mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Sunday, February 28, 2016

DK KIGWANGALA AHIMIZA JAMII KUWA NA UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA


dk hk
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla akitoa hutuba fupi wakati wa tukio hilo la kambi maalum ya matibabu ya bure kwa wananchi wote iliyoandaliwa na Care Foundation kwa kushirikiana na wadau wengine akiwemo Mbunge wa jimbo la Ilala, Mh. Mussa Hazan Zungu.
………………………………………………………………………………………………………………………………….
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla amehimiza Jamii kuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara katika hali ya kubaini matatizo yanayowakabili ilikuchukua hatua ikiwemo kupata tiba mapema
Dk. Kigwangalla ametoa kauli hiyo mapema leo Februari 28.2016, jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa mgeni rasmi katika kambi maalum ya kupima afya bure kwa wananchi mbalimbali wakiwemo wa Jimbo la Ilala kwa kuandaliwa na Care Foundation na wadau wengine wa afya ikiwemo Hospitali ya Ebrahim Haji Chartable Health Centre ambao wanasimamia kutoa huduma za matibabu kwa kushirikiana na taasisi zingine.
Akitoa hutuba yake fupi, kwa wananchi mbalimbali walifika katika tukio hilo la kupatiwa matibabu hayo ya bure, Naibu Waziri, Dk. Kigwangalla amesema Jamii wanatakiwa kuwa na maisha yenye afya hivyo zoezi la kupima afya mara kwa mara ni bora zaidi kaika kuimalisha afya ya mwili.
“Wananchi wapo na wakati mwingi wakifanya shughuli zingine na hata muda kupima afya inakuwa ngumu. Kukinga ni bora Zaidi kuliko tiba. Zoezi hili litasaidia sana wananchi wengi na tunaomba muendelee na maeneo yote ya nchi yetu.” Ameeleza Dk.Kigwangalla.
Aidha, Dk. Kigwangalla amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Hazan Zungu kwa kuwezesha kuandaa zoezi hilo kwa kushirikiana na wadau hao kwani ni mfano bora wa kuigwa na wabunge wengine pindi wapatapo nafasi ya kutumikia jamii iliyowachagua.
Pia katika zoezi hilo, Mbune wa jimbo la Ilala, Mh. Mussa Zungu na Naibu Waziri Dk. Kigwangalla walipata wasaha wa kupima afya zao pamoja na kutembelea maeneo ya kutolea huduma na kushuhudia namna huduma zinavyotolewa kwa wananchi.
Kambi hiyo ya matibabu, inatoa matibabu hayo bure kwa wananchi wote wanaofika hapo ambapo pia mbali na matibabu wanatoa huduma ya dawa huku wakitoa pia mawani kwa watu wenye matatizo ya macho. Watu mbalimbali wamekaribishwa kupatiwa matibabu hayo ambayo pia yanatolewa na madaktari bingwa wa magonjwa husika.
yi
Tukio likiendelea
DK KIGWANGALLA 65
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla akiwa katika meza ya kupima afya ya mwili ikiwemo magonjwa yasio ambukiza kama vile Magonjwa ya moyo, sukari, shinikizo la damu na mengine mengi katika zoezi linaliendelea katika viwanja vya Bustani ya jiji iliyopo mkabara na Ukumbi wa Karimjee.
Dk. Kigwangalla
Naibu Waziri wa Afya. Dk.Kigwangalla akiwa katika vipumo hivyo..
DK
Mbunge wa Ilala, Mh. Mussa Hazani Zungu, akipima afya katika zoezi hilo..
TIBA 3
Dk. Efrahim Mika Zaky wa Msimbazi Eyes Vision Center, (kushoto) akimpima macho mmoja wa wananchi waliojitokeza katika zoezi hilo linaloendelea leo jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Bustani ya jiji, mkabara na Ukumbi wa Karimjee.
TIBA
Uchunguzi wa macho ukiendelea..
TIBA3
Dk. Efrahim Mika Zaky wa masuala ya macho, akimpima macho Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla wakati wa zoezi hilo..
TIBQ667
Naibu Waziri wa Afya Dk. Kigwangalla akiwa katika kupima macho kwenye kambi maalum ya kutoa huduma za matibabu ya bure yaliyoandaliwa na Care Foundation na wadau wengine katika viwanja vya Bustani ya Jiji, Posta Jijini Dar es Salaam.
TIBA222
Naibu Waziri Dk.Kigwangalla akiwa katika moja ya sehemu ya kutolea dawa na miwani kwa watu watakaobainika kuwa na matatizo katika macho..
DK KIGWANGALLA 685
Naibu Waziri akipokea ua maalum kama ishara ya kukaribishwa katika ufunguzi huo wa kambi maalum ya matibabu ya bure yaliyoandaliwa na CARE Foundation na wadau wengine akiwemo Mbunge wa jimbo la Ilala, Mussa Hazzan Zungu.(Picha zote na Andrew Chale, modewjiblog/Mo tv).

