mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Sunday, March 13, 2016

K AMA MZAZI: WalimuAMA 8 na mapenzi ya wanafunzi, inasikitisha



SIKUAMINI mara moja kile nilichokuwa nasoma katika gazeti juu ya habari inayohusu walimu wanane wa shule ya sekondari iliyoko ndani ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, kuwa wanatuhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi wao.
Kinachomshangaza zaidi Kama Mzazi ni ukweli kwamba kashfa na aibu hii ya walezi hao wa watoto wetu, ni idadi yao kubwa kutuhumiwa kwa vitendo hivyo tena katika shule moja! Taarifa zinaonesha kwamba walimu watano walikuwa bado wanafundisha katika shule hiyo ya sekondari ya Mihama huku wengine watatu wakiwa wameshahamishiwa shule nyingine kutokana na tuhuma hizohizo za kufanya mapenzi na wanafunzi wao.
Najua hizi ni tuhuma tu, na huenda hata wakawapo wanaosingiziwa, lakini pia waswahili wanasema ‘lisemwalo lipo’. Ndio maana Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, kwa ujasiri na busara aliamua kuunda tume kufuatilia malalamiko ya wananchi juu ya tuhuma hizo.
Tume ikaonesha kwamba ‘lisemwalo lipo’, na ndipo akaamuru kukamatwa kwa watuhumiwa ili kufikishwa katika mikono stahiki, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake. Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978, kufanya mapenzi na mwanafunzi ni kosa la jinai na ndicho tunachotarajia kuona watuhumiwa wote katika kashfa hii ya aibu, wafikishwe mahakamani ili waweze kupata wanachostahiki.
Hakuna ubishi kwamba kila kazi ina miiko yake na taaluma ya ualimu pia ina miiko yake na hivyo Kama Mzazi kwa tukio kama hilo, ambalo bila shaka linapingana na miiko na maadili ya malezi kwa watoto wetu, kwa kiasi kikubwa wamewaangusha wanataaluma wenzao, yaani walimu.
Kimsingi karibu kila mtu katika jamii yoyote makini, anawaheshimu na kuwategemea, siyo tu kwa sababu wao ni walimu lakini pia wao ni walezi wazuri na wa kutegemewa wa watoto wetu. Wao ndio hukaa na watoto wetu kwa muda mrefu kuliko sisi wazazi tunaokuwa wakati huo tuko kwenye mahangaiko mengine.
Haiingia akilini kuona kwamba hawa wachache wenye uchu na tamaa iliyopitiliza wawaharibia wenzao kwa maelefu katika taaluma hii ambayo hakuna mtu wala taifa linaloweza kuibeza. Watoto wetu kwa mujibu wa taarifa ya kamati walitumbukia katika mtego wa walimu hao kwa kuwarubuni kuwapatia fedha na upendeleo kwenye majaribio ya masomo.
Ni jambo la kushangaza lakini ndiyo hivyo tena limeshatokea. Haya yanatokea katika manispaa ya jiji kubwa la Mwanza, mahali ambapo kila aina ya huduma ambayo walimu hao wanane wangetaka wangeweza kuipata.
Nadharia ni kwamba mitaani kuna wanawake wengi ambao pengine wanatafuta wanaume, kwanini wasiende huko hadi kurubuni mabinti wadogo ambao hata akili zao hazijapevuka vya kutosha kiasi cha kupambanua vyema zuri na baya?
Hivi tujiulize, kama haya yanatokea katika jiji la Mwanza, hali ikoje katika shule ambazo zipo nje ya miji na hata vijijini kabisa? Uhusiano wa walimu na wanafunzi wao wa kike na hata wale wa kiume ukoje?
Wananchi wa Ilemela hususani wale waliotoa bila uoga malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuhusu vitendo vya kinyama vya walimu kufanya mapenzi na wanafunzi wao badala ya kuwafundisha, wanastahili pongezi za aina yake kutoka kwa Kama Mzazi.
Ujasiri huu wa wazazi wa Ilemela hauna budi kuchukuliwa pia na wazazi wengine na walezi nchini kote kutokuona haya pale wanapobaini walimu wetu kwa makusudi wanakiuka maadili yao kama walimu na walezi ili hatua zichukuliwe kudhibiti kama siyo kukomesha udhalimu wa aina hii. Hili linawezekana, tushikamane na kushirikiana kukabili ukatili na udhalimu huu.

No comments:

Post a Comment