mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Saturday, February 20, 2016

YANGA YAIBURUZA SIMBA MAGOLI 2-0 UWANJA WA TAIFA LEO, YAPAA KILELENI MWA LIGi

ya1
Wachezaji wa timu ya Yanga wakishangilia mara baada ya kufuga goli la pili katika mchezo wao wa ligi kuu kati yao na timu ya Simba zote za jijini Dar es salaam kwenye uwanja wa Taifa mjijini Dar es salaam, katika mchezo huo Yanga imeibuka na magoli 2 huku simba ikiangikia pua kwa kutoka uwanjani bila goli. 
ya4
Mchezaji wa timu ya Simba ya jijini Dar es salaam akitapatapa kuutafuta mpira katikati ya wachezaji wa Yanga wakati wa mchezo wao uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
ya5
Mashabiki wa timu ya Yanga wakishangilia kwa nguvu mara baada ya timu yao kuibuka na ushindi mnono wa magoli 2-1 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo.
……………………………………………………………………………………………………………………..
YANGA leo imeendeleza umwamba kwa Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya kuinyuka kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo wa duru la kwanza baina ya timu hizo kwenye uwanja huohuo Septemba mwaka jana, Yanga ilishinda kwa idadi kama hiyo ya mabao.
Bao moja katika kila kipindi kama ilivyokuwa mchezo wa Septemba yalitosha kuwapa furaha mashabiki wa Yanga na kuanza kuimba nyimbo za furaha kuwasifu wachezaji wao.
“Nyama ya Simba halali kwa Yanga… Yanga… nani kaua? Tambwe…Tambwe,” vilikuwa baadhi ya vibwagizo vya  mashabiki wa Yanga katika mchezo huo wa jana.
Yanga ilianza kuhesabu bao dakika ya 37 mfungaji akiwa Donald Ngoma baada ya beki Hassan Ramadhan ‘Kessy kurudisha mpira mfupi kwa kipa wake Vincent Angban na Ngoma kuuwahi na kupachika bao.
Simba iliyoanza mchezo wa jana kwa kasi kubwa na kuwapa matumaini mashabiki wake, ilijikuta muda mrefu ikicheza pungufu baada ya beki wake Abdi Banda kuoneshwa kadi ya pili ya njano iliyofuatiwa na nyekundu baada ya kumchezea madhambi Ngoma dakika ya 23.
Awali dakika ya 20 mwamuzi Jonensia Rukyaa wa Kagera alimpa kadi ya njano Banda baada ya kumchezea vibaya Ngoma, lakini dakika chache baadaye beki huyo alirudia tena kufanya madhambi na kupewa adhabu hiyo.
Dakika 15 za kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu, huku Simba ikifika mara nyingi golini ikiwa ni pamoja na kupata kona za mara kwa mara, lakini umaliziaji ulikuwa butu.
Simba ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 16 wakati shuti la Jonas Mkude lilipookolewa na beki Mbuyu Twite wakati mpira ulipokuwa ukielekea langoni huku mashabiki wa Simba wakiwa tayari wameamka katika viti kushangilia.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Amis Tambwe jana aliingia katika rekodi nyingine ya wachezaji waliopata kucheza Simba na Yanga na kufunga mabao katika kila timu aliyocheza.
Tambwe aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 73 kutokana na pasi ya Godfrey Mwashiuya, bao ambalo lilifanya mashabiki wa Simba kuanza kutoka uwanjani.
Hata hivyo bado Kiiza anaongoza katika ufungaji akiwa na mabao 16 akifuatiwa na Tambwe mwenye mabao 15 na Ngoma mwenye mabao 11.
Yanga ingeweza kuongeza idadi ya mabao, lakini washamuliaji wake wakiongozwa na Tambwe, Ngoma na Msuva walishika na papara za miguu kila walipokaribia lango la Simba.
Licha ya Simba kufungwa mabao hayo ilionekana kuzindunduka dakika za mwisho na kufanya mashambulizi ya kushtukiza, lakini bado suala la kutumbukiza mipira nyavuni lilikuwa tatizo.
Kutokana na matokeo hayo Yanga imefikisha pointi 46 na kushika uongozi wa ligi hiyo ikiiacha Simba ikiporomoka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45, baada ya jana Azam kuifunga Mbeya City mabao 3-0. Yanga ipo nyuma ya Simba kwa mchezo mmoja.
Kipigo hicho ni cha kwanza kwa Simba tangu iwe chini ya kocha Jackson Mayanja aliyerithi mikoba ya Dylan Kerr aliyetimuliwa mwezi uliopita.
Mayanja ameiongoza Simba kushinda mechi sita mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo jana ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza na Yanga akiwa kocha wa Simba.
Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’ Juma Abdul, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Mwinyi Hajji Mngwali, Pato Ngonyani, Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe Donald Ngoma na Haruna Niyonzima/Simon Msuva.
Simba: Vicent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Abdi Banda, Justice Majabvi, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto/Novaty Lufunga, Hamisi Kiiza/Danny Lyanga, Ibrahim Ajib/Brian Majwega na  Said Ndemla,
Naye Mwandishi Alexander  Sanga anaripoti kuwa timu ya JKT Ruvu na Stand United ya Shinyanga jana zilifungana bao 1-1 katika mchezo wa ligi hiyo Uwanja wa Kambarage.
Stand ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya saba mfungaji akiwa Elias Maguli kwa shuti la mbali lililomshinda kipa Shaaban Dihile.
JKT Ruvu inayoshika mkia katika msimamo wa ligi ilisawazisha dakika ya 13 mfungaji akiwa Abdulrahman Mussa baada ya makosa ya kipa wa Stand Frank Muwonge.
Nayo Toto Africans na Kagera Sugar zilitoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ambapo Toto Africans ilitangulia kufunga bao dakika ya 24 mfungaji akiwa Japhary Vedastus.
Mfungaji alimalizia kazi nzuri ya  Miraji Athumani kabla ya Kagera kusawazisha dakika ya 66 mfungaji akiwa Mbaraka Yusuph.
Nayo Azam FC ambayo ilifungwa mchezo wake uliopita, ilizinduka jana Uwanja wa Sokoine Mbeya baada ya kuifunga Mbeya City mabao 3-0 na hivyo kufikisha pointi 45 na kuchupa hadi nafasi ya pili ikitoka ya tatu.

No comments:

Post a Comment