WAZIRI NAPE AVITAKA VYOMBO VYA HABARI VYA SERIKALI KUWA VINARA WA UFICHUAJI WA MAOVU


OS1
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Nape Nnauye akiwa anakazia jambo kwa wafanyakazi wa kampuni ya magazeti ya serikali ya TSN kuhusu kuboresha kazi zao na kuandika habari zinazofichua maovu katika jamii na kusimamia haki bila kumuonea mtu.
OS2
Mhariri wa magazeti ya Daily News Bw.Charles Masele akimweleza jambo Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Nape Nnauye(hayupo pichani) mapungufu mbalimbali ya kampuni ya TSN na kumwomba waziri uyo awasaidie kuiboresha kampuni hiyo.
OS3
Mwenyekiti wa RAAWU tawi la Tanzania Standard Newspaper(TSN) Bw.Oscar Mbuza akimweleza waziri Nape(kulia) changamoto mbalimbali ya wafanyakazi.
OS4
Sehemu ya wafanyakazi wa kampuni ya magazeti ya serikali(TSN) wakimskiliza Mhe. Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Nape Nnauye(hayupo pichani).
OS5
Waziri Nape nnauye akipiga “Selfie” na mfanyakazi wa magazeti ya kampuni ya serikali ya TSN baada ya mkutano na wafanyakazi hao katika ofisi za kampuni hiyo.
OS6
Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya magazeti ya Serikali(TSN) wakifurahia picha ya pamoja na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Nape Nnauye.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye amewaasa wafanyakazi wa kampuni ya magazeti ya serikali ya Habari Leo,Daily News,SpotiLeo na Sunday News kuwa mstari wa mbele katika kufichua maovu katika jamii,kwani kwa kufanya ivyo watajijengea heshima katika jamii na kuongeza idadi ya watu kuwaletea kazi zao kwa ukaribu zaidi.
Waziri nape ameyasema hayo leo hii jijini Dar es Salaam katika ofisi za magazeti ya serikali(TSN) kwenye kikao na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
“Acheni kumumunya maneno,msaidieni Rais katika kufichua maovu ya nchi yetu ila tu msimuonee mtu bali mtende haki na hasa mkosoe ili kujenga na kwa namna hiyo mtajijengea heshima kubwa katika jamii”.
Waziri nape pia aliitaka menejimenti ya kampuni iyo kubadilisha fikara zao kwa kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara ili kampuni iyo ijitegemee vyema katika mambo yake.
Pia aliitaka menejiment ya kampuni iyo kukaa chini na RAAWU ili wahakikishe wafanyakazi wanafata taratibu za kazi na kuwaasa kushughulikia vipaumbele vya wafanyakazi hao ambavyo ni vifaa vya kazi ambavyo kutokuwa navyo inapelekea kushuka kwa morali ya kazi na pia madai ya wafanyakazi yashughulikiwe  ndani ya mwezi mmoja.
Nae Mwenyekiti wa RAAWU katika kampuni iyo Bw.Oscar Mbuza alimweleza waziri nape kuwa wanatambua haki na wajibu wa kila mfanyakazi na kwamba kumekuwa na ukiukwaji wa sheria,taratibu na kanuni kwa mtizamo wao na ivyo wanaomba yafanyiwe kazi ili kurudisha imani yao kwa viongozi wao.
Nao wafanyakazi mbalimbali wa kampuni iyo walieleza changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo kutokuwepo kwa bima ya afya,hawapandishwi cheo na kulipwa malimbikizo mbali mbali wanayoidai kampuni hiyo.
Mhe.Nape pia amehaidi kufanya vikao vya mara kwa mara na wafanyakazi wa kampuni iyo ili kuboresha mambo mbalimbali ya kampuni hiyo.

