mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Monday, March 14, 2016

Waliokopa HESLB wapewa siku 60


Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa siku 60 kuanzia leo kwa wanufaika wote wa mikopo wanaodaiwa na bodi hiyo wajitokeze ili kuanza kulipa madeni yao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, katika muda huo uliotolewa, waajiri pia wanatakiwa kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao wa kisheria wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao waliohitimu katika vyuo vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Jerry Sabi, alitoa taarifa hiyo jana kwa vyombo vya habari na kuwataka waajiri kuwasilisha taarifa zinazojumuisha majina kamili ya waajiriwa, vyuo na mwaka waliohitimu.
“Hivyo basi, taarifa hii inalenga kuwakumbusha waajiri ambao bado hawatimizi wajibu wao kisheria (kifungu cha 20) wa kuwasilisha majina ya waajiriwa wao wote ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu kwa HESLB ndani ya siku 28 tangu waajiriwe,” alisema Sabi.
Alifafanua kwamba, adhabu ya kutotekeleza wajibu huo kwa mwajiri ni faini ya Sh milioni saba au kifungo au vyote kwa pamoja. Sheria iliyoanzisha HESLB (Sura 178) (kama ilivyorekebishwa) inatoa wajibu kwa mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu na pia wajibu kwa mwajiri.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, baada ya Bodi kupokea orodha kutoka kwa mwajiri, itafanya uchambuzi kubaini wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu na kumwelekeza mwajiri kuingiza makato ya marejesho kwenye mshahara wa mnufaika na kuwasilisha makato hayo kwa HESLB.
Adhabu ya kutowasilisha makato kwa bodi ni faini ya asilimia 10 ya makato yote ambayo hayajawasilishwa na faini hii inapaswa kulipwa na mwajiri. Taarifa hiyo ya kaimu mkurugenzi, imefafanua kwamba, pamoja na wajibu wa mwajiri, wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu tangu mwaka 1994, wana wajibu wa kisheria (Kifungu cha 19 cha sheria ya HESLB), pamoja na mambo mengine, kutaarifu bodi kwa maandishi mahali alipo na kuandaa utaratibu wa kulipa deni lake la mkopo wa elimu ya juu.
Iwapo mnufaika wa mkopo atashindwa kutoa taarifa hizo, adhabu yake ni kushitakiwa mahakamani. “Aidha, HESLB inapenda kuwakumbusha wazazi, walezi na wadhamini wa wanafunzi walionufaika na mikopo kuwa wana wajibu wa kisheria (chini ya kifungu cha 22 cha sheria ya HESLB) wa kuhakikisha kuwa taarifa muhimu za mnufaika waliyemdhamini zinaifikia HELSB.”
Taarifa husika ni pamoja na mahali alipo mnufaika, majina aliyotumia wakati akipata mkopo, mwajiri wake na kuhakikisha mnufaika aliyemdhamini anarejesha mkopo wake kwa bodi. Kaimu Mkurugenzi, katika taarifa yake, alisema lengo la bodi ni kuhahakisha madeni yote yanakusanywa kuongeza uwezo wa kukopesha Watanzania wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment