mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Saturday, March 12, 2016

Majipu tisa yaliyoiva Dawasco yatumbuka



WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge amewasimamisha kazi kupisha uchunguzi vigogo tisa wa Kampuni ya Maji Safi na Taka (Dawasco) na kutaka aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Jackson Midala kusakwa na kuchunguzwa na ikibainika alihusika kwenye ubadhirifu wa maji, afikishwe mahakamani.
Kadhalika,Waziri Lwenge ameitaka Bodi ya Dawasco, kuchunguza tuhuma za wizi wa maji zinazofanywa na baadhi ya watendaji wa kampuni hiyo kwa kuwaunganishia maji bure kampuni na viwanda kadhaa jijini Dar es Salaam na kulipwa ujira kila mwisho wa mwezi na viwanda hivyo.
Waziri Lwenge alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Dawasco kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe, kuona utendaji wao na kuzungumza na watumishi hao.
Pia ameitaka bodi hiyo kuchunguza Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na kampuni nyingine pamoja na viwanda jijini Dar es Salaam kama wana akaunti za maji ya Dawasco na kwamba madai ya kuwa wao wana visima vyao vya maji, lazima ukweli upatikane.
Alisema kama kampuni inasema ina visima vyake binafsi vya maji, ni lazima wawe na kibali walichopata kutoka Wizara ya Maji, kinachowaruhusu wao kuchimba na kinaonesha kiwango cha maji, na kwamba kuna madai mengi ya kampuni na viwanda kuwa na visima vyao, ila wizara haifahamu.
“Kama unadai una kisima cha maji cha kwako kibali kinatolewa na wizara yangu, sasa yapo madai mengi viwanda vinasema vinatumia maji yao, ila zipo taarifa kwamba wanajificha kwenye hilo na ukweli ni kwamba wanaiba maji ya Dawasco, sasa lazima mchunguze hayo,” alisema Lwenge.
Waliosimamishwa kazi ni Meneja Rasilimali Watu, Mvano Mandawa, Meneja Ufuatiliaji na Tathmini, Reinary Kapera, Teresia Mlengu, Emmanuel Guluba, Peter Chacha, Fred Mapunda, Reginald Kessy, Jumanne Ngelela na Bernard Nkenda.
“Sehemu kubwa ya upotevu wa maji ni wizi unaofanywa na wezi ambao ni baadhi ya viwanda na kampuni kubwa kwa kushirikiana na watendaji wa Dawasco, tuna taarifa na kila mwisho wa mwezi wako kwenye ‘payroll’ wanaenda kuchukua malipo, hawa ni majipu lazima yatumbuliwe,” alisema Waziri Lwenge.
Mara baada ya kusomewa taarifa fupi ya utendaji kazi wa Kampuni hiyo kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja, Waziri Lwenge alitoa maagizo hayo na kusema pamoja na Kampuni kuwa na malengo mazuri, lakini ni lazima ifanyiwe mabadiliko ili kupata watendaji waadilifu.
Alisema upotevu wa maji hivi sasa ni asilimia 47 na kwamba maji hayo yanapotea katika mazingira tatanishi na kuikosesha kampuni hiyo mapato. Strabag Alitoa mfano mzuri wa Kampuni ya Ujenzi wa Barabara ya Strabag, ambayo ilipewa zabuni ya kujenga barabara za mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), kwamba tangu kampuni hiyo ianze kufanya kazi hadi sasa, haijalipa Dawasco bili ya maji iliyotumia.
“Strabag walifanya wizi wa maji, wamejenga barabara lakini hakuna malipo yoyote waliyofanyika Dawasco, wanadaiwa zaidi ya Sh bilioni 2.9 pamoja na faini na natoa siku 14, wawe wamelipa vinginevyo wakamatwe wafikishwe mahakamani.
Waziri Lwenge alisema Serikali haiwezi kufanya kazi na wabadhirifu ambao wako ndani ya taasisi, kampuni au mashirika yake na kusisitiza kuwa ni lazima watendaji wasio waaminifu waondolewe ili kuleta ufanisi nchini.
“Tunafanya mageuzi ili tufanye kazi kwa ufanisi na lazima tuwe na watendaji waadilifu na wenye maadili, si wanaoangalia maslahi binafsi,” alisema Lwenge. Waziri Lwenge alitoa wiki mbili kwa bodi hiyo kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo na zile za wateja wakubwa wa Dawasco kutokuwa na akaunti za maji, ili kuthibitisha ukweli wa madai hayo.
Maagizo mengine ni kuitaka Dawasco ifikapo Juni, mwaka huu kuhakikisha wamefanikiwa kupunguza upotevu wa maji kwa asilimia 30 na ifikapo 2020 upotevu huo uwe chini ya asilimia 20.
Awali Ofisa Mtendaji wa Dawasco, Luhemeja alisema changamoto kubwa ya Dawasco ni upotevu wa maji na kubainisha katika maeneo 10 wanayohudumia maji Dar es Salaam na Pwani, Magomeni ni eneo korofi kwa wizi wa maji.
Alisema eneo hilo hivi sasa limebainishwa na wameweka mtandao ambao kuanzia mwisho wa mwezi huu, utabaini wezi wote lakini pia hatua nyingine walizochukua ni kuweka vituo vya kuuza maji kwenye eneo korofi, vinavyosimamiwa na jamii ya eneo husika.
Alisema kwa miezi kadhaa sasa, tangu kuanza kwa huduma hiyo wameweka vituo 47 vya kuuza ambavyo vimefungiwa mita na wauzaji hutakiwa kulipa Dawasco bili ya maji baada ya kuwauzia wateja wadogo wadogo.
Ofisa Mtendaji huyo mpya wa Dawasco, alisema kwa kipindi cha muda mfupi tangu aingie kwenye kampuni hiyo, wamefanikiwa kuongeza mapato ya maji kutoka Sh bilioni 2.9 mwaka jana hadi kufika Sh bilioni 7.1 Januari mwaka huu.
Aliongeza kwamba lengo lao ifikapo Juni mwaka huu, ni kukusanya Sh bilioni 12 kwa mwezi na hiyo ni kutokana na kuweka mifumo imara na dhabiti ya kufuatilia mita za maji na masharti waliyopewa mameneja wa maeneo husika ya kampuni hiyo.
Dawasco hivi sasa ina wateja waliounganishiwa mita zaidi ya 151,000 na lengo lao ni kuongeza idadi ya wateja baada ya kuongeza uzalishaji na usambazaji wa maji hasa baada ya kuimarika kwa mitambo miwili ya maji ya Ruvu Chini na Juu.

No comments:

Post a Comment