WAZIRI MKUU ANUSA UFISADI BANDARI YA MTWARA

kasl4
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua bandari ya Mtwara na kunusa harufu ya ufisadi katika utoaji wa zabuni  ya ujenzi wa gati mpya tatu.
Wazi Mkuu ambaye alikagua eneo la ujenzi wa gati hizo jana (Jumamosi, Februari 27, 2016), alisema anazo taarifa juu ya utolewaji wa zabuni hiyo na mzabuni ameshashinda lakini kuna madai kwamba watu wa manunuzi kupitia PPRA  ndiyo wanakwamisha zabuni hiyo.
Aliwaomba wabunge wa mkoa wa Mtwara washirikiane kusimamia suala hilo ili ujenzi wake uweze kuanza mara moja na kuleta ajira kwa wana Mtwara. “Ujenzi ukikamilika siyo tu ajira zitaongezeka bali hata meli nyingi zitaleta mizigo katika bandari hii na mapato ya mkoa yataongezeka”, alisema.
“Natambua kwamba kuna mpango wa kujenga gati nne ambapo moja kati ya hizo itajengwa na TPA (Mamlaka ya Bandari) lakini hizi tatu zilitangazwa na kupata mzabuni ambaye ni kampuni ya Hyundai kutoka Japan. Lakini hii kampuni imekuwa ikizungushwa bila sababu. Tutafuatilia kubaini tatizo liko wapi,” aliongeza.
“Sasa hivi tuna uwezo wa kupaki meli moja tu, lakini gati zikikamilika tutaweza kuwa na meli tatu kwa mpigo, cha msingi tusimamie maamuzi yetu kwamba lazima wafanyabiashara wa korosho watumie bandari hii kusafirisha mizigo yao na si kuipeleka kwingine.”
“Kwenye Bodi ya Korosho nako kuna majipu yanahitaji kutumbuliwa. RCC ilishakaa na kupitisha uamuzi kuwa mizigo yote ipitie bandari ya Mtwara lakini kuna watu ndani ya Bosi hiyo wanatoa vibali vya kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam. “
Alimtaka mkuu wa bandari ya Mtwara (Port Master) Bw. Prosper Kimaro awe makini na watu wa kitengo cha manunuzi katika bandari hiyo kwani kimekuwa chanzo  cha upotevu wa fedha za Serikali kutokana na ujanja wa watu wachache.
“Hapa si kuna mtu alitaka kuiba sh. milioni 300 kwa kufoji saini za wakubwa wake? alihoji Waziri Mkuu swali ambalo lilijibiwa na Bw. Kimaro kwamba ni kweli lakini uongozi uliingilia kati kabla wizi huo haujakamilishwa.
Kuhusu fidia kwa wakazi wa vijiji vya Kisiwa na Mgao ambao wamekubali kuhama ili kupisha upanuzi wa bandari hiyo,  Waziri Mkuu aliwahakikishia wabunge hao pamoja na uongozi wa bandari kwamba kiasi cha sh. bilioni 13.8/- kimekwishatengwa na Wizara na kitatolewa mapema mwezi ujao.
Alitumia fursa hiyo kusisitiza udhibiti wa bandari bubu ambazo zinatumiwa kuingiza sukari na  mchele mchezo ambao unaikosesha Serikali mapato.  “Mkuu wa Mkoa, nilikwishatoa agizo kama hilo wakati nimeenda kukagua bandari ya Tanga. Kaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nanyi pia muweke mbinu za kudhibiti upenyo huu wa kuingiza bidhaa za magendo kwa sababu hawa ndiyo wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali,” alisisitiza.
Naye, Mkuu wa bandari hiyo, Bw. Kimaro wakati akitoa taarifa ya utendaji wa bandari mbele ya Waziri Mkuu, alisema bandari hiyo ilianzishwa mwaka 1950 na imekuwa inakabiliwa na ufinyu wa gati ya kuegesha meli, vifaa vya kupakulia na kupakia mizigo na kwamba hivi sasa wamekwishapata winchi ya bandarini (harbour crane) yenye uwezo wa kubeba tani 100 na tayari wako kwenye mpango wa kujenga gati moja.

