Ikiwa imepita siku mbili tangu aliyekuwa mgombea wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa mwamvuli wa UKAWA, Edward Lowassa kueleza tathimni ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano chini Rais John Magufuli, ambapo alidai kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi huo, kumekuwepo na ukiukwaji wa misingi ya demokrasia na utumishi wa umma kuwa kaa la moto.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimevunja ukimya na kumjibu kwa kusema kuwa katika kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita alikuwa wa kwanza kukiuka misingi ya demokrasia. Kuhusu utumishi wa umma kuwa kaa la moto, imemjibu kuwa wanao lalamika hivyo ni wale wanaotumiwa kuficha mafisadi na wakwepa kodi.
Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka amewaambia waandishi wa habari kuwa Lowassa hastahili kuituhumu serikali ya Rais Magufuli kuwa inakiuka misingi ya demokrasia.
“Demokrasia ya kweli lazima ianze ndani ya chama, ni demokrasia ipi iliyotoa mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea kuvigharamia kwa kuamua kumteua mgombea mtunguo ambaye hajapimwa wala hajawahi kuvipigania?,” amehoji.
Ole Sendeka ameongeza kuwa “Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na kuwanyima haki yao kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kulidhihirisha usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia.”
Amesema CCM haigopeshwi na matamko ya Lowassa anayotoa katika vyombo vya habari kwa kuwa havitaiathiri na kwamba imemamua kumjibu kwa madai kuwa anapotosha umma kwa kueleza mambo yasiyo na ukweli.
Ametoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutochukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko.
“Wanasayansi wa masuala ya siasa waiangalie demokrasia ya CHADEMA na UKAWA inavyofanya kazi maana ni kihoja, watuambie njia iliyotumika kuwapata wabunge viti maalumu. Kila kiongozi aliteua maswahiba zake na wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA,” amesema.
Pia Sendeka amemtaka kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo kutoichukia serikali ya Rais Magufuli kwa kuwa inatekeleza yale aliyokuwa anayapigania.
“Chuki ya Zitto ya kuendelea kunyooshea kidole serikali ya CCM haina tija, sababu inatekeleza yote aliyokuwa akiyapigania,” amesema.
Katika hatua nyingine, Sendeka amedai kuwa CCM haijashiriki kukihujumu chama cha Wananchi (CUF) kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa kuwa kinawachonganisha viongozi wa chama hicho ili kigawanyike.
“Hatuna haja ya kuhangaika na CUF na wapanga siasa za uongozi CHADEMA, hatujashiriki kukivuruga na hatuna muda huo,” amesema.
=======
Ndugu wanahabari,
Kwa muda sasa kumekuwepo na usambazaji wa taairifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wakishirikiana na baadhi ya vyombo vya habari zinazolenga kukejeri, kudhihaki, kukatisha tama, kubeza na kudhoofisha jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Seikali zake katika kuleta maendeleo kwa Watanzania
Kumekuwepo na makala zinazoandikwa na magazeti mawili ya nje ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili na ambazo zinapotosha na kuandika habari zisizo za kweli kuhusu Tanzania
Pia, yapo magazeti mawili ya ndani ambayo yamekuwa yakitoa makala mfululizo kwa kila wiki zinazolenga kumchafua Mheshimiwa Rais na kuichafua taswira ya nchi yetu.
Tumesikitishwa na waandishi wa makala hizo walioamua kujivua uzalendo na kushiriki mpango wa kuiharibu heshima na taswira ya nchi yetu kwa maslahi ya maadui zetu wa nje na baadhi ya wanasiasa. Tunafuatilia kujua nini kinawasukuma kufanya hivyo na kwa maslahi ya nani ilhali sote ni watanzania. Je ni tama ya madaraka tu au mengine?. Hakuna anayepinga ukosoaji bali unapaswa uwe ukosoaji wenye nia njema
Ndugu wanahabari,Mtakumbuka hivi karibuni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa tuhuma za ufisadi ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, alisambaza taarifa kwa vyombo vya habari aliyoiita tathimini ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa octoba 25,2015
Katika taairifa yake, alidai kuwa alileta msisimko mpya katika siasa za Tanzania, kwamba ameshirikiana na wenzake kuionyesha nchi yetu maana ya demokrasia na kukosoa juhudi za serikali na wateule wa Rais.
Demokrasia kimsingi ni dhana inayohusisha ushiriki na kuheshimu mawazo ya wengi katika kufikia uamuzi. Ikiwa maana halisi ni hii, tunajiuliza ni ipi demokrasia aliyoionyesha Lowassa ambayo leo anajisifu kuwa nayo?
