mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Tuesday, February 23, 2016

TFF, KTA ZAZINDUA PROGRAMU YA MAENDELEO YA SOKA KWA WANAWAKE

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na Taasisi binafasi ya Karibu Tanzania Association (KTA) kwa pamoja wamezindua programu ya maendeleo ya soka kwa wanawake vijana ili kuhamasisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji kijamii na kiuchumi kwa wanawake nchini itakayofadhiliwa na Shirika la Forum Syd kutoka nchini Sweden.
Uwekaji saini wa mkataba huo wa ushirikiano umefanywa na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mia Mjengwa Bergdahl, Mratibu wa Programu hiyo kutoka taasisi ya Karibu Tanzania Sweden katika ofisi za TFF zilizopo Karume.
Programu hiyo ni ya aina yake ambayo haijapata kufanyika nchini inalenga kujenga mfumo utakaotumiwa nchi nzima katika kutoa elimu na mafunzo kwa soka la wanawake kwenye maeneo ya ufundi (makocha), waamuzi (refarii), uongozi na tiba kwenye michezo.
Pia itawezesha kuendeleza vipaji kwa wachezaji wanawake vijana na kuongeza hali ya kujitambua na kujiamini kwa walengwa. Lengo ni kuongeza idadi ya wachezaji wenye ubora na viwango kwa soka la wanawake vijana katika ngazi zote, hivyo kuifanya programu hii kuwa nyenzo katika kuwawezesha wanawake.  
Kwa kuanzia kozi 20 za soka la wanawake vijana kwenye Vyuo 20 vya maendeleo ya wananchi zitaanzishwa kwenye kanda saba.  Jumla ya wanawake vijana 600 ikiwamo 30 kutoka katika kila chuo cha Maendeleo ya Wananchi watashiriki.
Katika programu hii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanashiriki kikamilifu kwa kuwezesha wanafunzi na miundo mbinu ya vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyo chini ya wizara hiyo kutumika katika kufanikisha programu hii.
Mafunzo yatatolewa sambamba na mafunzo mengine ya kawaida yanayotolewa kwenye Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi, kama vile maarifa ya jumla na mafunzo ya ufundi. 

No comments:

Post a Comment