LADY Jay Dee Arusha Jiwe Kigazani Baada ya Kauli ya Ruge Kuwa Walishamalizana
Wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, alidai kuwa vituo vyake vinaweza kuanza kucheza kazi za Lady Jaydee iwapo akiwaruhusu wafanye hivyo.
Kupitia Instagram, Lady Jaydee ameijibu ofa hiyo kwa dongo lililowaendea wasanii waliowahi kumshirikisha kwenye nyimbo zao lakini kwa kuogopa kuingia matatani na kituo hicho chenye nguvu nchini, walifuta sauti yake.
“Kwahiyo wale mlio omba collabo sijui feat baadae mkaenda kufuta chorus zangu mtafanyaje ? Habariiiiiiiiiii zenu buaaaaaana #SawaNaWao #TofautiNaHesabuZao,” aliandika Jide.
Ruge alitoa kauli hiyo Ijumaa iliyopita kwenye mahojiano na kipindi cha XXL.
“Tatizo ni kwamba hakuna ambacho hatujamaliza, tulimaliza, tunasubiri order. Unajua kimsingi ulipopewa order ya kwamba ‘nyimbo zangu usipige, jina langu usiseme kwenye chombo chako, vyovyote itakavyokuwa mimi sitaki kusikia hiyo kitu’ hiyo ndio order. Kwahiyo labda tukikutana, nimuombe tena [Lady Jaydee] kama tutaruhusiwa kufanya hiyo kitu,” alisema.
Ruge pia alisema ana muda mrefu hajawahi kukutana na Lady Jaydee, japo amedai ‘hata leo nikipata nafasi ya kahawa nitashukuru sana kwa huo mwaliko.’
Wiki kadhaa zilizopita Ruge na Joseph Kusaga walishinda kesi ya kuchafuliwa (defamation) iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya Lady Jaydee na muimbaji huyo kuamriwa kuwaomba radhi.
“Tunashukuru walau tulishinda ile kesi lakini at least ilitengeneza mfano wa watu kuelewa kwamba tusipende kutuhumu vitu kama watu huna uhakika. Bahati nzuri pia hata katika hiyo kesi alisema mwenyewe hajawahi kusikia tunasema, aliambiwa na watu. Lakini ni mambo yashapita hayo.”