Khadija Shamte Mzee, kuchukua nafasi hiyo.

Pia, taarifa ya Ikulu inaonyesha Dk Shein, amemteua Amour Hamil Bakari kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar kuchukua nafasi ya Abdi Khamis Faki ambaye anastaafu kwa mujibu wa sheria.

Vilevile, Dk Shein amemteua Umi Aley kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Magazeti ya Serikali; Said Bakar Jecha na Sebtuu Mohammed Nassor wameteuliwa kuwa Makamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wakati Ali Saleh Mwinyikai ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji Zanzibar.Wengine walioteuliwa ni Maryam Hamdan kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu na Utamaduni, wakati Maryam Abdulla Yussuf ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani Zanzibar na Profesa Ali Seif Mshimba, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Viwango Zanzibar. Uteuzi huo unaanza Julai 25.

Diwani Moshi Akwepa Risasi Sita, Apambana na Majambazi Mwanzo Mwisho....


Hii ni kama filamu lakini ndio ukweli, Diwani wa Kata ya Kiborlon Manispaa ya Moshi, Frank Kagoma (Chadema) ameonyesha ujasiri wa hali ya juu alipopambana na majambazi waliokuwa na silaha za moto.

Alinusurika kuuawa baada ya majambazi hao waliokuwa na bunduki na bastola, kumfyatulia risasi sita alipokuwa akiwafukuza ambazo hata hivyo, hazikumpata.

Tukio hilo ambalo lilionekana kama sinema, lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya majambazi hayo kuvamia duka la jumla la kuuza mitumba linalomilikiwa na Menti Mbowe na kupora Sh10 milioni.

Katika tukio hilo lililotokea saa tano asubuhi eneo la Kiborlon, majambazi hayo walimjeruhi kichwani mfanyabiashara huyo anayemiliki pia mabasi ya Machame Safaris. Hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri.

Henry Kilewo:Dar es Salaam ipo Chini ya Chadema/Ukawa, Ndio Maana Analazimisha Serikali Kuhamia Dodoma


Nimesikia Mwenyekiti Mpya wa CCM Taifa ambaye alikuwa anagombea pekee ambaye pia alitangazwa na NEC kuwa Rais akisema atahamishia serikali yake Mkoani Dodoma kutoka Dar es salaam..
Ni kweli ni lazima serikali ihamie Dodoma kwakuwa Dar es salaam ipo chini ya Chadema/Ukawa na siyo CCM ndiyo maana analazimisha ihamie Dodoma.. Mkuu unasubiri nini? Ihamishie kesho maana Dar es salaam imewakataa ccm peleka sehemu ambayo Nec wamewatangaza...

Naelewa kuwa serikali kuhamia Dodoma ilikuwa ni adhima ya Mwl.Nyerere ila lilipouzwa kwakuwa Dar es salaam lilikuwa shamba la Bibi ila kwasasa kwakuwa Dar es salaam imeikataa CCM ni lazima Serikali ihamie Dodoma kama ambavyo imekuwa matakwa ya wengi na kupuuzwa... Tunakwenda kuichukua Dodoma 2020 na ndiyo mwisho wenu.....
Henry Kilewo
Katibu Greater Dsm (Chadema)

Vikongwe wawili wauawa kwa tuhuma za uchawi


Vikongwe wawili mke na mumewe wa Kitongoji cha Nyag’holongo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameuawa kwa kutumia silaha za jadi na watu wasiojulikana wakituhumiwa kuwa ni wachawi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Isack Msengi alisema tukio hilo lilitokea Julai 22 saa tatu usiku nyumbani kwao.

Aliwataja wanandoa hao kuwa ni Machene Magina (80) na Mkewe Genke Bundara (75) ambao waliuawa na wananchi wakiwatuhumu kwa uchawi.

Msengi alisema watu watano wanashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea. Diwani wa Kata ya Nanda, Jumamosi Mathias alisema kundi la watu ambalo halijulikani lilivamia nyumbani kwa familia hiyo wakati wakijiandaa kulala na kufanya ukatili huo.

Mathias alisema akiwa nyumbani kwake, alisikia kelele za watu wakisema; “Tumechoshwa na hawa wachawi. Kwa kuwa hawa wazee ni majirani zangu, nilianza kuhangaika ili kuona jinsi ya kudhibiti maafa hayo,” alisema Mathias.

