mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Thursday, July 7, 2016

Wakili Alberto Msando Ayachambua Maagizo ya Paul Makonda



Wakili maarufu nchini Alberto Msando amechambua maagizo ya utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambayo amekuwa akiyatoa, likiwemo suala la uvutaji hadharani wa sigara na shisha.

Tangu alipoapishwa Machi mwaka huu, Makonda amekuwa akitoa maagizo mbalimbali na mikakati yake ya kutaka kulipanga upya jiji ili kuwe na maeneo maalum ya gereji, majumba ya maduka makubwa, maeneo ya kuuza magari tofauti na huduma nyinginezo. Mengine ni kuondoa ombaomba jijini, kutaka wasiovaa kofia ngumu kwenye bodaboda washtakiwe kwa kutaka kujiua, kuhakikisha mitaa inakuwa safi, kuondoa mashoga, kufungwa maeneo yanayofanya biashara ya shisha, kuondoa majengo yasiyo na maegesho, kutatua changamoto za elimu na barabara.

Lakini Msando anachambua mikakati hiyo, akionekana kushauri kuwa elimu itumike zaidi kwa kuwa maamuzi mengine yanahitaji nchi kutunga sheria, kitu ambacho hakitawezekana ndani ya siku saba.

Akichambua maagizo hayo huku akitolea mfano wa ombaomba, Msando anahoji katika uchambuzi wake aliouweka kwenye ukurasa wa facebook, kama bado wapo au wamerudi katika baadhi ya maeneo. Anasema huenda wengi wao hawakusikia matangazo kwenye televisheni au magazeti.

Alisema sababu za ombaomba hao kutoka huko walikokuwa kuja Dar es Salaam hazijaisha na ikiwa wataondoka Dar, si kwa sababu wameyachoka maisha ya kuombaomba bali kwa sababu hawatakiwi na mamlaka.

Alihoji itakuwaje ikiwa wataondoka Dar es Salaam na kwenda Morogoro au Kibaha mjini na kuendelea kuomba?

“Nadhani tatizo bado litabaki,” anasema akipendekeza mikakati iandaliwe kote wanakotoka na watakakopokewa.

Akizungumzia usafi wa mitaa, mwanasheria huyo anasema bado ni changamoto kwa kuwa kuna maeneo bado machafu.

“Hatuwezi kufanikiwa kama tabia ya uchafu haitakoma katika ngazi za familia na mitaa. Usafi na uchafu ni tabia. Ni mazoea. Watoto wafundishwe shuleni na nyumbani kuwa wasafi. Tujenge Tabia,” anashauri.

Kuhusu ushoga, Msando anasema sheria iko wazi kwamba hilo ni kosa la jinai na adhabu yake ni kifungo, lakini shida ni jinsi ya kuwakamata na kuwachukulia hatua. “Hatuwezi kutumia vigezo vya mavazi na mwendo. Kosa siyo kusema mimi shoga. Tunahitaji kuangalia hili kwa mapana. Lazima tuzipige vita,” anasema.

Msando anasema ukamataji wa watu wasiovaa kofia ngumu una changamoto zake kutokana na askari wa barabarani nao kufanya makosa hayo.

“Juzi nilimwona trafiki amemkamata dereva wa bodaboda, halafu akapanda hiyo pikipiki bila kuvaa helmet. Sasa nikajiuliza, huyu trafiki naye akamatwe na trafiki mwingine kwa kosa la kutaka kujiua? Hili kosa lipo kisheria?”anahoji.

Mwanasheria huyo anasema usalama wa raia ni jukumu la awali la raia mwenyewe na anayekufa au kupata ulemavu ni raia mwenyewe.

“Ni vyema kumwelimisha huyu raia mwenyewe, aogope na aache kupanda bodaboda bila kuvaa kofia. Akielewa wala hatuhitaji watu magerezani,” anasema.

Pia, Msando aligusia suala la uvutaji wa shisha na kusema kuwa hiyo ni tabia ambayo vijana wengi wanaiga kwa kufuata mkumbo, wanaona sifa na usasa zaidi, hasa wanafunzi wa vyuo.

“Ndani ya siku saba tutakuwa tumepitisha sheria kupiga marufuku? Unadhani jambo kama hili linakuwa” anahoji Msando.

Post titleGesi Ya Kupikia Kuagizwa kwa Pamoja Kuanza Septemba


Serikali itaanza kutumia mfumo wa uagizaji wa pamoja wa nishati ya gesi ya kupikia (LPG), kama inavyofanyika kwa mafuta ya ndege, petroli, dizeli na mafuta taa ifikapo Septemba mwaka huu. 

