mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Wednesday, March 16, 2016

Mwigizaji Lulu Azuiwa Kuingia Ikulu Kuonana na Waziri Mkuu...Kisa Kizima Kipo Hapa...


Imefichuka! Baada ya kuitwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa ajili ya kupongezwa kutokana na tuzo aliyopata nchini Nigeria, staa wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ alijikuta akihaha baada ya kuzuiwa kuingia Ikulu kutokana na kutokuwa na kitambulisho cha chama cha waigizaji.

Chanzo makini kililiambia gazeti hili kwamba Lulu alijikuta katika wakati mgumu kwani utaratibu wa wasanii kuingia Ikulu umebadilika, tofauti na serikali iliyopita kwani kwa sasa, wasanii wa filamu ni lazima wapitie kwenye Shirikisho la Filamu ‘TAFF’ kisha wizarani ndipo waruhusiwe kuonana na mhusika aliyemuita au anayetaka kumuona.

“Shughuli ilikuwa ifanyike Alhamis, Lulu alipofika wizarani akakutana na utaratibu huo mpya, si unajua yeye siyo mwanachama wa chama chochote cha filamu, ndiyo ikabidi aelezwe jambo hilo,” kilisema chanzo hicho.

JFKutokana na utaratibu huo, Lulu akalazimika kurudi katika ofisi za mwenyekiti wa waigizaji mkoa wa Kinondoni (TDFAA),  Ally Baucha ambapo alichukua fomu ya uanachama na kuijaza na kuirejesha siku hiyohiyo ya Alhamis iliyopita ili aweze kwenda kuonana na Waziri Mkuu siku iliyofuata (Ijumaa). “Yaani Lulu alihangaika kweli siku hiyo kwani hata siku ya kupokelewa pale Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere hakuna msanii wa TAFF aliyekwenda  kumpokea hata mmoja wala viongozi wake, hivyo hata alipopata mwaliko wa Ikulu ikashindikana kuingia bila ya utambulisho wa uanachama wa shirikisho na chama cha waigizaji mkoa anaoishi wa Kinondoni,” kilisema chanzo hicho.

Baada ya kuzinyaka habari hizo paparazi wetu alimtafuta Mwenyekiti wa TDFAA, Ally Baucha ambapo alikiri kwamba ni kweli Lulu alikwenda kuchukua fomu harakaharaka na kuijaza na kuwa mwanachama ikiwa ni baada ya kupata mwaliko wa kwenda kupewa pongezi na Waziri Mkuu.
Naye Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania ‘TAFF’, Simon Mwakifwamba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba ni kweli kwa sasa hakuna msanii anayeruhusiwa kuingia Ikulu bila kupitia kwenye shirikisho na wizarani hata kama ameitwa na nani.

“Utaratibu umebadilika sasa, msanii hata kama ameitwa na kiongozi gani ni lazima afuate utaratibu huo ndivyo tulivyokubaliana, hivyo Lulu alishindwa kwenda moja kwa moja mpaka alipokwenda kujiunga kwanza na chama cha waigizaji na kutambulika na shirikisho ndipo nikawapeleka Ijumaa iliyopita na msanii mwenzake aliyeshinda tuzo pia, Single Mtambalike ‘Richie’ na kwenda kupongezwa kwa kutwaa tuzo hizo za kimataifa.

“Wasanii wanatakiwa kuufahamu utaratibu huo kwani hata wakipita moja kwa moja lazima watarudishwa tu kwenye shirikisho, wakati wao ukifika kama Lulu naamini watajiunga tu hatumlazimishi mtu,”alisema Mwakifwamba.

Hivi karibuni, wasanii hao wawili walishinda Tuzo za African Movies Viewers Choice (AMVC) zilizofanyika nchini Nigeria ambapo  Lulu alishinda katika Kipengele cha Filamu Bora ya Afrika Mashariki (Mapenzi ya Mungu) huku Richie akichukua kwenye Kipengele cha Filamu Bora ya Kiswahili Afrika Mashariki (Kitendawili), tukio lililofanyika Nigeria wiki iliyopita.

No comments:

Post a Comment