“KAMA Sheria ya uanzishwaji wa mabaraza ya Kata namba saba ya mwaka 1985 itatekelezwa ipasavyo, kuanzia mahakama za mwanzo hadi Mahakama Kuu, hakutakuwa na mlundikano mkubwa wa kesi zinazosubiri kusikilizwa.” Ni kauli ya Jobu Mwalukosya, Wakili na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakati wa mahojiano na mwandishi wa makala haya.
Mahojiano hayo yaliendelea namna hii: Mwandishi: Nini lengo kuu la serikali katika kuanzisha mabaraza ya kata kisheria? Mwanasheria: Mabaraza haya yalianzishwa mwaka 2002. Lengo ni kuwarahisishia wananchi hasa waishio vijijini kupata huduma za kisheria kwa urahisi na haraka zaidi; lakini pia kupunguza mlundikano wa kesi hasa ndogo kwenye mahakama za kawaida sambamba na kupunguza utaalamu wa kisheria kwa kesi ndogo ambazo kimsingi hazihitaji utaalamu wa kisheria.
Serikali iliiongezea makali sheria ya mabaraza ya kata kwa kutunga na kuanzisha sheria namba mbili ya mwaka 2002 inayohusu mabaraza ya ardhi. Sheria hii ya mabaraza ya ardhi iliongezewa baada ya serikali kuona kuwa, migogoro ya ardhi inayohusu mashamba, viwanja, mipaka na majengo ilikuwa ikiongezeka siku hata siku tofauti na ilivyokuwa katika miaka michache baada ya uhuru. Mwandishi: Ni zipi ngazi za mabaraza ya ardhi ya kata?
Mwanasheria: Kwa kawaida, baraza lina ngazi ambazo ni Baraza la Ardhi la Vijiji ambalo kazi yake ni usuluhishi. Baraza la Ardhi la Kata ambalo linasuluhisha na kutoa hukumu au kuendesha kesi, Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, na Mahakama Kuu kitengo cha ardhi. Mwandishi: Je, kuna muundo wowote unaoyatambulisha mabaraza haya kwa jamii? Mwanasheria: Muundo wa mabaraza ya kata umejikita katika sheria zote mbili; yaani sheria namba saba ya mwaka 1985 na namba mbili ya mwaka 2002.
Kwa pamoja zinatamka bayana ambapo kila kata itakuwa na Baraza la Kata ambalo litakuwa na wajumbe wanane wanaochaguliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika. Aidha, Sheria Namba Saba ya mwaka 1985 inasema, wajumbe wanane bila kuzingatia jinsia ila Sheria Namba Mbili ya mwaka 2002 inasisitiza kuwa, kati ya wajumbe hao wanane, wajumbe watatu lazima wawe wanawake.
Mwandishi: Ni utaratibu gani unaozingatiwa wakati wa vikao vya mabaraza hayo? Mwanasheria: Ili vikao vifanyike kihalali, lazima akidi itimie kwa mujibu wa sheria zote mbili ambazo zinatamka wazi kuwa, baraza linaweza kuendesha vikao vyake kuanzia wajumbe wanne hadi wanane. Hii ni kusema kuwa, chini ya wajumbe wanne, vikao na maamuzi au hukumu zake itakuwa ni batili.
Mwandishi: Ni watu gani wenye sifa za kuwa wajumbe katika mabaraza ya kata? Mwanasheria: Siyo kila mtu anaweza kuwa mjumbe katika Baraza la Kata. Kuna kanuni na taratibu za kufuata ambazo zinaeleza kuwa, mjumbe yeyote wa Baraza la Kata lazima awe ni raia wa kijiji, mtaa au kitongoji ndani ya kata husika. Awe mtu mzima kuanzia miaka 18 na kuendelea.
Awe ni mtu mwadilifu, msikivu, mwenye ushirikiano na wenzake, awe ni mtu mwenye akili timamu; tena mtu mwenye hekima, busara na mtunza siri. Baadhi ya watu ambao hawatakiwi kuwemo kwenye mabaraza hayo ni pamoja na mfanyakazi yeyote wa serikali, mjumbe wa serikali ya kijiji au mtaa, Mbunge, Wakili au Mwanasheria yeyote, mfanyakazi wa Mahakama (hata kama amestaafu), Diwani na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji au mtaa.
Mwandishi: Ni utaratibu upi unatumika kumpata Katibu wa Baraza la Kata? Mwanasheria: Kuna namna ambayo Katibu wa Baraza la Kata anapatikana na siyo kiholela. Kila Baraza la Kata litakuwa na Katibu wa baraza ambaye yeye si mjumbe wa Baraza la Kata. Hata hivyo, hataruhusiwa kuhojiwa, kupiga kura katika kufikia maamuzi ya baraza husika.