 Hata hivyo, alisema kabla ya kutoa taarifa polisi, watu hao waliivamia nyumba hiyo na kufanya mauaji hayo ya kinyama kwa vikongwe hao.

Alilaani kitendo kilichofanywa na watu hao kuwa ni cha kikatili dhidi ya wazee kwani tangu aishi nao kijijini hapo hakuwahi kusikia tuhuma za uchawi dhidi yao.

Mathias alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwahisi wazee kuwa ni wachawi na kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawathamini na kuwalinda kwani wazee ni hazina ya Taifa.

Friday, July 22, 2016

Tanzania Yatahadharishwa kuongezeka deni la taifa


Tanzania imeshauriwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo na kuchukua hatua kali dhidi ya fedha haramu badala ya kutegemea mikopo ya nje.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika utambulisho wa ripoti kuhusu Maendeleo ya Uchumi barani Afrika ya mwaka 2016 ya Shirika la Maendeleo ya Biashara la Umoja wa Mataifa (UNCTAD), Claudia Roethlisberger alisema mikopo siyo njia endelevu ya maendeleo.

Alisema licha ya ripoti hiyo kuonyesha kuwa madeni ya nchi za Afrika yanahimilika, lakini Serikali za nchi za bara hilo zinatakiwa kuchukua hatua ya kuzuia ukuaji wa haraka kwa madeni ili yasiwe mgogoro kama ilivyotokea miaka ya mwishoni mwa 1980 na 1990.

Akizungumzia ripoti hiyo, mchumi kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Prosper Charle alisema mikopo yenye masharti nafuu ambayo  Tanzania imekuwa ikitegemea imepungua na kubaki yenye masharti magumu, hivyo inapaswa kutafuta njia mbadala.

“Deni la Taifa kwa sasa linahimilika kwa sababu Tanzania ilikuwa ikipata mikopo yenye masharti nafuu ,” alisema.

Steven Mwombela kutoka Taasisi ya Utafiti wa Sera za kuondoa Umasikini (Repoa), alisema suluhisho kwa Tanzania ni kuwekeza kwenye ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi ili kupata maendeleo endelevu.

Nay wa Mitego Afungukia Picha za ‘Pale Kati’ Zilizo Mdhalilisha Mwanamke, Azikana


Msanii Nay wa Mitego ambaye siku za karibuni wimbo wake mpya ‘Pale kati’ umefungiwa na Baraza la sanaa Taifa (BASATA) amefunguka na kusema kuwa suala la watu kusambaza picha kwenye mitandao ya jamii huku zikiwaonyesha wanawake wakiwa hawana nguo kabisa siyo kosa lake yeye kwani hakufanya hicho kitu bali kuna watu walitengeneza hizo picha wakiwa na malengo yao.

Nay wa Mitego amesema hayo katika kipindi cha Planet Bongo ya East Africa Radio na kudai kuwa kuna watu walikuwa wanatengeneza picha hizo na kuzisambaza ila yeye hajafanya hivyo, na kudai kuwa alishajaribu kuwaripoti watu wengine ambao walikuwa wanafanya mchezo huo.

“Suala la picha za wimbo huo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii huku zikionyesha wanawake wakiwa nusu uchi si suala langu mimi, maana dunia ya sasa kuna watu wanafanya ‘editing’ ya picha sana, kama mtakumbuka hata kipindi nimetoa ‘Shika adabu yako’watu walinitengeneza sana kwenye picha na kusambaza kwenye mitandao ya jamii, hivyo suala la picha hilo siyo tatizo langu” alisema Nay wa Mitego.

Mbali na hilo Nay wa Mitego amesema kuwa yeye hajaridhishwa na maamuzi ya BASATA kufungia wimbo wake mpya kwa kigezo cha picha kwani walipaswa kusubiri video itoke ndiyo inaeleza vizuri maana ya wimbo wake huo.

