mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Thursday, March 31, 2016

13 wadakwa na sare za JWTZ

Kamishna wa Polisi, Simon Sirro wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akionesha bastola na sare za Jeshi ambazo wamezikamata katika msako unaoendelea jijini.
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 13 kati yao wawili ni wanawake kwa tuhuma za kuwa na sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ). Aidha, limetoa onyo kwa watu wanaotumia vibaya majina ya viongozi mbalimbali.
Akizungumza na wanahabari jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 23, mwaka huu maeneo ya Ulongoni ‘B’ katika Manispaa ya Ilala.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya askari kupata taarifa kutoka kwa wananchi kuwepo kwa kundi la wahalifu wakijiandaa kufanya uhalifu. Alisema askari walifanya ufuatiliaji na hatimaye kuwakamata watu hao wakiwa na vielelezo mbalimbali.
Miongoni mwa vitu walivyotuhumiwa kukamatwa navyo ni sare za jeshi hilo ambazo ni suruali tatu, mashati manne, fulana mbili, viatu vyeusi jozi mbili, kofia mbili zenye nembo ya JWTZ. Pia walikutwa na pikipiki moja aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 444 AZL, mapanga mawili, sime mbili, visu na sururu mbili.
Akitoa onyo kwa wanaotumia vibaya majina ya viongozi, Kamanda Sirro alisema jeshi hilo linawatahadharisha watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara kuwa makini. Alisema watu hao hupiga simu na kutuma barua kutumia majina ya viongozi ili wajipatie fedha.
Alisema watakapokuwa na mashaka wanatakiwa kutoa taarifa katika jeshi hilo kama alivyofanya Mkurugenzi wa Kampuni ya Usangu Logistics baada ya kupokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa yeye ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Katika simu hiyo, alitakiwa kutoa punguzo la asilimia 25 za kodi na kwamba kila kampuni iliyolengwa na msamaha atatakiwa kulipa Sh milioni 25 kuboresha miundombinu.

No comments:

Post a Comment