mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira
Showing posts with label Habari kitaifa. Show all posts
Showing posts with label Habari kitaifa. Show all posts

Sunday, November 27, 2016

SABABU Zilizofanya Waziri Mkuu wa Zamani Fredrick Sumaye Kunyang'anywa Shamba lake

Hatimaye shamba lililokuwa linamilikiwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, lililopo Mabwepande limefutiwa hati zake na umiliki umerudishwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambayo itafanya utaratibu wa kupima viwanja na kuwagawia wananchi waliohusika kwenye mgogoro huo.

Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi zaidi ya 250 kulalamikia unyanyasaji wanaofanyiwa kupitia shamba hilo, na Mkuu wa Wilaya hiyo, Ally Hapi kupeleka malalamiko hayo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo Rais John Magufuli aliidhinisha kufutiwa hati kwa shamba hilo.

Akizungumza na wananchi wa kata hiyo ya Mabwepande jana, Hapi alisema shamba hilo lenye ekari 33 limefutiwa hati zake tangu Oktoba 28, mwaka huu na kwamba tayari Sumaye ameandikiwa barua ya kutojihusisha na shamba hilo baada ya kushindwa kukidhi masharti ya kisheria.

“Vyombo vya ulinzi na usalama watakuwepo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba shamba hili halitafanyiwa shughuli zozote isipokuwa baada ya taratibu za Manispaa zitakapofanyika,” alisema Hapi na kuongeza;

“Mgogoro wa shamba hili ni wa muda mrefu uliowahusisha wananchi. Lakini tunayo idadi ya wananchi ambao walikuwepo kwenye huu mgogoro na sasa wataalamu wataandaa mpango bora wa matumizi ya shamba hili,” alisema.

Aliongeza kuwa, wananchi hao waliokuwamo kwenye mgogoro ambao wataonekana wana vigezo vya kupatiwa viwanja, watafikiriwa kwa masharti ambapo baada ya kupimwa viwanja hivyo watawekewa gharama nafuu kwa ajili ya wao kununua.

Pia alisema, wananchi hao wenye makazi ya kudumu kwenye eneo hilo, watahakikiwa ili kuepusha watu wasiokuwamo kujiingiza kwa lengo la kuonekana nao walikuwa sehemu ya tukio.

Hata hivyo, alisema wataendelea kutoa taarifa kwa Rais kuhusu maeneo ambayo wananchi wanayahodhi bila ya kuyafanyia kitu chochote ili nayo yafutiwe hati.

“Natoa rai kwa wananchi wengine wenye maeneo ambayo hawayaendelezi tutayafutia hati na tutayamiliki wenyewe Manispaa ya Kinondoni. Pia tuendee kumuombea kwa kazi zake nzuri ili Mungu ampe ujasiri wa kupambana na ukabaila unaofanywa na wanaohodhi rasilimali za umma,” aliongeza.

Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Aaron Kagurumjuli kwa upande wake alisema, watahakikisha hadi Alhamisi wiki ijayo, timu ya ardhi wanaanza kupima viwanja hivyo na kuwagawia wananchi kwa masharti watakayoweka.

Kagurumjuli alisema watakaopewa kipaumbele katika ugawaji wa viwanja hivyo ni wale wenye makazi ya kudumu na watu ambao hawana makazi ya aina hiyo, watafikiriwa.

Wakazi wa kata hiyo walimpongeza Rais kwa hatua hiyo na kueleza kuwa matatizo kama hayo yapo sehemu nyingi nchini na yanatakiwa kutafutiwa ufumbuzi.

Abdallah Mohammed alisema kuwa walikuwa wanapata mateso kutoka kwa baadhi ya maaskari ambao walikuwa wanawanyanyasa kwa kuwatoa majumbani mwao usiku wa manane na kuwafungulia kesi.

Happy Makole alisema walikuwa wanaishi kwa wasiwasi kwa kuwa askari walikuwa wanawakamata waume zao na kuwaacha peke yao.

“Tumenyanyasika sana kuhusu eneo hili, mimi niliachwa usiku wa manane nikiwa na mtoto wakati mume wangu alipokuja kukamatwa. Lakini pia yapo maeneo mengine tunaendelea kunyanyasika tunaomba wayafanyie kazi malalamiko yetu,” alisisitiza Makole.

 – HABARILEO

Jengo la Makao Makuu ya TANESCO Ubungo Kubomolewa Wakati Wowote Kupisha Ujenzi wa 'Interchange'

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli amesema kuwa Jengo la Makao Makuu ya TANESCO lililopo Ubungo litabomolewa wakati wowote kuanzia sasa ili kupisha ujenzi wa Ubungo Interchange yenye ghorofa 2 mpaka 3 hali itakayopunguza msongamano wa magari kwenye eneo hilo.

Rais Magufuli amesema kuwa Serikali imepata shilingi Bilioni 67 kwa ajili ya ujenzi huo hivyo wakati wowote jengo hilo litabomolewa kwa vile lipo kwenye hifadhi ya barabara.

Hongera sana Rais Magufuli kwa kukumbusha tena suala hilo ambalo uliahidi miaka kadhaa iliyopita japo liliwekewa kizuizi na Rais Kikwete. Kwa sasa wewe ndiwe mwenye Rungu hivyo naamini kuwa hilo litatekelezwa ili kuondoa Double Standard.

Wednesday, November 16, 2016

Waziri Mkuu Kumtumbua Makonda Iwapo Atashindwa Kukomesha Matumizi ya Shisha

Warizi Mkuu, Kassim Majaliwa amesema atamwajibisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda iwapo hatasimamia ipasavyo kukomesha matumizi ya dawa za kulevya, aina ya shisha.
waziri-mkuu-kassim-majaliwa

Hatua hiyo inatokana na kauli ya Makonda kuwatuhumu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Suzan Kaganda, kulegalega kusimamia suala hilo huku akihofia wanaweza kuwa wamehongwa na watu waliotaka kumhonga lakini akakataa.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema katika udhibiti wa suala la shisha, mkuu huyo wa mkoa amefanya kazi nzuri, na kwamba kwa kuwa ameshatoa maelekezo, akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Makonda hana budi kuyatekeleza.