“Huwezi kufungia ‘Audio’ kwa sababu ya picha BASATA walitakiwa kusubiri nitoe video kwani video inatoa tafsiri nzuri ya wimbo huo na kama kungekuwa na tatizo kwenye video ndiyo tulipaswa kukaa na hawa walezi wetu katika muziki BASATA ili kuona tunaweza kurekebisha jambo gani katika video” alimalizia Nay wa Miteg

TANZIA: KUNDAMBANDA afariki Dunia


Msanii maarufu wa VICHEKESHO (Komedi) Ndugu. Ismail Issa Makombe a.k.a KUNDAMBANDA, amefariki Dunia usiku wa kuamkia leo.

Kundambanda alikuwa mgombea ubunge wa CUF na UKAWA kwenye jimbo la Masasi - Mtwara katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Disemba 2015 baada ya ule wa Oktoba kutofanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mgombea wa awali wa UKAWA, Mhe. Emmanuel Makaidi (NLD). Katika uchaguzi huo wa Disemba 2015 Kundambanda alipata kura 14,069 dhidi ya kura 16,597 za (mshindi) Rashid Chua Chua kutoka CCM. Taratibu za mazishi zinafanyikia nyumbani kwao Masasi.  Inna lillah wainailayna rajiun. RIP Kundambanda.

Thursday, July 21, 2016

CHADEMA Wafungua kesi mahakama ya Afrika Mashariki dhidi ya Serikali


Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kimefungua rasmi kesi dhidi ya Serikali katika mahakama ya Afrika Mashariki kupinga zuio la kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika aliwaambia waandishi wa habari kuwa wameamua kufungua kesi hiyo kwakuwa tamko hilo la Serikali ni kinyume cha katiba na mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na sheria ya vyama vya siasa.

Mnyika ambaye aliambatana na mwanasheria wa chama hicho, John Mallya alisema kuwa wamekusanya ushahidi wa kutosha wa matamko ya katazo la kufanyika mikutano ya kisiasa na namna chama hicho kilivyozuiwa kufanya mikutano hiyo sehemu mbalimbali nchini.

“Tumeleta vielelezo vya zuio lenyewe la polisi kama ushahidi wa kwamba ni kweli polisi wa Tanzania wametoa agizo kama hilo. Pili, tumeleta vielelezo vya mikutano iliyozuiwa… mikutano ya Kahama, Mahafali ya wanachuo wa Chadema kule Dodoma, Mahafali yaliyofanyika kule Moshi na mikutano mingine,” alisema Mnyika.

“Katiba na sheria zetu zingekuwa zinaruhusu kumburuza moja kwa moja mahakamani Rais Magufuli, basi leo mashtaka yangekuwa dhidi ya Magufuli. Lakini  mwanasheria wa Serikali anasimama kwa niaba ya Serikali,” aliongeza.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema alisema kuwa mbali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wamemshtaki pia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani analo jukumu la kusimamia mikataba ya Jumuiya hiyo.

Alisema kuwa kesi hiyo ni aibu kwa Serikali ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzingatia kuwa Rais Magufuli ndiye mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa sasa.

Kikwete Akata Mzizi wa Fitina....Awapiga Kijembe Waliodhani CCM Itakufa


MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete, amekata mzizi wa fitna kwa kutangaza rasmi kuwa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, utakaofanyika mjini Dodoma kesho utafanya kazi moja tu ya kumchagua Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Kikwete alisema hayo alipofungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM kwenye ukumbi wa White House, makao makuu ya CCM, mjini hapa jana. Kauli hiyo ya Kikwete inamaliza minong’ono ya muda kuwa hapangekuwa na kupokezana kijiti katika mkutano huo.

Pia kauli hiyo imezima madai kwamba kungekuwa na mchujo katika uchaguzi wa Mwenyekiti, ambapo majina hadi matano yangependekezwa na Kamati Kuu na kupelekwa katika Halmashauri Kuu ambayo ingekata mawili na kupeleka matatu kwenye Mkutano Mkuu Maalumu, ili yapigiwe kura kumchagua Mwenyekiti.

“Ajenda yetu kubwa leo (jana) ni moja tu; nayo ni kupendekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili nayo Halmashauri Kuu ya Taifa ipendekeze kwa Mkutano Mkuu wa CCM ili achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM,” alisema Kikwete kwenye ufunguzi huo wa Kamati Kuu, akitumia dakika tano tu, kisha wajumbe wakaendelea na ajenda. Rais Magufuli alichaguliwa kuongoza Tanzania Oktoba mwaka jana.