- Tulishuhudia akiwa mgombea Urais wa chama ambacho hakijui, hakushiriki kukijenga wala kutoa mchango wowote unaompa hadhi ya kupeperusha bendela huku katiba na kanuni ya chama hicho ikivunjwa. Kidemokrasia anayepewa fursa ya kupeperusha bendela ya chama chochote makini duniani ni kiongozi au mwanachama aliyethibitika kwa imani na matendo, kuzielewa, kuzitekeleza, kuzitetea falsafa, itikadi na malengo ya msingi ya chamahicho. Mgombea ni taswira halisi na alama muhimu inayoakisi dhamira ya chama husika machoni kwa wananchi.
- Demokrasia ya kweli lazima ianzie ndani ya chama, ni demokrasia ipi inayotoa mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea, kuvigharamia na walivyovitumikia kwa kuamua kumteua mgombea “MTUNGUO” (ambaye hajapimwa wala hajawahi kuvipigania). Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kilidhihirisha usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia
- CHADEMA watuambia njia iliyotumika kuwapata wabunge wa viti maalumu. Ni demokrasia gani inayotoa fursa kwa baadhi tu ya viongozi kuteua wabunge ambao wanakiwakilisha chama chote. Ambapo kila kiongozi aliteua maswahiba zake na wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA walikosa watu wanaowafahamu na kuamua kuwateua wanawake maswahiba wao ndani ya CCM. Msingi wa kawaida wa kupata wabunge wa viti maalumu ukiacha kura za maoni, kigezo kingine muhimu ni mchango wa mgombea / mwanachamahuyo katika kukijenga na kukitumikia chama chake. Yaliyotokea kwa CHADEMA kwenye wabunge wake wa viti maalumu ni mapya kwenye ulimwengu wa demokrasia. Inahitaji wataalamu wa sayansi ya siasa kufanya utafiti wa aina hii mpya ya demokrasia
Tulidhani baada ya mwaka mmoja kupita, wenzetu hawa wangelikuwa wamejifanyia tathimini, kujikosoa, kujisahihisha, na hata kufanya uungwana wa kuwaomba radhi wanachama wao kwa uvunjifu mkubwa wa misingi ya demokrasia, katiba na kanuni za vyama vyao
Tunatoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutokuchukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko, yasiwe ni nyimbo za kuburudisha au kutoa matumaini hewaq kwa wanachama na wananchi. Kanuni mojawapo ya demokrasia ndani ya vyama ni lazima ionekane katika muundo wake na katika utekelezaji wa muundo huo
Umefika wakati vyama vya siasa vinapaswa kujifunza kuuza sera ili kujenga na sio kusubiri matukio kwa ajili ya kupata huruma ya wananchi. Tunasubiri kushuhudia na kusikia demokrasia demokrasia itakavyoendeshwa katika uchaguzi wa ndani wa vyama hivyo ambapo kuna taarifa mmoja wa vigogo amefanikiwa kupata kiasi cha dola milioni 15 zitakazomsaidia kupanga safu yake ya uongozi
Katika kutimiza mpango huo, tayari yapo mawasiliano ya mara kwa mara ya baadhi ya viongozi wakitoka Zanzibar na sehemu zingine za nchi kuja Dar es Salaaam, na imeonekana dhahiri mazungumzo yao kutowashirikisha viongozi wenzao waandamizi kwani yanalenga kafanikisha mpango huo.
Mheshimiwa Rais Dk John Pombe Magufuli, ameendelea kufanya juhudi kubwa katika kujenga nchi kwa kuimarisha utendaji na nidhamu ya utumishi serikalini, kukusanya mapato na kusimamia matumizi sahihi ya fedha, kupambana na kuzuia mianya ya rushwa pamoja na kusimamia haki, usawa na wajibu kwa raia. Mwenzetu anayaona haya kuwa ni kuufanya utumishi wa umma kaa la moto.
Juhudi hizi na nyinginezo ikiwemo ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, afya na kununua vitanda vya wazazi, kutoa elimu burekuanzia shule ya msingi mpaka sekondari na nyinginezo hazipaswi kukatishwa tama kwa maslahi ya wachache ni vyema kuziunga mkono kwa maslahi ya taifa letu
Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais Dk. Magufuli madarakani, CCM inawaomba wananchi kuendelea kummunga mkono katika dhamira yake safi yakuwaondolea kero, kuboresha huduma za jamii na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
CHRISTOPHER OLE SENDEKA
MJUMBE WA NEC NA MSEMAJI WA CCM
28/10/2016