mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Sunday, March 13, 2016

Majaliwa atuhumu uingizwaji wahamiaji holela


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua pazia kuashiria uzinduzi wa kiwanda cha maji cha Bunena Spring Water, Bukoba akiwa kwenye ziara yake mkoani Kagera jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameishukia Idara ya Uhamiaji nchini akiituhumu kuruhusu uingizaji holela wa wageni mkoani Kagera. Amesema ongezeko hilo la kiholela la wageni hao ni hatari kwa ustawi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana mjini Bukoba baada ya kupokea taarifa ya mkoa kutoka kwa mkuu wa mkoa, John Mongella, alipoanza ziara ya siku nne mkoani humo. Alisema upo udhaifu mkubwa katika kudhibiti uingiaji holela wa wageni katika wilaya za Missenyi, Kyerwa, Ngara na kidogo Biharamulo, hali inayotishia ustawi wa wilaya hizo, mkoa na Taifa.
"Uhamiaji mmekuwa chanzo cha kuingia watu kuholela. RIO (Mkuu wa Uhamiaji wa Mkoa), na wenzako wa wilaya mbadilike mara moja kulinda nchi," alisema Majaliwa. Alisema uingiaji holela wa watu utaleta matatizo makubwa ikiwamo kuhatarisha usalama wa nchi, kuongeza idadi ya watu na ongezeko la bajeti hivyo kuathiri utoaji wa huduma kwa Watanzania.
Alisema mipaka ya nchi inapaswa kulindwa na kudhibitiwa. Aidha, alisema kumekuwa na mauaji ya wananchi Watanzania katika ranchi ya Missenyi ambayo kuna mifugo kutoka nje.
Aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Uhamiaji kudhibiti hali hiyo. "Serikali isingependa kurejesha ile operesheni ya mwaka 2012 na 2013. Ikibidi tutaanzisha tena," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

No comments:

Post a Comment