mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Friday, March 11, 2016

Rais wa Vietnam aahidi kuisaidia Tanzania


Rais Truong Tan Sang wa Vietnam akihutubia wakati wa hafla iliyoandaliwa na Rais John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam juzi.

RAIS wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Truong Tan Sang amevutiwa na jitihada pamoja na mikakati ya Serikali ya Tanzania kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda. Ameahidi kusaidia Tanzania kufikia malengo yake hayo kwa kuitangaza katika mataifa mbalimbali duniani ili kuvutia wawekezaji zaidi.
Rais Sang alisema hayo Dar es Salaam jana wakati alipotembelea Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) inayojulikana kama Benjamin William Mkapa, na kukagua kiwanda cha kutengeneza kadi maalumu za kielektroniki cha DZ Card Africa Limited. Alisema anaamini kuwa uanzishwaji na upanuzi wa ukanda huo Tanzania nzima, ndio njia bora ya kuhamasisha uwekezaji na kukuza sekta ya viwanda.
Alisema nchi yake pia ilipitia wakati ilipopambana kukuza uchumi wake na sasa imefanikiwa na sekta ya viwanda nchini humo imeimarika. “Nawapongeza Watanzania kwa mpango huu na ninawaahidi sisi kama marafiki zenu wa karibu tutawasaidia kuwatangaza ili kupata wawekezaji wengi zaidi. Nitakapohudhuria mikutano ya kimataifa nitakuwa sauti yenu na ninawahakikishia wawekezaji watakuja kwa wingi,” alisisitiza.
Alisema nchi yake ilipokuwa katika harakati za kukuza sekta ya viwanda nayo ilianzisha mpango huo wa EPZA ulioanza kwa maeneo takribani 10 hadi 20 ya ukanda huo lakini sasa nchi hiyo ina zaidi ya maeneo hayo takribani 150. Alisema mwanzoni nchi yake iliwawekea masharti wawekezaji katika ukanda huo, kuhakikisha wanapozalisha bidhaa zao wazitafutie soko la nje kwa asilimia 100.
Alisema kadri uchumi wa nchi hiyo ulivyokuwa ukiimarika ndivyo, nchi hiyo ilivyowafungulia njia na sasa wawekezaji hao wanauza bidhaa zao kwa wateja mbalimbali ndani na nje ya Vietnam.
“Naamini mtafikia malengo yenu, nimefurahi kusikia kuwa mpango huu sasa umeweza kuvutia uwekezaji unaofikia dola bilioni 1.3 na kwamba mmepanga kuhakikisha uwekezaji huo kwa siku zijazo utaongezeka na kufikia dola za Marekani bilioni 10, lakini pia mamlaka hii imefanikiwa kutengeneza ajira takribani 36,000 hadi sasa haya ni mafanikio makubwa,” alisema.
Rais huyo wa Vietnam alikiri kuwa Tanzania ni moja ya nchi zilizobahatika kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kuzungukwa na masoko mengi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).
Aidha alisema pamoja na upatikanaji huo wa soko, Tanzania imebarikiwa kwa kuwa na rasilimali nyingi, hali itakayorahisishia wawekezaji katika uzalishaji wa bidhaa zao katika kiwango kinachotakiwa hali ambayo pia itaongeza mapato ya nchi. “Vietnam tulipoanzisha EPZA tulizingatia suala la mapato na ndiyo maana tulianza na uwezekezaji wa takribani dola za Marekani bilioni 10 lakini hadi sasa tuna uwekezaji wa zaidi ya dola za Marekani bilioni 150,” alifafanua.
Rais Sang alisema katika ziara yake hiyo kwenye Ukanda huo wa EPZA eneo la William Mkapa jijini Dar es Salaam, amebaini kuwa hakuna mwekezaji kutoka Vietnam na kwamba mwekezaji pekee kutoka nchini mwake, ni kampuni ya simu za mkononi ya Halotel ambaye naye hayumo ndani ya ukanda huo.
“Naamini mafanikio ya kampuni ya Halotel hapa nchini kwenu ndiyo itakuwa chachu ya wafanyabiashara wengine wa Vietnam kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika ukanda huu wa EPZA,” alisema.
Alisisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa maeneo ya kiuchumi huku akitolea mfano nchini kwake ambako alisema wapo mawaziri wengi wanaosimamia maeneo ya viwanda, biashara na uwekezaji hali iliyochangia nchi hiyo kupata mapato ya takribani dola za Marekani bilioni 200 kupitia maeneo hayo.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, alisema ukanda wa EPZA unaomilikiwa na Serikali ulianzishwa kwa lengo la kuvutia wawekezaji kutoka nje, kukaribisha teknolojia za kisasa, kuongezea nchi mapato kupitia kodi lakini pia kutengeneza ajira za kutosha kwa Watanzania.
Alisema pamoja na EPZA ya Mabibo, jijini Dar es Salaam, Serikali iko kwenye mchakato wa ujenzi wa eneo lingine wilayani Bagamoyo mkoani Pwani. Pamoja na kutenga maeneo ya viwanda vikubwa na vidogo, pia litakuwa na bandari kubwa yenye uwezo wa kuhifadhi kontena takribani 10,000 na uwanja wa ndege.
Maeneo mengine yatakayoanzishwa ni Kigoma, Morogoro, Kagera, Mtwara, Songea na Bunda. “Lakini pia malengo yetu ni kuhakikisha mpango huu unafikia mikoa yote nchini kwa sababu ina faida kubwa ikiwemo ajira.
EPZA ya Dar es Salaam tayari imetengeneza ajira 36,000 ile ya Bagamoyo inatarajiwa kutengeneza ajira 500,000. “Ndio maana tumewaalika hawa wenzetu wa Vietnam ili watupatie ujuzi wao na sisi tuweze kukua kiuchumi kama wao.
Hawa hali yao ya maisha ilikuwa kama sisi lakini kupitia taratibu hizi tunazopitia wamefanikiwa kufika hapo walipofika. Tayari jana (juzi) Rais John Magufuli amenitaka mimi na Katibu wangu kwenda Vietnam kujifunza zaidi,” alisisitiza.
Alimuomba Rais wa Vietnam kuwahamasisha wafanyabiashara nchini kwake, waje wawekeze nchini akisisitiza kwamba zipo fursa nyingi za uwekezaji zitakazowapatia faida .
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA Joseph Simbakalia, alisema eneo hilo la EPZA lililopatiwa jina la Rais wa Awamu ya Tatu William Mkapa, ndio eneo la kwanza la mradi huo, unaotarajiwa kusambaa nchi nzima ili kuongeza fursa zaidi ya uwekezaji.

No comments:

Post a Comment