Serikali
itaanza kutumia mfumo wa uagizaji wa pamoja wa nishati ya gesi ya
kupikia (LPG), kama inavyofanyika kwa mafuta ya ndege, petroli, dizeli
na mafuta taa ifikapo Septemba mwaka huu.
Akizungumza
wakati wa semina ya wadau wa sekta ya mafuta kutoka mikoa ya Kanda ya
Ziwa, Mkurugenzi wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji
(Ewura), Godwin Samuel alisema mpango huo utasaidia kupunguza gharama na
bei ya gesi hiyo inayoanza kutumika kwa kasi majumbani.
Samuel alisema mpango huo pia utaongeza udhibiti wa mapato ya Serikali katika sekta hiyo inayoshika kasi nchini.
Kuhusu
uagizaji wa mafuta ya ndege, petroli, dizeli na mafuta ya taa,
Mkurugenzi huyo alisema mchakato unaendelea kuboresha mfumo wa sasa kwa
kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau yatakayotumika kubadilisha
taratibu zilizopo ifikapo Novemba, mwaka huu mikataba ya sasa
itakapomalizika.
“Tunakusudia
kuongeza ushindani wenye tija katika uagizaji wa pamoja wa mafuta ya
ndege, petroli, dizeli na mafuta taa kwa kuongeza idadi ya kampuni
kulinganisha na kandarasi zilizopo zinazofikia kikomo ifikapo Novemba
mwaka huu,” alisema Samuel.
Kuhusu
elimu kwa wadau, Mkurugenzi huyo alisema Ewura inalenga kuwawezesha
kujua na kuzingatia mabadiliko yanayotokea katika sekta na biashara ya
mafuta ili kuwezesha kila upande kutimiza wajibu kulingana na sheria,
kanuni na taratibu.
“Changamoto zinazoikabili sekta na biashara ya mafuta hayawezi kutatuliwa na Ewura pekee bali ni kwa ushirikiano wa wadau wote,”alisema.
No comments:
Post a Comment