Alisema alivyosikia anawaagiza wakuu wake wa wilaya wote kusimamia maagizo yake na kama hawakusimamia atachukua hatua, basi naye atachukua hatua kwake (Makonda) asipotekeleza suala hilo ambalo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni tatizo kubwa.

“Sasa mimi nasema nakuagiza wewe usimamie na kama hutasimamia suala hilo nitakuchukulia hatua, hivyo hangaika na shisha kwa wanaopuliza wakiwa wamelala hakikisha unawadhibiti,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa wakati akijibu sehemu ya salamu za Makonda alipopewa fursa ya kusalimia wananchi katika hafla hiyo.

Katika salamu zake, Makonda alisema Waziri Mkuu alipiga marufuku matumizi ya shisha, hivyo alimwagiza Kamanda Sirro kuhakikisha suala hilo linatekelezwa kwa kiwango kikubwa.

“Lakini Waziri Mkuu nimeshangaa kupita katika baadhi ya maeneo na kuona watu wameanza tena kuvuta shisha na nilipouliza wakasema wewe ndiyo umetoa kibali cha shisha,” alieleza Makonda na kuongeza alishangaa Waziri Mkuu alipiga marufuku shisha, ni lini ametoa kibali kuanza kutumika.

Lakini mkuu huyo wa mkoa alienda mbali zaidi na kudai kuna kikundi cha watu 10 waliokwenda kwake ambao anawatambua kama “maajenti wa shetani” ambao wanapata faida kati ya Sh milioni 35 mpaka Sh milioni 45 kwa mwezi kutokana na dawa hizo za kulevya.

Alidai watu hao walipanga mikakati ya kumshawishi kupokea Sh milioni tano kwa kila mmoja kwa mwezi yaani Sh milioni 50 ili asipige kelele kuhusu shisha na wao waendelee kupata faida. “Shisha imerudi katika Mkoa wa Dar es Salaam na nimeshamuagiza Kamishna Sirro, lakini nimeona kama ana kigugumizi… lakini sijajua kama hizi tano tano zimepita kwake na pia RPC wa Kinondoni nimemuona hapa, lakini hawa wana kigugumizi sijui kama hizi tano tano zimepita kwao,” alisema Makonda.

Alisema aliamua kufanya ziara mwenyewe na kushuhudia watoto wadogo wanavuta shisha, hivyo uwezekano miaka 10 ijayo vijana wengi kuwa matatizo ya afya, hivyo kumwomba Waziri Mkuu kutochoka kusimamia suala hilo na taasisi zote ili likome katika mikoa yote.

Kuhusu wafanyabiashara wadogo, alisema suala hilo linamnyima usingizi na kutoa rai kwa wakuu wa wilaya kuwa, kama kuna mkuu wa wilaya atachelewa kutekeleza yale aliyoagiza kuwapeleka machinga katika maeneo yaliyoruhusiwa atachukua hatua kabla ya Waziri Mkuu kufanya hivyo.

Source: Habari Leo

Naibu Waziri wa Afya Anasa Kiwanda cha Viroba FEKI


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, akiwa ameongzana na timu ya Serikali yenye wataalamu na wanausalama wameendesha operesheni kali ya kusaka viroba feki na pombe nyingine haramu katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam  na kufanikiwa kukama shehena kubwa ya bidhaa hizo feki na haramu kwenye maeneo  hayo.

Katika operesheni hiyo, pia wamefanikiwa kukibaini kiwanda bubu kinachotengeneza kinywaji aina ya konyagi na Smirnoff feki maeneo ya Sinza Jijini Dar  es Salaam. 

Kiwanda hicho kinatengeneza vinywaji hivyo kwa kutumia ‘spirit’ ambayo inachanganywa na ‘gongo’; spirit, gongo, chupa tupu na zilizojazwa, vizibo, vifungashio vimekamatwa.

Kwa hatua hiyo Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili ambao inasemekana wanafanya kazi pamoja na bwana Yusuf Abdul Kalambo, ambaye anatafutwa na polisi mpaka sasa kwa tuhuma za kuendesha shughuli hizo.



Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla  akiwa ameshika vifuniko vya bidhaa za pombe feki katika moja ya kiwanda bubu cha kutengeneza pombe hizo aina ya Konyagi. katika zoezi hilo eneo la Sinza

Sunday, November 6, 2016

BUNGE LAPITISHA RASMI MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI WA 2016.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye alipokuwa akitoa hoja kabla Kamati ya Bunge zima kujadili Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 ambao umepitishwa leo mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge akitoa maelekezo wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 ili mjadala uwe na tija kwa maendeleo ya tasnia ya habari, wanahabari na taifa kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Aannastasia Wambura akichangia hoja juu ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 leo mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Walemavu Dkt. Possi Abdallah akichangia hoja juu ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 leo mjini Dodoma.
Mhe. Saada Mkuya Salum akichangia hoja juu ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 leo mjini Dodoma.
Wabunge wakiwa kwenye mjadala wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 leo mjini Dodoma.
Baadhi ya Watendaji wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto) wakifuatilia mjadala wa Wabunge wakati wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 leo mjini Dodoma.
Baadhi ya Watendaji wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto) wakifuatilia mjadala wa Wabunge wakati wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 leo mjini Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 leo mjini Dodoma.
Baadhi ya wageni wakifuatilia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 leo mjini Dodoma.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo mara baada ya kupitishwa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 leo mjini Dodoma. Wa nne kulia Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel.


Saturday, November 5, 2016

Bodi ya Mikopo Elimu Ya Elimu ya Juu Yaagizwa Kuwapa Wanafunzi Fedha Zao ifikapo Leo

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), imeagizwa kuhakikisha kuwa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo zinapelekwa vyuoni ifikapo leo.

