WASIMAMIZI wa uchaguzi wa majimbo wametakiwa kuhakikisha kasoro zote zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 zinafanyiwa kazi kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu, unakuwa huru na haki.
Hayo yalisemwa na Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Idrissa Jecha wakati akifungua mafunzo ya siku sita kwa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ambayo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa marudio yenye lengo la kuwapiga msasa watendaji hao kusimamia vizuri majukumu yao kikamilifu.
Jecha alisema wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo wanakabiliwa na majukumu makubwa ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika na kuzipatia ufumbuzi kasoro zote zinazoweza kujitokeza kwa mara moja bila ya kuathiri matokeo mazima ya uchaguzi huo.
Alisema katika uchaguzi wa Oktoba 25 zilijitokeza baadhi ya kasoro zilizosababisha kuwepo kwa malalamiko kwa baadhi ya vyama vya siasa ikiwemo baadhi ya mawakala kuchelewa kupata vitambulisho vilivyowawezesha kusimamia majukumu yao.
Alisema kwa upande mwingine ZEC tayari imeyapatia ufumbuzi masuala mbalimbali ambayo katika uchaguzi uliopita yaliibua wasiwasi na hofu kwa vyama vya siasa kiasi ya uchaguzi wa marudio matarajio kufanyika vizuri.
Jumla ya mada mbili ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ikiwemo Kanuni za Uchaguzi iliyotolewa na Ofisa wa Uchaguzi Mkoa wa Kaskazini B, Makame Pandu ambaye alisema uchaguzi unakabiliwa na kanuni zake ambazo ni wajibu kwa kila vyama kuzifuata kwa ajili ya kuepuka malalamiko.
Aidha, Jafaar Jihadi aliwasilisha mada ya nafasi ya uchaguzi wa marudio, na kuwataka wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo kufahamu vizuri kwamba uchaguzi ndiyo mfumo sahihi.
No comments:
Post a Comment