mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Sunday, November 27, 2016

KUFUATIA Agizo la Waziri wa Elimu Wanafanzi wa IFM Wavuliwa Majoho Katikati ya Mahafali

Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kimeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kwa kuwazuia wahitimu wa ngazi ya cheti na stashahada kuvaa majoho na kofia wakati wa mahafali yao.

Kitendo hicho kilitokea katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam juzi baada ya mratibu wa mahafali ya 42 ya IFM, Dk. Godwin Kaganda, kutangaza utaratibu huo licha ya wahitimu wao kuvaa majoho yao.

Dk. Kaganda alisema utaratibu huo ni kwa mujibu ya miongozo iliyotolewa na Serikali kuhusu uvaaji wa majoho, ambao unataka yavaliwe na wahitimu wa kuanzia ngazi ya shahada na kuendelea.

“Wahitimu wote wa ngazi ya cheti na stashahada hamtovaa majoho wala kofia pamoja na kwamba mlishapewa awali, tunaomba radhi kwa sababu ndiyo miongozo tuliyopewa,” alisema Dk. Kaganda.

Wiki iliyopita, Profesa Ndalichako  alipokuwa akiwatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa njia ya masafa, iliyotolewa na Wakala wa Usimamizi na Uongozi wa Elimu (ADEM) mkoani Mbeya, alisema kumekuwa na matumizi holela ya majoho suala linaloshusha hadhi yake na kuagiza yavaliwe kuanzia ngazi ya shahada.

“Siku hizi hata mwanafunzi akimaliza chekechea anavalishwa joho. Nafikiri haya majoho yangebaki kwa wanaohitimu digrii peke yake, ili hawa wengine nao watamani kufika ngazi hiyo na si kila mtu anavaa,” alisema Profesa Ndalichako.

Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 2,857 wa ngazi za cheti, stashahada, shahada, stashahada ya uzamili na shahada ya uzamili walihitimu masomo yao.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mwenyekiti wa Baraza la IFM, Profesa Letisi Rutashoga, alielezea changamoto katika utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa chuo hicho, ikiwamo kupanua miundombinu na utoaji wa taaluma.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni uhaba wa fedha za kuanza mradi wa ujenzi wa kampasi mpya ya Msata iliyopo Bagamoyo na kuiomba Serikali kuupangia Sh bilioni 2.5 katika mwaka ujao wa fedha.

Pia aliomba kuyafanyia kazi mapendekezo ya kubadilisha sheria namba 3 ya mwaka 1972 iliyoanzisha chuo hicho, ili iweze kuendana na malengo ya sasa ya uendelezaji wa chuo

No comments:

Post a Comment