Agizo hilo lilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako baada ya wabunge mbalimbali kuomba miongozo kwa Spika kuhusu kuwapo kwa wanafunzi wengi waliokosa mikopo kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Mwongozo kwa Spika ulitiliwa mkazo na Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwan Kikwete aliyeeleza kuwapo taarifa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa wanafunzi wanataka kugoma kwa kukosa fedha za mikopo.

Kutokana na miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga aliitaka Serikali kutoa maelezo.

Akitoa kauli ya Serikali, Profesa Ndalichako alisema fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi zilikwenda vyuoni wiki moja iliyopita.

“Tatizo lililotokea kwa UDSM sijui kama walidanganyana au la lakini hawakujaza fomu. Serikali haitatoa mkopo kwa mwanafunzi ambaye hajajaza fomu. Na waliosaini leo wataingiziwa fedha zao kwenye akaunti na vyuo,”alisema.

Kuhusu wanaoendelea na masomo, Profesa Ndalichako alisema wanafunzi wote wanufaika na wanaoendelea na masomo wataendelea kupatiwa mikopo kama ilivyokuwa mwaka uliopita.

Alisema wanafunzi ambao vyuo vyao vimewasilisha HELSB taarifa za matokeo, Bodi imekwishawatumia fedha vyuoni kwa ajili ya kuwapa mikopo wanafunzi hao.

Hata hivyo, alisema taratibu za kuwabaini wanafunzi wenye sifa zinaendelea na wasio na sifa wataendelea kuondolewa kupata mikopo.

Pia, alikiri kuwa ucheleweshaji wa matokeo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo umeathiri kasi ya kutuma fedha vyuoni.

“Wizara yangu imekwishaagiza vyuo vyote ambavyo havijawasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi wao kwa mwaka wa masomo uliopita, kufanya hivyo mara moja,”alisema.

Ndalichako alisema hadi kufikia Novemba 3 mwaka huu, Sh71.042 bilioni zilikwishatumwa vyuoni kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.

Akizungumzia utoaji wa mikopo kwa mwaka wa fedha 2016/17, Ndalichako alisema katika mwaka huo, Sh483 bilioni zimetengwa na zimelenga kutoa mikopo kwa wanafunzi 119,012, wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo na wa mwaka wa kwanza 25,717.

Ndalichako alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 wanafunzi 58,010 walidahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na orodha yao iliwasilishwa HELSB na hadi Novemba 2, mwaka huu, wanafunzi 21,190 wa mwaka wa kwanza wamepewa fedha. Kati yao 4,321 ni yatima, 118 wenye ulemavu na 87 ni waliosoma sekondari kwa ufadhili wa taasisi mbalimbali.

Wednesday, November 2, 2016

Boniface Jacob Ashinda ‘Umeya’ Manispaa ya Ubungo

Diwani wa Kata ya Ubungo ambaye pia alikuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kabla madiwani wake hawajagawanyika, Boniface Jacob ameshinda katika uchaguzi wa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo uliofanyika mapema leo mchana.

Mhe. Boniface Jacob kupitia Chadema ambaye pia anaungwa mkono na UKAWA ameshinda kwa kura 16 kati ya kura 18 za wajumbe.

Matokeo hayo yametangazwa na katibu wa mkutano huo DED Kayombo na yalikuwa kama ifuatavyo;

Nafasi ya Naibu Meya wapiga kura walikuwa 18, Kura halali zilikuwa 18, kura zilizoharibika 0.

Abdul Lema wa CCM amepata kura 3, Kwangaya Ramadhani wa Ukawa amepata kura 15 hivyo Kwangaya Ramadhani (Ukawa) ndiye Naibu Meya wa almashauri ya Manispaa ya Ubungo.

Nafasi ya Meya Wapiga kura walikuwa 18, Kura zote halali zilikuwa 18, Kura zilizoharibika ni 0.

Yenga CCM alipata kura 2 huku Boniface Jacob akipata kura 16.

Kwa matokeo hayo, Mhe. Boniface Jacob ndiye Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo

Mke wa Lema Aunganishwa Kesi ya Kumtusi RC Arusha

MKE wa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, Neema Lema (33) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na kuunganishwa katika kesi ya mume wake ya kumtukana Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuwa ni shoga.

Akimsomea mashitaka hayo kwa mara ya kwanza, Wakili wa Serikali, Blandina Msawa mbele ya Hakimu Augustino Rwezile, alidai kuwa kati ya Agosti 20, mwaka huu ndani ya Arusha, Neema ambaye ni mkazi wa Njiro alimtumia ujumbe wa simu ya kiganjani mkuu huyo wa mkoa wenye lugha ya matusi, huku akijua ni kosa kisheria.

Alidai mtuhumiwa huyo alituma ujumbe kutoka namba 0764 150 747 na 0756 551 918 kwenda namba 0766 757 575 uliokuwa ukidai, “Karibu, tutakudhibiti kama Uarabuni wanavyodhibiti mashoga.”

Mshitakiwa alikana shitaka hilo na yupo nje kwa dhamana hadi Novemba 15, mwaka huu itakapotajwa tena kesi hiyo.

Wapinzani Wapinga Takwimu Ukuaji Uchumi

LICHA ya takwimu za hivi karibuni kuonesha uchumi wa Taifa pamoja na Pato la Taifa vimekuwa vikikua kwa kasi na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye uchumi imara, kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imedai kuwa uchumi wa Tanzania umeyumba.

Kambi hiyo imetaja baadhi ya maeneo yanayothibitisha hilo kuwa ni mikopo inayotolewa na benki za biashara kwenye sekta binafsi kuwa imeshuka katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016.

Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Halima Mdee alisema mikopo hiyo imefikia Sh bilioni 1,167.2 ikilinganishwa na ongezeko la Sh bilioni 1,577.5 la mwaka 2015 katika kipindi kama hicho.

