WATANZANIA wiki iliyopita hawakutoka na furaha kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam baada ya timu yetu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu ‘Twiga Stars’ kufungwa mabao 2-1.
Mchezo huo unaifanya Twiga Stars ihitajike kushinda mabao 2-0 zitakaporudiana nchini Zimbabwe wiki ijayo ili iweze kufuzu hatua inayofuata ya michuano hiyo ya kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa wanawake.
Mechi ya marudiano itachezwa Zimbabwe Machi 18 mwaka huu, ambapo timu itakayovuka raundi hiyo itamenyana na mshindi kati ya Zambia na Namibia. Fainali za michuano ya Afrika ya soka kwa wanawake zimepangwa kufanyika Cameroon baadaye mwaka huu. Wapo baadhi ya mashabiki matokeo hayo yaliwakatisha tamaa na kuona kwamba tayari Twiga imetolewa ingawa katika soka kwa kawaida huwezi kutabiri namna hiyo.
Kwanza tunawapongeza wachezaji wa Twiga kwa kupambana kadri walivyoweza na tunasisitiza kwamba wakijipanga vizuri wanaweza kwenda kufanya maajabu ugenini. Tunasema ni mchezo ambao Twiga ikijipanga vizuri kama tulivyosema ushindi utapatikana na hatuna shaka itajiandaa vilivyo na itashinda.
Lakini Twiga Stars haitashinda kwa maneno au kwa kuandikwa vizuri magazetini au kwenye redio na televisheni, bali ni kwa juhudi uwanjani na sio vinginevyo, maana matendo hukidhi haja kuliko maneno maridhawa.
Ushindi wa Twiga Stars ni wa wote, utaitangaza nchi, tunaomba Watanzania tushirikiane kuiunga mkono timu yetu kwa hali na mali. Kwa upande wao wachezaji nao wahakikishe hawafanyi makosa ambayo yatawapa mwanya adui, maana soka ni mchezo ambao ukifanya makosa mwenzako akiyatumia utajuta.
Tunawasihi Watanzania tuzidi kuiunga mkono Twiga Stars, maana wenzetu nchi nyingine linapokuja suala la kimataifa wanakuwa na ushirikiano, tukumbuke Twiga Stars ikifanikiwa kusonga mbele itakuwa imeitangaza nchi, wala si kitu kingine na nchi ikitangazwa ni jambo zuri kwetu sote.
Tunasema dakika 90 za mchezo wa kwanza zimemalizika kwa Twiga Stars kulala mabao 2-1, bado dakika 90 nyingine ugenini, ambazo bado Twiga Stars ina nafasi kubwa sana ya kufanya vizuri. Kama wao Zimbabwe wameshinda mabao 2-1 Dar es Salaam, kwa nini Twiga Stars nayo isiende kuwafunga kwao?
Tunaamini kiasi cha fedha walichopewa Twiga Stars wiki hii ni motisha mzuri kwao kuhakikisha wanafanya vizuri mechi ya marudiano na kusonga mbele. Twiga Stars wapambane wasiwaangushe waliowasaidia maana watambue bado soka kwa wanawake haijapata msukumo mkubwa wa wadhamini, hivyo hawa wachache waliowapata wahakikishe hawawakatishi tamaa.
Tunasema inawezekana, vijana wetu wasikate tamaa wafanye maandalizi ya kutosha, wajipange kwani watacheza wakiwa wanafahamu vyema nguvu ya adui ipoje.
No comments:
Post a Comment