Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete hakutumia ibara ya 45 ya Katiba kutoa msamaha kwa baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), wanaoelezwa kuamriwa kurejesha fedha walizochukua.Aidha, alisema pale ambapo kuna makosa, Rais anaweza kumsamehe mtu ambaye tayari amehukumiwa au kupewa adhabu kwa kutumia ibara hiyo.Alisema, “Mimi kwa taarifa nilizonazo Mheshimiwa Rais mstaafu hakutumia kifungu hicho,” Dk Mwakyembe alisema bila kueleza kifungu kilichotumiwa.Alisema hivyo jana bungeni mjini hapa, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) aliyetaka kujua endapo Rais aliyepita alitumia madaraka yake vibaya, alikosea au alikuwa sahihi kuruhusu baadhi ya watuhumiwa walipe fedha walizodaiwa kuzifanyia ubadhirifu kupitia akaunti ya EPA (Hawakutajwa).Pia, mbunge huyo katika swali lake la pili la nyongeza alitaka kujua ni lini watafikishwa mahakamani akieleza kuwa msamaha waliopewa haukuwa wa kikatiba na kwamba wanastahili kushitakiwa.Katika swali lake la msingi, Haji alitaka kujua iwapo Rais ana mamlaka ya kisheria kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambayo mashauri yake yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi, upelelezi au mahakamani.
No comments:
Post a Comment