“Hii maana yake sekta binafsi imekosa Sh bilioni 410.3 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016. Hali hii imefanya mzunguko wa sarafu na noti mikononi mwa watu kushuka kutoka asilimia 188.8 Desemba 2015 na kufikia asilimia 6.7 Julai mwaka 2016,” alieleza.

Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amana za wateja katika benki zilipungua kutoka Sh trilioni 20.52 Desemba 2015 hadi kufikia Sh trilioni 20.24 Juni mwaka 2016.

Akichangia mapendekezo ya mpango huo wa maendeleo, Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM) alisema takwimu zinaonesha asilimia 53 ya viwanda vikubwa nchini vipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Kagera na Arusha, uwiano ambao si mzuri na kutaka viwanda viwepo kwenye mikoa mingine pia.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Dk Albina Chuwa, katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu, Pato la Taifa limeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 7.9 ikilinganishwa na asilimia 5.8 ya robo ya pili ya mwaka jana.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu alisema ukuaji wa Pato la Taifa katika nusu ya kwanza ya mwaka ya Januari hadi Juni, umeongezeka na kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 5.7 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2015

Tuesday, November 1, 2016

Magufuli: Huwa Nawasiliana na Rais Kenyatta, Hatuna Bifu Kama Watu Wanavyozani

Baada ya mwaka mzima tangu kuchaguliwa, rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amefanya ziara ya kwanza ya kiserikali nchini Kenya.

Kulikuwepo uvumi kuwa huenda kuna tofauti kali ya rais huyo na mwenzake wa Kenya hasa baada ya rais Magufuli kukosa kuhudhuria mkutano mkuu wa kibiashara ulioandaliwa jijini Nairobi.
Ziara hiyo ya siku mbili inanuiwa kudhihirisha nia safi kati ya Kenya na Tanzania pamoja na kuimarisha biashara.

Mwaka Mmoja wa Magufuli Kama Rais "Kamwe Huwezi Kuleta Mabadiliko ya Kimsingi Bila ya Kuwa na Kiwango Fulani cha Uwendawazimu"

Ndugu zangu,
Juzi hapa kwenye siku yake ya kuzaliwa, Rais wa Awamu ya Tano, Dr John Pombe Magufuli yumkini aliacha kula keki yake ya kusheherekea siku yake hiyo na kuamua kuwa kazini.
Zikatujia taarifa kubwa mbili; utenguzi wa uteuzi wa DCI na ziara ya kushtukiza wizara ya Maliasili na Utalii.

Nataka niwe mkweli kwa nafsi yangu, kuwa hata kama tungekuwa, kama nchi, na utaratibu wa kuwa na Rais wa kipindi cha mwaka mmoja, basi, huyu tuliye naye sasa, John Pombe Magufuli, angekuwa amemaliza muda wake wa mwaka mmoja akiwa ameacha alama nyuma yake, alama za kudumu muda mrefu.

Ukweli nchi yetu imeanza kubadilika na fikra za watu wake pia zimeanza kubadilika. Maana, ilifika mahali, kuna walioacha kazi kwenye NGO- Mashirika yasiyo ya Kiserikali na kwenda kufanya kazi Serikalini ikiwamo kwenye Halmashauri zetu wakitamka wazi kuwa kwenye NGO kazi nyingi, wanarudi Serikalini na kwenye Halmashauri kupumzika na kula posho za safari na nyinginezo.
Nchi haiwezi kusonga mbele ikiwa na watu wenye mitazamo kama hiyo. Ni lazima kuwe na nidhamu ya utendaji kazi na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu. Na wenye kukiuka hayo, ni lazima wajue kuna adhabu yenye kuendana na matendo yao maovu. Ndiyo siri kubwa ya nchi za wenzetu zilizoendelea.


Nilipata kuandika hapa, kuwa inavyoonekana; Magufuli Ana Uwezo Wa Kumwona Bata Na Sungura Kwa Wakati Mmoja..! ( Novemba 30, 2015)
Hii ni dhana kongwe ya kimtazamo iliyojengeka kifalsafa. Ni uwezo wa mwanadamu katika taswira moja kuwaona viumbe wawili wenye kufanana. Hivyo, inahusu uwezo kuliona jambo hilo hilo katika sura tofauti.

Ndio, kuna kuona kikiwa na kuona kama. Kuliangalia jambo kwa mtazamo tofauti.
Mwanafalsafa Thomas Kuhn yeye anazungumzia dhana ya ' Paradigm Shift'. Ni ile hali ya uwepo wa mapinduzi ya kifikra na ya kisayansi yenye kupelekea mabadiliko ya kimsingi katika jambo lile lile tulilokuwa na mazoea nalo.

Captain Thomas Sankara, kiongozi mwanapinduzi aliyeuawa wa Burkina Faso, katika wakati wake, alizungumzia umuhimu wa kuwa na ujasiri wa kuyapa mgongo mazoea ya kale.
Sankara aliacha hiba njema ya kuenziwa ndani ya nchi yake, Afrika na duniani. Mwanamapinduzi huyu alikuja kuawa kwa kupigwa risasi na wapinga mapinduzi na maendeleo ya Burkina Faso.
Sankara alipata kukaririwa akisema: “Ningependa kuacha nyuma yangu, imani ya kuwa, kama tunaimarisha kiwango fulani cha uangalifu na oganaizesheni, basi, tunastahili ushindi.

Kamwe huwezi kuleta mabadiliko ya kimsingi bila ya kuwa na kiwango fulani cha uwendawazimu. Hali hii inatokana na kutoshinikizwa na taratibu zilizozoeleka, kuwa na ujasiri wa kuzipa mgongo kanuni za kizamani, ujasiri wa kuanzisha mustakabali. Ni wendawazimu wa jana waliotuwezesha kuyafanya tuyafanyao leo. Ninataka kuwa mmoja wa wendawazimu hao.” (Hayati, Kapteni Thomas Sankara)

Yumkini tunachokishuhudia kwenye nchi yetu ni Magufuli's paradigm shift'. Hali ya kuwa na mabadiliko ya msingi.
Na hii ya Magufuli paradigm shift inaweza kuibadili nchi kwa haraka, maana kila mmoja atalazimika kubadilika.
Maggid,
Iringa

‘Makonda’ Feki Awatapeli Wachina Mil 22.8

Dar es Salaam. Raia wa China wametapeliwa fedha taslimu Sh 22.8 milioni wakidai kuwa sauti waliyoisikia kwenye simu ya kiganjani iliyotumiwa na tapeli ilifanana na ya  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alisema jana ofisini kwake kuwa Oktoba Mosi, mwaka huu mfanyakazi wa Kampuni ya Group Six ambaye  ni raia wa China, Marco Li (24) alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni Makonda.

Sirro alisema tapeli huyo alimtaka raia huyo atoe Dola 3,500 za Marekani kwa ajili ya msaada wa kumsomesha mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Manilla kilichopo nchini Ufilipino.

“Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Jensen Hung (39) alikubali ombi la mkuu wa mkoa huyo feki na kumtuma msaidizi wake, Marco Li aende ofisini kwake kwa ajili ya kujiridhisha,” alisema Sirro.

Saturday, October 29, 2016

Bibi Aliyejichongea Jeneza Afariki Dunia

Mkazi wa Kijiji cha Lindusi Peramiho mkoani Ruvuma aliyejichongea jeneza, Scholastica Mhagama amefariki dunia  kwa ugonjwa wa pumu.

Mapema mwaka huu wakati alipohojiwa na gazeti hili, bibi huyo alitaja sababu za kujichongea jeneza kabla ya kifo kuwa, ni kuhofia kuzikwa kama mnyama baada ya kuwa na ugomvi wa mara kwa mara na kaka zake.

Kaka yake mkubwa aliyekuwa akimhudumia kabla ya kufariki dunia, Felix Mhagama (82) alisema dada yake alikufa Jumanne ya wiki iliyopita kwa ugonjwa huo.

Mhagama alisema licha ya kipindi cha uhai wa dada yao, kugombana mara kwa mara walikuwa wakipatana na kumaliza tofauti zao.

“Ingawa mdogo wangu alikuwa na upungufu niliendelea kuzungumza naye na kumhudumia, kwani hakuwa na uwezo wa fedha na alinitegemea kwa kila kitu,” alisema. Alisema alikuwa akiumia kuona dada yake akiishi na jeneza hilo na kwamba, kuna wakati alimuuliza sababu za kufanya hivyo, alimjibu kuwa ni kutokana na kutokuelewana kwao.

Alibainisha kuwa kabla ya kifo chake, kuna watu walikwenda nyumbani kwake na kuvunja jeneza hilo na kuahidi kumtengenezea jingine.


Kuhusu chanzo cha ugomvi wa Scholastica na kaka zake, jirani yao, Cassian Kazimoto alisema  alikata tamaa ya kuishi kutokana na maradhi hayo ya pumu yaliyokuwa yakimsumbua na ulemavu baada ya kukatwa mguu.

Alisema  Scholastica alikuwa akiona kama anaonewa na kaka zake kutokana na ugomvi wao.

Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kimeshtushwa na tuhuma dhidi ya kiongozi wake wa chama, Zitto Kabwe kwamba ana miliki mali za kifisadi pamoja na kuhusishwa na ununuzi wa ardhi maeneo ya Kigamboni uliofanywa na NSSF kwa bei ya milioni 800 kwa ekari moja, wakati bei halisi ni milioni 25 na kwamba kitendo hicho kimeitia hasara serikali .

Tuhuma hizo zilitolewa jana na Msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Christopher Ole Sendeka, ambapo alivitaka vyombo vya uchunguzi kufanya uchunguzi katika shirika hilo ili kubaini waliohusika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria, huku akimhusisha Zitto katika uchunguzi huo.

Ole Sendeka alitaka akaunti za benki za Zitto pamoja na maisha yake binafsi kuchunguzwa kama yana uhalisia na kipato chake halali.

Tuhuma hizo zimekiibua chama cha ACT, ambapo leo Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa ACT, Habibu Mchange amevitaka vyombo vya uchunguzi haraka iwezekanavyo kuchunguza mali, madeni, akaunti zote za benki pamoja na mfumo wa maisha ya Zitto.

“ACT imeshtushwa na tuhuma, kashfa, porojo na matusi mbalimbali yaliyotolewa jana na Ole sendeka dhidi ya kiongozi wa chama chetu,” amesema.

Amesema kuwa, katiba ya chama hicho huwataka viongozi wote kuweka hadharani matamko ya mali zao na madeni na kwamba Zitto alitekeleza matakwa hayo ya kisheria hivyo mali na madeni yake yako hadharani na mtandaoni.

“Tunaamini kama kuna kiongozi ambaye mali, madeni, maslahi, na akaunti zake viko wazi basi ni ndugu Zitto,” amesema.

Aidha, Mchange amedai kuwa, kilichomsukuma Sendeka kutoa tuhuma hizo kwa Zitto ni harakati zake za kuupinga muswada mpya wa habari.

“Tuhuma za ole sendeka kuna kitu nyuma yake, jitihada za zito za kupambana na mswada wa habari ndizo zilizomuibua, sababu wanataka upitishwe ili kuviua vyombo vya habari,” amesema.

Amesema ACT itaendelea kuisimamia serikali katika mambo ya bungeni kama anavyofanya mbunge na kiongozi wao wa chama.

Breaking Newssss: Rais Dkt Magufuli Atengua Uteuzi Wa Mkurugenzi Wa Upelelezi Makosa Ya Jinai (Dci) Diwani Athumani Leo

Taarifa kutokea Ikulu Dar es salaam leo October 29 2016 ni pamoja na hii ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kutengua uteuzi wa mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI) Diwani Athumani.

Friday, October 28, 2016

Ripoti ya Mkataba wa Lugumi, Polisi Yafika kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Projestus Rwegasira amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge ya kuhakikisha mfumo wa vifaa vya utambuzi wa alama za vidole unafungwa katika wilaya za kipolisi 108 nchi nzima kwa muda wa miezi mitatu.

Zabuni ya kufunga na kusambaza mashine hizo za utambuzi wa vidole katika Jeshi la Polisi ulifanywa na Kampuni ya Lugumi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo Naghenjwa Kaboyoka, aliwathibitishia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa ripoti hiyo tayari imekabidhiwa kwa Ofisi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Kaboyoka alisema ripoti hiyo baada ya kukabidhiwa kwa Spika Ndugai ataipitia na baadaye kuiwasilisha kwa kamati hiyo ya PAC.

Juni 30, mwaka huu, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya kuahirisha Bunge la Bajeti aliiagiza serikali kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi kwa ajili ya kuwadhibiti wahalifu na kuitaka Kamati ya PAC ifuatilie suala hilo.

Dk Tulia alitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa yenye utata ya kuhusu zabuni yenye thamani ya Sh bilioni 37 ya kufunga mashine hizo katika vituo vyote vya Polisi baina ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited iliyotolewa mwaka 2011.

“Ninashauri serikali ihakikishe mradi huu unakamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia leo…, mradi huu utasaidia Jeshi la Polisi kuwatambua kwa haraka watu waliohusika katika matukio ya uhalifu mbalimbali,” alisema.

Katika mkataba huo, Lugumi inatakiwa kusambaza na kufunga mashine hizo za utambuzi wa vidole katika wilaya 108 za kipolisi nchi nzima.

Hata hivyo, mashine hizo zilifungwa kwenye vituo 14 pekee wakati tayari kampuni hiyo ilishapokea kiasi cha asilimia 99 za malipo yake.

Katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2013/14 ilionesha kuwa pamoja na kampuni hiyo ya Lugumi kulipwa asilimia 99 ya malipo sawa na Sh bilioni 34, bado haijakamilisha mradi huo kwa muda wa miaka mitano sasa.

Aprili, mwaka huu, PAC iliunda kamati ndogo kwa ajili ya kuchunguza mkataba huo wa utata baina ya Kampuni ya Lugumi na Jeshi la Polisi.

Sumaye Kunyang’anywa Shamba na Serikali, Apewa Notisi ya Siku 90

Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema hati ya shamba lililopo maeneo ya Bunju la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fredrick Sumaye liko katika hatua ya kufutwa na kwamba Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kinondoni Rehema Mwinuka ameshatoa barua ya notisi ya siku 90.

Lukuvi ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wandishi wa habari.

“Shamba la Sumaye hati yake iko katika hatua za kufutiwa,
Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ambaye anajukumu la kutoa notisi, ameshatoa notisi kwamba hajaendeleza eneo hilo kwa muda mrefu hivyo kwa mujibu wa sheria hati yake inatakiwa kufutwa,” alisema.

Alisema serikali haitofumbia macho wamiliki wa ardhi na mashamba ambao hawajayaendeleza kwa muda mrefu.

Pia, kufuatia ongezeko la matapeli wanaotumia nyaraka za kughushi za barua za toleo (ofa) zinazodaiwa kutolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Lukuvi alitoa agizo hususani kwa wakazi wa jiji hilo wanaomiliki ardhi pasipo kuwa na hati miliki, kujisalimisha kwa kupeleka barua zao za ofa kwa Kamishna wa Ardhi ili wapatiwe hati halali.

“Wamiliki wote wanaomiliki ardhi kwa karatasi za ofa halali wazibadilishie ili wapewe hati halali, na atakaegundulika kumiliki ofa feki polisi watawakamata na kupelekwa mahakamani,” alisema.

Alisema asilimia 60 ya watu wanaopeleka kesi za migogoro ya ardhi wizarani, chanzo cha migogoro hiyo ni karatasi za ofa zinazotoka katika halamshauri za jiji na manispaa.

“Natoa miezi mitatu ili karatasi hizi zisitokee tena kila mtu alete barua ya ofa watapewa hati zao ndani ya mwezi mmoja ,wazilete kwa kamishna wa ardhi wa mkoa, baada ya hapo sitasikiliza malalamiko ya watu walioibiwa ardhi wakiwa na ofa ya namna hii.

“Tumieni miezi mitatu vizuri kubadilisha ofa,” amesema.

Hali kadhalika, Lukuvi alipiga marufuku vitendo vya uvamizi wa ardhi na mashamba vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, na kuwataka wananchi kutoa taarifa pindi watakapobaini kuwa kuna shamba au ardhi isiyoendelezwa.

“Serikali ina laani uvamizi wa ardhi na mashamba unaofanywa na baadhi ya wananchi sababu baadhi yao yanamilikiwa kihalali na yana hati, serikali ipo na sheria zipo zitafanya kazi yake,” alisema.

CHADEMA yapinga kununuliwa na Lowassa, yashindwa kuzungumzia tuhuma za ufisadi.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema ni uongo na ni propaganda za wapinzani wao kwamba Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa alimhonga Mwenyekiti Freeman Mbowe ili kupata nafasi ya kugombea urais mwaka 2015.

Dkt.  Mashinji ameyasema hayo katika kipindi cha Kikaangoni  kinachorushwa na kituo cha EATV kupitia ukurasa wa facebook ambapo wananchi walikuwa wakimuuliza maswali ya papo kwa papo naye anayajibu.

“Si kweli kwamba Mwenyekiti Freeman Mbowe alimhonga Lowassa ili agombee urais kupitia CHADEMA , ni propaganda zinazoenezwa na wapinzani wetu ili kuwadanganya wananchi” Amesema Dkt. Mashinji.