Akizungumza wakati wa semina ya wadau wa sekta ya mafuta kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mkurugenzi wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Godwin Samuel alisema mpango huo utasaidia kupunguza gharama na bei ya gesi hiyo inayoanza kutumika kwa kasi majumbani. 

Samuel alisema mpango huo pia utaongeza udhibiti wa mapato ya Serikali katika sekta hiyo inayoshika kasi nchini. 

Kuhusu uagizaji wa mafuta ya ndege, petroli, dizeli na mafuta ya taa, Mkurugenzi huyo alisema mchakato unaendelea kuboresha mfumo wa sasa kwa kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau yatakayotumika kubadilisha taratibu zilizopo ifikapo Novemba, mwaka huu mikataba ya sasa itakapomalizika.

“Tunakusudia kuongeza ushindani wenye tija katika uagizaji wa pamoja wa mafuta ya ndege, petroli, dizeli na mafuta taa kwa kuongeza idadi ya kampuni kulinganisha na kandarasi zilizopo zinazofikia kikomo ifikapo Novemba mwaka huu,” alisema Samuel. 

Kuhusu elimu kwa wadau, Mkurugenzi huyo alisema Ewura inalenga kuwawezesha kujua na kuzingatia mabadiliko yanayotokea katika sekta na biashara ya mafuta ili kuwezesha kila upande kutimiza wajibu kulingana na sheria, kanuni na taratibu. 

“Changamoto zinazoikabili sekta na biashara ya mafuta hayawezi kutatuliwa na Ewura pekee bali ni kwa ushirikiano wa wadau wote,”alisema.

Post titleWatu Waliokufa Katika Ajali ya City Boy Wafikia 32


Idadi ya watu waliokufa katika ajali iliyohusisha mabasi mawili ya Kampuni ya City Boy imeongezeka na kufikia 32 baada majeruhi aliyekuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kufariki dunia.

Ajali hiyo iliyohusisha mabasi hayo wakati moja likitokea Dar es Salaam kuelekea Kahama mkoani Shinyangana lingine likitokea Kahama kuelekea Dar es Salaam, ilitokea saa tisa Jumatatu katika eneo la Maweni, Kata ya Kintiku Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Akizungumza jana Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,  Dk Ibehzi Ernest alisema kazi ya kutambua miili ya marehemu hao bado inaendelea.

Alisema hadi jana miili ya watu 25 waliokufa kwenye ajali hiyo ilikuwa imetambuliwa na ndugu zao. Dk Ernest ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Ajali, Upasuaji na Mifupa alisema kati ya maiti 25 zilizotambuliwa 12 zimechukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi.

“Wengine wametibiwa na kuruhusiwa tumebaki na majeruhi watano ambao hali zao zinaendelea vizuri,” alisema. 

Kwa siku nzima ya juzi na jana watu walikuwa wakipishana kuwatambua ndugu zao katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Dodoma. Kutokana na miili kuharibika, ndugu hao walikuwa wakirudi mara mbili kuangalia.

Wednesday, July 6, 2016

Waziri Kigwangalla: Kuanzia Sasa Lazima Kila Mwananchi Awe na Bima ya Afya


Naibu Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt. Khamis Kigwangala amesisitiza kuwa kuanzia sasa itakuwa ni lazima kwa kila Mtanzania kuwa na Bima ya afya,huku akiwatoa hofu wananchi wasio na uwezo kwamba serikali kupitia Sera ya taifa ya afya ya mwaka 2007, itakuwa tayari kugharamia matibabu ya makundi maalumu ya kijamii wakiwemo wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60, watoto chini ya umri wa miaka mitano na watu wenye magonjwa ya kudumu.

Naibu Waziri kigwangala, ameyasema hayo wakati akifunga Maadhimisho ya miaka 50 ya utume wa injili kwa waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato Kirumba Mwanza yaliyofanyikia katika uwanja wa CCM Kirumba, yakiwa yametanguliwa na zoezi la utoaji wa huduma za afya bure kwa wakazi hilo zilizofanywa na madaktari bingwa wa macho,meno,kibofu cha mkojo,tezi dume,kisukari na saratani ya shingo ya kizazi kwa siku saba mfululizo.

Sherehe za miaka 50 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo la Waadventista wa Sabato katika jiji la Mwanza mnamo mwaka 1935,lililopo chini ya jimbo la Nyanza Kusini,ambalo hadi sasa limefikisha makanisa 84 pia zimehudhuriwa na Naibu Waziri wa ardhi, nyumba na makazi Mh.Angelina Mabula, ambaye amesema kazi kubwa ya kanisa ni kuendelea kuokoa maisha ya waumini wake kiafya na kiroho pamoja na kusimamia maadili mema ndani ya jamii.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato tanzania Dk.Godwin Lekundayo, ameiomba serikali kuharakisha usajili wa hospitali ya Pasiansi inayojengwa na kanisa hilo ili iweze kuanza kutoa huduma kwa muda uliopangwa, lengo la kanisa la SDA jimbo la Nyanza Kusini ni kuifanya hospitali hiyo kutoa huduma za matibabu ya rufaa ili kuokoa maisha ya watu.

