mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Friday, March 11, 2016

Wizara kuwa na madaftari ya kusajili zawadi


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki

MAKATIBU Wakuu wameagizwa kuanzisha daftari la kusajili zawadi kwenye wizara zote, kuhakikisha utumishi wa umma unakuwa na uadilifu. Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki kwenye semina ya watendaji hao iliyofanyika jana Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye ufunguzi, Kairuki alisema kusajili zawadi kutasaidia kufanya tathmini ya zawadi ambazo mtumishi wa umma anapokea kutoka kwenye jamii na kuangalia kama ziko ndani ya sheria au la.
Semina hiyo ya siku moja ya maadili kwa makatibu na manaibu wao, iliandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Umma ikilenga kuwajengea uwezo katika suala zima la maadili na uwajibikaji.
Alisema baadhi ya watumishi waandamizi bado wanashawishi kupokea au kukubali, kuhamishiwa mali zenye maslahi ya kiuchumi zaidi ya kiwango kinachokubalika kinyume na Kifungu cha 12 cha Maadili ya Viongozi wa Umma ambacho kinaelekeza kiwango kinachokubalika ni Sh 50,000.
“ Hali hii inaweza kutatuliwa kwa kuanzisha daftari la kusajili zawadi ambalo litasaidia kubainisha viongozi ambao wanapokea zawadi au kitu kidogo na kuona kama zawadi hizo zinatangazwa kwa maofisa masuuli kama inavyotakiwa kisheria,” alisema.
Alisisitiza kwamba, Sheria iko wazi kuwa kiongozi wa umma, anayepokea zawadi yenye thamani inayozidi Sh 50,000, anatakiwa kuitangaza na thamani na kuwasilisha kiapo hicho kwa ofisa masuuli ambaye ataamua matumizi yake.
Kamishna wa Sektretarieti ya Maadili ya Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda alisema tangu ateuliwe, hakuna kiongozi yeyote kutoka serikali, Bunge au Mahakama ambaye ameshatangaza zawadi aliyopokea.
“Hakuna kiongozi yeyote aliyetangaza zawadi alizopokea, ingawa tumekuwa tukishuhudia viongozi wengi wakipokea kitu kidogo, zawadi na kuhamishiwa mali za kiuchumi,” alisema.
Jaji Kaganda aliwataka makatibu na manaibu wao kuchukua hatua za kuzuia wanapofanya kazi na watu mbalimbali, hususan wanasiasa. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amewataka makatibu na manaibu wao kuhakikisha wanazingatia kanuni za maadili.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi ambao wana utovu wa nidhamu. “Sitakuwa na furaha kuona mtu yeyote kati yenu anakuwa wa kwanza kumtumbua jipu, kwa wewe kuwa salama unapaswa kufanya kazi zaidi na kuhakikisha unazingatia maadili na uadilifu,” alisema.

No comments:

Post a Comment