Amesema Lowassa alijiunga na CHADEMA kwa njia halali kwa mujibu wa taratibu za chama, na maamuzi ya kumteua kugombea urais yalifanywa na vikao halali kuanzia ngazi ya Kamati Kuu hadi Mkutano Mkuu.

Kuhusu sababu za CHADEMA kumkaribisha Lowassa licha ya kumtaja miaka mingi kuwa alihusika na ufisadi, Dkt Mashinji, hakutaka kulifafanua kwa undani, lakini aliishia kusema kuwa wao walijiridhisha kuwa hakuwa na hatia yoyote na kwamba kama kweli alikuwa ni fisadi, basi vyombo vya dola vingemchukulia hatua.

"Kama mtu kweli alikuwa ni fisadi, kwanini hakuwahi kuchukuliwa hatua, hata kufikishwa mahakamani?, nadhani hilo tuliache" Alisema kwa ufupi Dkt Mashinji.

Aidha Dkt. Mashinji amewataka watanzania na wapenzi wa CHADEMA kufahamu kwamba chama hicho hakipo kimya bali kinaendelea na mikakati ya kuhakikisha kwamba kinawafikia watanzania kwa kuwatetea kwa kila hali kutokana na mambo yanayoendelea nchini.

Tamko: CCM Yawajibu Lowassa na Zitto Pia Yakana Kushiriki Kwenye Kuivuruga CUF

Ikiwa imepita siku mbili tangu aliyekuwa mgombea wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa mwamvuli wa UKAWA, Edward Lowassa kueleza tathimni ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano chini Rais John Magufuli, ambapo alidai kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi huo, kumekuwepo na ukiukwaji wa misingi ya demokrasia na utumishi wa umma kuwa kaa la moto.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimevunja ukimya na kumjibu kwa kusema kuwa katika kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita alikuwa wa kwanza kukiuka misingi ya demokrasia. Kuhusu utumishi wa umma kuwa kaa la moto, imemjibu kuwa wanao lalamika hivyo ni wale wanaotumiwa kuficha mafisadi na wakwepa kodi.

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka amewaambia waandishi wa habari kuwa Lowassa hastahili kuituhumu serikali ya Rais Magufuli kuwa inakiuka misingi ya demokrasia.

“Demokrasia ya kweli lazima ianze ndani ya chama, ni demokrasia ipi iliyotoa mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea kuvigharamia kwa kuamua kumteua mgombea mtunguo ambaye hajapimwa wala hajawahi kuvipigania?,” amehoji.

Ole Sendeka ameongeza kuwa “Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na kuwanyima haki yao kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kulidhihirisha usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia.”

Amesema CCM haigopeshwi na matamko ya Lowassa anayotoa katika vyombo vya habari kwa kuwa havitaiathiri na kwamba imemamua kumjibu kwa madai kuwa anapotosha umma kwa kueleza mambo yasiyo na ukweli.

Ametoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutochukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko.

“Wanasayansi wa masuala ya siasa waiangalie demokrasia ya CHADEMA na UKAWA inavyofanya kazi maana ni kihoja, watuambie njia iliyotumika kuwapata wabunge viti maalumu. Kila kiongozi aliteua maswahiba zake na wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA,” amesema.

Pia Sendeka amemtaka kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo kutoichukia serikali ya Rais Magufuli kwa kuwa inatekeleza yale aliyokuwa anayapigania.

“Chuki ya Zitto ya kuendelea kunyooshea kidole serikali ya CCM haina tija, sababu inatekeleza yote aliyokuwa akiyapigania,” amesema.

Katika hatua nyingine, Sendeka amedai kuwa CCM haijashiriki kukihujumu chama cha Wananchi (CUF) kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa kuwa kinawachonganisha viongozi wa chama hicho ili kigawanyike.

“Hatuna haja ya kuhangaika na CUF na wapanga siasa za uongozi CHADEMA, hatujashiriki kukivuruga na hatuna muda huo,” amesema.

=======

Ndugu wanahabari,

Kwa muda sasa kumekuwepo na usambazaji wa taairifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wakishirikiana na baadhi ya vyombo vya habari zinazolenga kukejeri, kudhihaki, kukatisha tama, kubeza na kudhoofisha jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Seikali zake katika kuleta maendeleo kwa Watanzania

Kumekuwepo na makala zinazoandikwa na magazeti mawili ya nje ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili na ambazo zinapotosha na kuandika habari zisizo za kweli kuhusu Tanzania

Pia, yapo magazeti mawili ya ndani ambayo yamekuwa yakitoa makala mfululizo kwa kila wiki zinazolenga kumchafua Mheshimiwa Rais na kuichafua taswira ya nchi yetu.

Tumesikitishwa na waandishi wa makala hizo walioamua kujivua uzalendo na kushiriki mpango wa kuiharibu heshima na taswira ya nchi yetu kwa maslahi ya maadui zetu wa nje na baadhi ya wanasiasa. Tunafuatilia kujua nini kinawasukuma kufanya hivyo na kwa maslahi ya nani ilhali sote ni watanzania. Je ni tama ya madaraka tu au mengine?. Hakuna anayepinga ukosoaji bali unapaswa uwe ukosoaji wenye nia njema

Ndugu wanahabari,

Mtakumbuka hivi karibuni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa tuhuma za ufisadi ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, alisambaza taarifa kwa vyombo vya habari aliyoiita tathimini ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa octoba 25,2015

Katika taairifa yake, alidai kuwa alileta msisimko mpya katika siasa za Tanzania, kwamba ameshirikiana na wenzake kuionyesha nchi yetu maana ya demokrasia na kukosoa juhudi za serikali na wateule wa Rais.

Demokrasia kimsingi ni dhana inayohusisha ushiriki na kuheshimu mawazo ya wengi katika kufikia uamuzi. Ikiwa maana halisi ni hii, tunajiuliza ni ipi demokrasia aliyoionyesha Lowassa ambayo leo anajisifu kuwa nayo?

- Tulishuhudia akiwa mgombea Urais wa chama ambacho hakijui, hakushiriki kukijenga wala kutoa mchango wowote unaompa hadhi ya kupeperusha bendela huku katiba na kanuni ya chama hicho ikivunjwa. Kidemokrasia anayepewa fursa ya kupeperusha bendela ya chama chochote makini duniani ni kiongozi au mwanachama aliyethibitika kwa imani na matendo, kuzielewa, kuzitekeleza, kuzitetea falsafa, itikadi na malengo ya msingi ya chamahicho. Mgombea ni taswira halisi na alama muhimu inayoakisi dhamira ya chama husika machoni kwa wananchi.

- Demokrasia ya kweli lazima ianzie ndani ya chama, ni demokrasia ipi inayotoa mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea, kuvigharamia na walivyovitumikia kwa kuamua kumteua mgombea “MTUNGUO” (ambaye hajapimwa wala hajawahi kuvipigania). Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kilidhihirisha usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia

- CHADEMA watuambia njia iliyotumika kuwapata wabunge wa viti maalumu. Ni demokrasia gani inayotoa fursa kwa baadhi tu ya viongozi kuteua wabunge ambao wanakiwakilisha chama chote. Ambapo kila kiongozi aliteua maswahiba zake na wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA walikosa watu wanaowafahamu na kuamua kuwateua wanawake maswahiba wao ndani ya CCM. Msingi wa kawaida wa kupata wabunge wa viti maalumu ukiacha kura za maoni, kigezo kingine muhimu ni mchango wa mgombea / mwanachamahuyo katika kukijenga na kukitumikia chama chake. Yaliyotokea kwa CHADEMA kwenye wabunge wake wa viti maalumu ni mapya kwenye ulimwengu wa demokrasia. Inahitaji wataalamu wa sayansi ya siasa kufanya utafiti wa aina hii mpya ya demokrasia

Tulidhani baada ya mwaka mmoja kupita, wenzetu hawa wangelikuwa wamejifanyia tathimini, kujikosoa, kujisahihisha, na hata kufanya uungwana wa kuwaomba radhi wanachama wao kwa uvunjifu mkubwa wa misingi ya demokrasia, katiba na kanuni za vyama vyao

Tunatoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutokuchukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko, yasiwe ni nyimbo za kuburudisha au kutoa matumaini hewaq kwa wanachama na wananchi. Kanuni mojawapo ya demokrasia ndani ya vyama ni lazima ionekane katika muundo wake na katika utekelezaji wa muundo huo

Umefika wakati vyama vya siasa vinapaswa kujifunza kuuza sera ili kujenga na sio kusubiri matukio kwa ajili ya kupata huruma ya wananchi. Tunasubiri kushuhudia na kusikia demokrasia demokrasia itakavyoendeshwa katika uchaguzi wa ndani wa vyama hivyo ambapo kuna taarifa mmoja wa vigogo amefanikiwa kupata kiasi cha dola milioni 15 zitakazomsaidia kupanga safu yake ya uongozi

Katika kutimiza mpango huo, tayari yapo mawasiliano ya mara kwa mara ya baadhi ya viongozi wakitoka Zanzibar na sehemu zingine za nchi kuja Dar es Salaaam, na imeonekana dhahiri mazungumzo yao kutowashirikisha viongozi wenzao waandamizi kwani yanalenga kafanikisha mpango huo.

Mheshimiwa Rais Dk John Pombe Magufuli, ameendelea kufanya juhudi kubwa katika kujenga nchi kwa kuimarisha utendaji na nidhamu ya utumishi serikalini, kukusanya mapato na kusimamia matumizi sahihi ya fedha, kupambana na kuzuia mianya ya rushwa pamoja na kusimamia haki, usawa na wajibu kwa raia. Mwenzetu anayaona haya kuwa ni kuufanya utumishi wa umma kaa la moto.

Juhudi hizi na nyinginezo ikiwemo ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, afya na kununua vitanda vya wazazi, kutoa elimu burekuanzia shule ya msingi mpaka sekondari na nyinginezo hazipaswi kukatishwa tama kwa maslahi ya wachache ni vyema kuziunga mkono kwa maslahi ya taifa letu

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais Dk. Magufuli madarakani, CCM inawaomba wananchi kuendelea kummunga mkono katika dhamira yake safi yakuwaondolea kero, kuboresha huduma za jamii na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Imetolewa na;-

CHRISTOPHER OLE SENDEKA

MJUMBE WA NEC NA MSEMAJI WA CCM

28/10/2016

Sumaye: Sirudi CCM hata waninyang’anye Mashamba Yangu Yote

Siku moja baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutangaza nia ya Serikali kumnyang’anya shamba Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, mwanasiasa huyo mkongwe amedai hilo halimtikisi.

Sumaye ambaye tayari ameshakabidhiwa notisi ya siku 90 kutokana na kutoliendeleza, amesema kuwa tayari suala hilo ameshaliwasilisha mahakamani na kwamba mwanasheria wake ndiye anayefahamu tarehe iliyopangiwa kesi hiyo.

“Nilienda mahakamani na ikaamuriwa kusiwe na shughuli yoyote, nasubiri tarehe ya kesi ambayo mwanasheria wangu ndiyo anaijua,” Sumaye anakaririwana MwanahalisiOnline.

Mwanasiasa huyo aliyehamia Chadema miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka jana, amesema kuwa kama CCM wanataka kumdhoofisha kwa kumnyang’anya mashamba ili arejee haitawezekana.

“Kama walidhani kwa kunifanyia hivi nitarudi Chama Cha Mapinduzi (CCM) wasahau, hata kama nilikuwa na nia hiyo sirudi,” amesema Sumaye.

Serikali imetangaza kuanza mchakato wa kumnyang’anya Sumaye shamba lake lililoko Mwabwepande jijini Dar es Salaam kwa madai kuwa ameshindwa kuliendeleza kwa muda mrefu, kinyume na matakwa ya sheria.