Katika hotuba yake hiyo ya jana, Kikwete aliwajia juu ‘wafitini’ walioombea chama hicho kife katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Alisema “Wapo watu walidhani CCM ingekufa na walishajiandaa na salamu za rambirambi. Walidhani wataibuka. Hawakuibuka na hawataibuka kamwe.” 

Kikwete aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa kilikuwa kikao chake cha mwisho cha Kamati Kuu, kauli iliyobainisha wazi kuwa anang’atuka kumwachia kijiti Rais Magufuli kuongoza chama.

Alisema amekuwa Mwenyekiti wa Chama kwa miaka 10, hivyo aliwashukuru wajumbe wa Kamati Kuu kwa kumsaidia katika kipindi chote hicho huku akisisitiza; “Bila msaada wenu CCM isingekuwa imara kama ilivyo hivi leo.” 
 
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli alikuwa akifahamika kama Tingatinga na kwenye mikutano kadhaa, Rais mstaafu Kikwete aliweza kumuita kwa jina hilo.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete jana alikagua ukumbi wa mikutano wa CCM na kuoneshwa sehemu mbalimbali ambapo alisema ameridhika na maandalizi ya mkutano kwamba yanaenda vyema.

Maeneo mengine aliyotembelea ni mabanda ya mama na baba lishe, sehemu za kutolea huduma za Benki na mabanda ya maonesho ya wajasiriamali.

Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, makamu Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula, waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye, msemaji wa CCM Christopher Ole sendeka, naibu katibu mkuu wa CCM Bara Rajab Luhwavi na wajumbe wa Kamati Kuu Pindi Chana na Mohamed Seif Khatib. Wajumbe wa mkutano Mkuu maalum wa CCm walianza kuwasili jana na wengine wengi wanatarajiwa leo.

Zuio la Mikutano ya Kisiasa ni Kumyima Mwanchi Uhuru wa Haki ya Kujumuika- Kijo Bisimba.


Serikali imetakiwa kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali ambazo zimeonekana kuwa kandamizi ikiwepo ile sheria za vyombo vya habari ambazo zinakandamiza uhuru wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wenyewe.

Akitoa ripoti ya nusu mwaka mbele ya wanahabari kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu Bi Hellen Kijo Bisimba amesema kuwa vyombo vya habari havifanyi kazi kwa uhuru kwani zipo sheria ambazo bado ni kandamizi.

”Vyombo vya habari bado havina uhuru kwani sheria kandamizi bado zinatumika mfano, gazeti la mawio kufungiwa na kutakiwa kutoandika nakala zake hata kwenye mitandao bila sababu maalumu”.Ilielezwa katika ripoti ya kituo hicho

Aidha ripoti hiyo ya miezi sita imesema kuwa wananchi bado wananyimwa haki zao za msingi  ikiwa ni pamoja na  kunyimwa haki ya habari kwasababu  serikali imeamua kutorusha matangazo ya bunge kwa sababu mbalimbali ambazo zinakinzana.

Katika ripoti hiyo pia imegusa haki za kujumuika ambapo kituo hicho kimesema matamko ya jeshi la polisi hasa katika kuzuia mikutano ya vyama imeonekana  kupendelea chama tawala huku vyama vya upinzani  vikiwa vinakandamizwa.

”Mfano mkutano wa Chadema shinyanga ulipewa vibali vyote lakini baadae ukaja kutawanyishwa kwa kutumia nguvu mpaka mabomu, aidha ACT walikuwa na kongamano la kuchambua bajeti lakini jeshi la polisi walizuia lakini wakati huo huo CCM walikubaliwa kufanya mkusanyiko” Ilieleza semu ya ripoti ya Kijo Bisimba.

Pamoja na hayo ripoti hiyo imetoa mapendekezo kwa Serikali  ikiwa kuboresha sheria hizo kandamizi kwa wananchi pamoja na kuachia vyombo vya habari kufanya kazi zake pasipo kuingiliwa sambamba na Vyama vya siasa kupewa haki sawa.