Lazima awe mtu mwenye elimu ya kutosha kwani yeye ndiye mtaalamu wa baraza ambaye kimsingi, kazi zake zitakuwa ni kuandika kila kinachozungumzwa na wadau na kinachohojiwa na wajumbe tu. Majukumu mengine ya Katibu ni pamoja na kuandaa mwito wa kuitwa shaurini na kupeleka majalada ya kesi mahakama za mwanzo na Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya.
Mwandishi: Upi muda maalumu wa kukaa madarakani kwa wajumbe wa baraza? Mwanasheria: Wajumbe watakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu, lakini mjumbe anayefaa anaweza kuchaguliwa tena. Tofauti na wajumbe, Katibu yeye hukaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano na anaweza kuchaguliwa tena pale itakapoonekana anafaa.
Mwandishi: Ni kesi zipi ambazo mabaraza ya kata hayana mamlaka ya kisheria kuzisikiliza? Mwanasheria: Mkanganyiko huanzia hapa. Ndiyo maana kutokana na mabaraza ya kata yaliyo mengi kukosa uelewa sahihi wa masuala ya kisheria, wamejikuta wanasikiliza kesi ambazo hawana mamlaka nazo. Kisheria, mabaraza hayo hayaruhusiwi kuzisikiliza kesi za mauaji, jaribio la kuua au kujiua, wizi wa kutumia silaha, mirathi, talaka, kutenganisha ndoa, ubakaji, mimba kwa watoto wa shule, dawa za kulevya, wahamiaji haramu, uhaini, ujangili na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Mwandishi: Changamoto zipi ambazo ofisi yako inazipitia zinazochangia matatizo ya kisheria eneo lako la kazi? Mwanasheria: Zipo nyingi, ila baadhi ni zile zinazochangia migogoro isiyo ya lazima kutokana na kukosekana kwa semina kwa mabaraza hayo ili yatekeleze majukumu yake vizuri. Kwa mfano, kwa mara ya mwisho ilifanya semina Desemba 2008, miaka saba iliyopita.
Kwa kawaida, huwa inatakiwa kufanyike semina kila baada ya miaka mitatu. Semina nyingine ilitakiwa ifanyike Desemba 2011, na nyingine ilitarajiwa ifanyike Desemba 2014 lakini zote hizo hazijafanyika kutokana na ukosefu wa fedha. Ili kunusuru hali isiwe mbaya zaidi, ambacho tumekuwa tukifanya hapa wilayani na wenzangu ni kujaribu kuwashauri baadhi ya waheshimiwa madiwani kujitolea kuleta wajumbe wao wilayani au kutupeleka wataalamu wa sheria kwenye kata zao kutoa elimu ya sheria hususani katika mabaraza ya kata angalau katika kiwango cha utangulizi.
Mwandishi: Kwa kutumia mbinu hiyo mbadala mmefanikiwa kwa kiasi gani ukilinganisha na maeneo yale ambayo bado hamjayafikia? Mwanasheria: Mpaka sasa, kata ambazo tulizipatia huduma hiyo ya kisheria kwa utaratibu huo wa ushirikiano na madiwani na wadau wengine, ni kata za Kikolo, Kihungu, Mpepai, Utiri, Matiri, kata zote za Bonde la Hagati, Langiro, Mpapa, Maguu, Mapera, Mikalanga, Kambarage, Kigonsera, Mbinga Mjini na Bethlehemu.
Hata hivyo, ni eneo dogo tulilofanikiwa kulifikia likilinganishwa na idadi ya kata zote 66 za Wilaya ya Mbinga. Mwandishi: Nini matarajio ya ofisi yako siku za usoni; na pengine umejipangaje kuifikisha elimu ya kisheria kwa wananchi pamoja na changamoto zilizopo? Mwanasheria: Kwa taarifa nilizonazo, ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, tunayofanya nayo kazi kwa karibu inaangalia uwezekano wa kuandaa bajeti kulingana na hali itakavyokuwa katika mwaka wa serikali wa bajeti ili ikiwezekana semina za kuyajengea uwezo mabaraza ya kata hasa katika kata mpya zipewe kipaumbele na jamii kwa ujumla.
Mwandishi: Mwito gani unatoa kwa wadau wa sheria nchini na jamii kwa ujumla? Mwanasheria: Nawashauri wadau wote wa sheria nchini na jamii kwa ujumla, kujizoeza kuendeleza na kusimamia utamaduni wa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ili tuwe na jamii iliyostaarabika.
Naamini hayo yakifanyika inavyotakiwa wananchi wataondokana na upotevu wa muda mwingi katika migogoro inayotokana na kutokujua sheria na badala yake muda huo watautumia katika shughuli za uzalishaji mali.
No comments:
Post a Comment