MH PAUL MAKONDA AFANIKISHA MPANGO WA KUWASAFIRISHA WALIMU KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM


MAK1
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Paul Makonda akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Lamada Posta jijini Dar es salaam leo wakati alipozungumzia mpango wa kuwasafirishwa walimu bure jijini Dar es salaam wakati wa kwenda na kurudi kazini huku akiwa ameongozana na viongozi wa vyama vya usafirishaji wa abiria jijini Dar es salaam pamoja na viongozi wa Madereva wa Daladala jijini Dar es salaam, kutoka kulia ni Makamu mwenyekiti waUmoja wa Madereva, Shabani Mdemu na katikati ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam, (Uwadar),William Masanja
MAK2
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Paul Makonda wa pili kutoka kushoto  akimsikiliza Said Mabrouk Mwenyekiti wa Chama Chama  Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es salaam wakati akizungumzia mwitikio wa wamiliki hao kuhusu kuwasafirisha  walimu ili kuunga mkono juhudi za Mkuu wa Wilaya ya Konondoni Mh. Paul makonda na Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kutoa elimu bure hapa nchini.
……………………………………………………………………………………………………………….
Moja ya jambo ambalo serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa John Pombe Magufuri imelifanya kuwa kipaumbele kikubwa kwenye mipango yake ya kimaendeleo ni suala la uboreshaji wa sekta ya elimu nchini na ndio maana serikali imeanza utekelezaji wa mpango huu kwa kufuta ada zote mashuleni.
Kimsingi ni ndoto hii ya Mheshimiwa Raisi ambayo nina hakika kila mmoja wetu anaelewa ukubwa wa faida zake kwenye ujenzi wa Tanzania mpya na yenye wasomi na wataalamu wa kila namna tena wanaopatikana bila kuzingatia hali ya kipato cha familia anayotokea mwanafunzi, iliyonifanya mimi kama msaidizi wake katika nafasi ya ukuu wa wilaya nijiulize kila wakati juu ya ushiriki wangu wa kuhakikisha inatimia kikamilifu. Maswali ambayo yamenifikisha kwenye wazo la kuboresha sekta hii kwa kuchagua kufanya jambo ambalo wakati serikali ikiendelea kupigania changamoto nyinginezo za kuboresha ajira za walimu ikiwemo upandishwaji wa madaraja na mishahara, basi na mimi katika nafasi yangu nishiriki kwenye mchakato huu mzima kwa kutoa motisha ya usafiri wa bure kwa walimu wote wanaofundisha kwenye shule za serikali zilizopo jijini Dar es Salaam.
Kwa ufupi ni kwamba, wazo hili limejengwa juu ya msingi wa sababu kubwa tatu. Moja, kwa kuzingatia changamoto za nauli za mara kwa mara wanazolazimika kuzilipa walimu ili kuyafikia kwa wakati maeneo yao ya kufanyia kazi na pili, ni kuhakikisha mimi na serikali yangu ya wilaya ya Kinondoni tunakuwa sehemu ya juhudi za Mheshimiwa Raisi za kuboresha maslahi na mazingira ya walimu ya kufanyia kazi ili matarajio ya ndoto yake anayoipigania usiku na mchana ya kutaka kuiona sekta ya elimu nchini ikikua kwa kasi yanatimia. Na tatu, ni kuwafanya walimu wa wilaya ya Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla kama watumishi wenzangu wa serikali nao wanafaidi sehemu ya matunda ya serikali yao ambayo kwa dhati imedhamiria kubadilisha maisha yao ili na wao waweze kubadilisha maisha ya vijana wetu kupitia taaluma.
Kwasababu hizo nilizozianisha hapo juu ninaomba kuwatangazia walimu wangu wa shule zote za serikali kuanzia za msingi mpaka sekondari ya kwamba, sasa watasafiri bure wanapokwenda kutufundishia wadogo zetu na watoto wao. Hii ni baada ya kufanya vikao na mazungumzo ya kina na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma kupitia vyama vyao vya Darcoboa na Uwadar na hatimaye mazungumzo hayo kuitimishwa na mkutano wa vyama vyote hivyo viwili vya wamiliki wa vyombo vya usafiri ambao kwa sauti moja wamekubali kuniunga mkono kwenye utekelezaji wa wazo langu hili.
Kipekee na kwa unyenyekevu mkubwa, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wamiliki hawa wa vyombo vya usafiri wa umma pamoja na viongozi wa vyama vya Darcoboa na Uwadar kwani walikuwa na kila sababu ya kukataa hasa ukizingatia kuwa wao ni wafanyabiashara na tena wanazo changamoto nyingi katika sekta yao ya usafirishaji, wengine wakiwa hata wamekopa kwenye mabenki ili wapate uwezo wa kufanya biashara, lakini kwenye jambo hili wote kwa umoja wao wameseme ndio na wako tayari kuanza haraka iwezekanavyo.
Utaratibu kwa walimu juu ya utumiaji wa fursa ambayo tumeipata utakuwa kama ifuatavyo:- Moja, nimemuelekeza ofisa elimu wa sekondari na shule za msingi, kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule zote za serikali zilizopo wilayani kwangu na wilaya nyinginezo za jiji la Dar es Salaam, kutengeneza vitambulisho vya shule zao vitakavyokuwa na picha ya mwalimu, jina lake kamili, jina la shule anayofundisha, namba ya simu ya mkuu wa shule husika pamoja na saini yangu mimi mwenyewe Paul Makonda ili kuepuka udanganyifu.
Nimewataka zoezi hili walifanye na kulikamilisha ndani ya wiki moja ambapo baada tu ya kukamilika itakuwa ni furaha yangu kuwatangazia walimu wote wa shule za serikali jijini Dar es Salaam kuwa, watakuwa wakipanda daladala bure ila tu kwa siku za jumatatu mpaka Ijumaa na kwa muda wa saa kumi na moja asubuhi mpaka saa mbili asubuhi na kati ya saa tisa mpaka saa kumi na mbili jioni. Ingawa, kila mwalimu atalazimika kuonyesha kitambulisho chake alichotengenezewa kwenye shule yake pamoja na kile cha ajira ya serikali.

Saturday, February 27, 2016

TAARIFA YA KUPANDA KWA BEI YA UMEME SOMA HAPA



SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limepeleka maombi kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kuomba kupandisha bei ya nishati hiyo, kinyume na matakwa ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ya kushusha bei hiyo.
 
Taarifa ya Ewura kwa umma iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa maombi hayo yamepokewa Jumatano ya wiki hii na kutaka wadau kujitokeza kujadili uhalali wa nyongeza hiyo siku mkutano huo utakapoitishwa.
 
“Mamlaka inaanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau, ili kujua uhalali wa maombi ya nyongeza ya bei za huduma iliyoyapokea kutoka Tanesco,” imeeleza taarifa hiyo.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanesco iliwasilisha ombi husika kulingana na Sheria ya Umeme namba 131, inayoitaka Ewura kufanya mabadiliko ya bei zinazotozwa na mtoa huduma mara moja kila baada ya miaka mitatu.
 
“Pendekezo la wastani wa badiliko la bei za umeme ni asilimia 1.1 kuanzia Aprili mosi 2016 na asilimia 7.9 kuanzia Januari mosi 2017,” limeeleza tangazo hilo.
 
Mapendekezo hayo japo ya kisheria, lakini yanapingana na msimamo wa Waziri Muhongo, ambaye tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo, alielezea kusudio lake la kutaka bei ya nishati hiyo ishushwe.
 
Profesa Muhongo alikwenda mbali na kuagiza Tanesco, Ewura na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kumpelekea mapendekezo ya kushuka kwa bei ya umeme kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.
 
Katika maagizo hayo, Profesa Muhongo alihoji kwa nini bei ya umeme isishuke, wakati gharama za uzalishaji wa umeme wa kutumia mafuta zimeshuka kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
 
Kutokana na maombi hayo ya Tanesco, Ewura imewataka wadau wa nishati wanaopenda kutoa maoni yao kwa maandishi, kufanya hivyo kwa kutuma maoni yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, ghorofa ya saba jengo la LAPF Pensions Fund Tower, mkabala na Kijiji cha Makumbusho, Kijitonyama Dar es Salaam.
 
Kwa watakaotuma kwa njia ya posta, wameombwa kufanya hivyo kwa kutumia Sanduku la Posta 72175, Dar es Salaam, Tanzania, simu namba (+255-22) 2123853-4; Fax namba (+255-22) 2123180; Barua pepe info@energyregulators.org au tovuti http://www. energyregulators. org.
 
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mamlaka hiyo pia, itaitisha mikutano ya wazi ili kukusanya maoni kuhusu mapendekezo hayo kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwamo Baraza la Wawakilishi wa Watumiaji wa Huduma (CCC); Baraza la Ushauri la Serikali (GCC) pamoja na wananchi kwa ujumla.