Maalim Seif kutinga Mahakama ya ICC leo Kuwashitaki Viongozi wa Serikali


Chama cha Wananchi (CUF) kimesema katibu wake mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad leo atakwenda katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) kuwashtaki viongozi wa Serikali kwa madai walitumia mamlaka yao vibaya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kisha kuwatesa, kuwakamata na kuwapiga wafuasi wa chama hicho bila makosa. 

Chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar, kimesema taratibu zote za kufungua mashtaka hayo zimeshakamilika, ikiwa ni pamoja na kuweka wakili. 

Mei 22 mwaka huu, chama hicho kilizindua ripoti yake ya uvunjwaji wa haki za binadamu Zanzibar wakati wa uchaguzi huo na kutangaza azma yake ya kwenda ICC kuwashtaki Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP). 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema mpango huo umekamilika na Maalim Seif ambaye yuko nje ya nchi kwa ziara ya kueleza alichodai ‘figisufigisu’ zilizotokea katika uchaguzi mkuu, ataweka wazi kila kitu kilichotokea na jinsi ukiukwaji wa demokrasia ulivyoshika kasi nchini. 

Mazrui alimtuhumu IGP Mangu kuwa anatumiwa na CCM kuwakamata viongozi wa CUF ili wasitimize azma yao ya kueleza ukweli wa yaliyotokea katika uchaguzi, huku akimtaka afute azma yake ya kumkamata Maalim Seif kwa maelezo kuwa “ataitumbukiza Zanzibar kwenye machafuko”. 

Siku tano zilizopita, IGP Mangu wakati akihojiwa na Azam TV alisema Jeshi la Polisi wakati wowote litamburuza mahakamani Maalim Seif kwa kuhamasisha uchochezi Zanzibar. Iwapo CUF itatekeleza azima hiyo, itakuwa tukio la kwanza kwa Tanzania kupeleka viongozi wake kwenye mahakama hiyo. 

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na naibu wake, William Ruto wameshafikishwa huko, lakini kesi dhidi yao zilikosa nguvu na kuondolewa. 

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Salim Jecha Salim alifuta matokeo ya rais, wawakilishi na madiwani Oktoba 28, mwaka jana siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za urais. 

CUF ilidai kuwa ilishinda uchaguzi huo na Jecha alipotangaza uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu, chama hicho kilijitoa na hivyo CCM kushinda viti vyote. 

Mazrui ambaye aliambatana na viongozi wengine wa chama hicho alisema: “Mpango wa kuishawishi dunia kuwachukulia hatua wahusika wote wa ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjwaji wa demokrasia uko palepale, hautasitishwa kwa vitisho vyovyote.

 “Lengo ni kuhakikisha unyama dhidi ya raia wasio na hatia unakomeshwa na uzingatiwaji wa sheria za nchi unatamalaki. Tunawaambia polisi kuwa tumechoshwa na figisufigisu maana zitazaa timbwiri.” 

Mazrui alisema wanaotaka kuzuia mpango wa CUF kueleza ukweli na kwenda ICC, wanaandaa utaratibu wa kumkamata Maalim Seif aliyedai; “Ni kipenzi cha Wazanzibari”, akisisitiza kuwa jambo hilo ni hatari kwa sababu litaivuruga Zanzibar. 

Akifafanua zaidi kile alichokiita mikakati ya CCM kupitia kwa IGP Mangu kuficha ukweli, Mazrui alidai kuwa polisi wamekuwa wakiwakamata wanachama wa CUF mara kwa mara. 

"Niongeavyo hapa wanachama zaidi ya 400 wa CUF wamekamatwa na wengine wapo nje wa dhamana,” alisema. 

Alisema ni jambo la ajabu kuona IGP Mangu akishindwa kutoa kauli yoyote baada ya Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DDCI), Salum Msangi kuwatishia mawakili kuwatetea wananchi wanaokamatwa kwatuhuma  mbalimbali. 

Alisema viongozi wa CUF hawatatishwa wala kunyamazishwa katika kudai haki ya ushindi wa Wazanzibari kutokana na uamuzi wao wa uchaguzi mkuu. 

Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Shaweji Mketto alisema endapo IGP Mangu ataendelea kuwatisha viongozi wa CUF, watajipanga kwenda kumtembelea ofisini kwake.

IGP Mangu ajibu 
Alipoulizwa kuhusu kauli za CUF, IGP Mangu alisema tayari ameshatoa msimamo wa Jeshi la Polisi na walichokifanya viongozi wa chama hicho ni kumjibu tu. 