Sunday, July 3, 2016

Serengeti Boys Yafanya Mauaji...Yaipiga Shelisheli Bao Sita


Timu ya taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, imeitoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0 katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za vijana Afrika mwakani.

Mchezo wa kwanza uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Serengeti ilishinda mabao 3-0.

Katika mchezo wa jana, Serengeti iliandika bao la kwanza katika dakika ya tisa lililofungwa na Ibrahim Abdallah kabla ya Mohamed  Abdallah aliifungia Serengeti bao la pili kwa shuti kali dakika ya 43.

Asad Juma alifunga bao la tatu dakika ya 50 na Issa Makamba alifunga bao la nne kwa mkwaju wa penalti dakika ya 61 baada ya kufanyika madhambi eneo la adhabu.

Asad aliifungia Serengeti bao la tano dakika ya 70 baada ya kuwatoka mabeki wa Shelisheli na Yohana Mkomola alihitimisha kwa kufunga bao la sita dakika ya 90.

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Afichua Jipu la Kutisha


Ni jipu. Ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kusema halmashauri 34 nchini zimetumia Sh1.45 trilioni za miradi kugharimia shughuli ambazo hazikuwamo kwenye bajeti.

Profesa Assad ameyasema hayo katika mafunzo yaliyotolewa kwa watu wa kada mbalimbali kuhusu Toleo la Vijarida Maalumu vya Wananchi kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni mwaka 2014 na kukusanya maoni ya ripoti ya CAG.

“Hili limekuwa tatizo kubwa hapa nchini. Utakuta fedha zimetengwa kwa mradi fulani, badala yake wanabadilisha matumizi na kununua vitu ambavyo havina  stakabadhi,” amesema Profesa Assad.

 “Lengo kuu la fedha hizo za miradi ni kutumika katika shughuli za maendeleo na kutoa huduma muhimu za kijamii.”

CHADEMA Waapa Kutibua Mkutano wa CCM, Vijana 2000 Kupelekwa Dodoma Kwa Ajili ya Kazi Hiyo


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepanga kulisaidia Jeshi la Polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitoa zuio la mikutano ya siasa ya wazi na ya ndani nchini kote, hata hivyo CCM imepanga kufanya Mkutano Mkuu tarehe 23 Julai mwaka huu mjini Dodoma.

Kwenye mkutano huo, Dk. Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM atakabidhi mamlaka hayo kwa Dk. John Magufuli ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa chama hicho.

Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) limepanga kuzuia mkutano huo kwa madai ya kulisaidia Jeshi la Polisi kusimamia agizo lake kwa vyama vya siasa nchini.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Slaam viongozi wa Bavicha walisema, hatua hiyo ni katika kuhakikisha wanalisaidia jeshi kutekeleza amri iliyotolewa na Rais Magufuli ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020.

“Tumeandaa vijana takribani 2000 kutoka mikoa yote nchini watakaokwenda Dodoma kusaidiana na Jeshi la Polisi kutawanya mkutano usio halali wa CCM.  Kwa sababau Jeshi la Polisi limezuia mikutano yote ya siasa kwa sasa.

“Pia ni katika kuunga mkono kauli ya Rais Magufuli kwamba, hakuna mikutano ya vyama vya siasa mpaka mwaka 2020. Huu ndio msiamamo wa baraza.

“Mikutano yetu sisi kama Chadema tunazuiwa lakini CCM wanafanya. Mahafari ya chama cha mapinduzi yanafanyika. Ni jana CHASO (Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Chadema) Morogoro tumezuiwa lakini UVCCM (Umoja wa Vijana wa CCM) Mkoa wa Morogogo wamefanya na picha zipo. Hii sio haki, kama mbwai na iwe mbwai,” alisema Patrick ole Sosopi, Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo.

George Tito, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya alisema “… ni kwamba, huko mikoani vijana wameshajipanga. Wana ari kubwa ya kwenda Dodoma.

“Tumeamua kufikia hatua hii kwa sababu tumekuwa tunaona hakuna haki katika nchi hii. Kuna mahafali yanafanyika vyuo vikuu, wenzetu CCM wanaruhusiwa sisi Chadema tunakatazwa.Vijana wa Chadema wamekuwa wakikamatwa bila sababu za msingi,” alisema Tito.