“Ukipendwa sana ukafanya uhalifu tukuache? Tukikutuhumu unafanya makosa tutakukamata hatuwezi kuogopa umaarufu wako,” alisema huku akisisitiza kuwa jalada kuhusu Maalim Seif lipo kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka).

“Umesema hao CUF wamesema kuna wanachama wao wamekamatwa, sasa wamekueleza hao wanachama ni kina nani?… kama wamekamatiwa Zanzibar wapo maofisa wa polisi wa mikoa wanaoweza kuzungumzia hilo huko Zanzibar.”

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema: “CCM hatuwezi kujiingiza katika hoja za IGP na CUF tumewaachia wenyewe. Kwa sasa tupo katika maandalizi ya kuhakikisha Rais (John) Magufuli anashinda kwa kishindo kuwa mwenyekiti wa CCM.” Alisema chama hicho hakina sababu ya kutumia Jeshi la Polisi kukandamiza wanachama na viongozi wa CUF.

Kesi za Uhujumu Uchumi zaigiza Bilioni 29


Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema Mahakama Kuu chini ya kitengo kinachosimamia kesi za kuhujumu uchumi imetoa adhabu ya kifungo na kulipa faini ya Sh29 bilioni kwa watu 12 baada ya kutiwa hatiani.

Pia, alisema Mahakama ya Mafisadi iliyoahidiwa na Rais John Magufuli wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, itakapoanza itashugulikia kesi za ufisadi zenye ushahidi.

Dk Mwakyembe alisema hayo jana kwenye mahojiano katika kipindi cha 360 kinachorushwa moja kwa moja, asubuhi siku za wiki na Televisheni ya Clouds.

 “Tuna kesi 176 za kuhujumu uchumi tangu Juni mwaka jana hadi sasa. Kesi 13 zimekamilika, watu 12 wamehukumiwa vifungo vya jela na tunawadai Sh29 bilioni kwa hiyo kama mtu alikuwa na ‘kastore’ tutauza tupate hiyo pesa,” alisema Dk Mwakyembe.

Aliongeza: “Nchi ilipofikia tunataka tuachane na hizi tabia za udokozi unapopewa mamlaka ya kuhudumia umma.”

 Alipoulizwa kuhusu mahakama ya mafisadi alisema: “Hatujaanzisha Mahakama, tumeanzisha divisheni (kitengo) ambacho kitasimamia kesi hizo kwa haraka na kwa weledi zaidi.”

Itakumbukwa kuwa Aprili Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowasilisha hotuba ya makadirio na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni alisema Serikali imeanzisha Divisheni ya Rushwa na Ufisadi ya Mahakama Kuu.

Majaliwa alisema mahakama hiyo itaanza kushughulikia kesi 10. Dk Mwakyembe alipoulizwa kama kuna kesi zozote zinazohusu EPA, Escrow au Richmond zitakazo sikilizwa, alijibu: “Sheria tunayotumia ni kwamba, kesi za jinai hazina vizuizi kwa upande wa Jamhuri.Hata kama ulichukuwa miaka 20 iliyopita, kama ushahidi unapatikana tutaendelea. Lakini hatuna interest kufufua makaburi ya huko nyuma.” 

Kuhusu mchakato wa Katiba inayopendekezwa alisema: “Ni kiporo ambacho tumepokea Serikali ya awamu ya tano na lazima tukimalize.”

Alisema kinachofanyika sasa ni kufuata Katiba kwa sababu mchakato huo ulisimama kupisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

“Tusingeweza kusimamisha uchaguzi kwa ajili ya kupiga kura ya maoni. Kwa hiyo tunasubiri wenzetu NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) wawe tayari ili mchakato uweze kuendelea,” alisema.

MAGAZETI YA LEO IJUMAA JULLY 22


Kikwete Atoa Dongo "Wapo Watu Walidhani CCM ingekufa na Walishajiandaa na Salamu za Rambirambi"


MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete, amekata mzizi wa fitna kwa kutangaza rasmi kuwa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, utakaofanyika mjini Dodoma kesho utafanya kazi moja tu ya kumchagua Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Kikwete alisema hayo alipofungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM kwenye ukumbi wa White House, makao makuu ya CCM, mjini hapa jana. Kauli hiyo ya Kikwete inamaliza minong’ono ya muda kuwa hapangekuwa na kupokezana kijiti katika mkutano huo.

Pia kauli hiyo imezima madai kwamba kungekuwa na mchujo katika uchaguzi wa Mwenyekiti, ambapo majina hadi matano yangependekezwa na Kamati Kuu na kupelekwa katika Halmashauri Kuu ambayo ingekata mawili na kupeleka matatu kwenye Mkutano Mkuu Maalumu, ili yapigiwe kura kumchagua Mwenyekiti.

“Ajenda yetu kubwa leo (jana) ni moja tu; nayo ni kupendekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili nayo Halmashauri Kuu ya Taifa ipendekeze kwa Mkutano Mkuu wa CCM ili achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM,” alisema Kikwete kwenye ufunguzi huo wa Kamati Kuu, akitumia dakika tano tu, kisha wajumbe wakaendelea na ajenda. Rais Magufuli alichaguliwa kuongoza Tanzania Oktoba mwaka jana.

Katika hotuba yake hiyo ya jana, Kikwete aliwajia juu ‘wafitini’ walioombea chama hicho kife katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Alisema “Wapo watu walidhani CCM ingekufa na walishajiandaa na salamu za rambirambi. Walidhani wataibuka. Hawakuibuka na hawataibuka kamwe.”

Kikwete aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa kilikuwa kikao chake cha mwisho cha Kamati Kuu, kauli iliyobainisha wazi kuwa anang’atuka kumwachia kijiti Rais Magufuli kuongoza chama.

Alisema amekuwa Mwenyekiti wa Chama kwa miaka 10, hivyo aliwashukuru wajumbe wa Kamati Kuu kwa kumsaidia katika kipindi chote hicho huku akisisitiza; “Bila msaada wenu CCM isingekuwa imara kama ilivyo hivi leo.”

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli alikuwa akifahamika kama Tingatinga na kwenye mikutano kadhaa, Rais mstaafu Kikwete aliweza kumuita kwa jina hilo.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete jana alikagua ukumbi wa mikutano wa CCM na kuoneshwa sehemu mbalimbali ambapo alisema ameridhika na maandalizi ya mkutano kwamba yanaenda vyema.

Maeneo mengine aliyotembelea ni mabanda ya mama na baba lishe, sehemu za kutolea huduma za Benki na mabanda ya maonesho ya wajasiriamali.

Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, makamu Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula, waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye, msemaji wa CCM Christopher Ole sendeka, naibu katibu mkuu wa CCM Bara Rajab Luhwavi na wajumbe wa Kamati Kuu Pindi Chana na Mohamed Seif Khatib. Wajumbe wa mkutano Mkuu maalum wa CCm walianza kuwasili jana na wengine wengi wanatarajiwa leo.

Samatta Kaisaidia KRC Genk Kutinga Round ya Pili ya Europa League


Mtanzania Mbwana Samatta bado anaendelea kufanya vizuri na kuzidi kuaminiwa na kocha wake Peter Maes ambaye kwa sasa amekuwa akimpa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza na kucheza dakika zote 90, usiku wa July 21 2016 Mbwana Samatta aliichezea KRC Genk mchezo wa pili wa Europa League dhidi ya Buducnost ya Montenegro.

Genk imecheza mchezo wake wa pili na kulazimishwa kucheza kwa dakika 120 na baadae mikwaju ya penati, dakika 120 zilimalizika kwa Buducnost kuongoza kwa goli 2-0, goli ambazo zilifungwa na Djalovic dakika ya 2 na Raickovic dakika ya 40 lakini mchezo uliamuliwa kwa mikwaju ya penati kutokana na KRC Genk kuibuka na ushindi kama huo katika mchezo wao wa kwanza.

Katika mikwaju ya penati Genk imefanikiwa kuibuka  na ushindi wa penati 4-2, penati za ushindi wa Genk zilipigwa na nahodha wao Thomas Buffel, Heynen, Mbwana Samatta na Walsh, hivyo kwa matokeo hayo sasa Genk itacheza round ya pili ya Europa League dhidi ya Cork City ya Jamhuri ya Ireland.