Mwenyekiti wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Kanga Meternity Trust (KMT) Dkt. Mohd Hafidh akitoa maelezo ya taasisi hiyo inavyofanya kazi zake kuhakikisha Mama wajawazito wanapata huduma bora wanapokwenda kujifungua hospitali Kuu ya Mnazimmoja katika hafla ya kuwasilishwa Utafiti wa Mradi wa PartoMa iliyofanyika Hoteli ya Tembo, Forodhani Mjini Zanzibar.
Madaktari bingwa wa Hospitali ya Mnazimmoja Dkt. Naufal Kassim (kushoto), Dkt. Zaki (kati) na Mwenyekiti wa KMT Dkt. Mohd Hafidh wakijadiliana jambo wakati wa hafla ya kuwasilishwa utafiti uliofanywa na Dkt. Anna Maaloe (hayupo pichani) kuhusu wadi za wazazi za Hospitali ya Mnazimmoja.
Mtafiti kutoka Mradi wa PartoMa Dkt. Anna Maaloe akiwasilisha utafiti wake juu ya huduma za wodi za wazazi za Hospitali kuu ya Mnazimmoja katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Tembo Forodhani Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Baraza la wauguzi na wakunga Dkt. Amina Abdulkadir akitoa mchango wake wakati wa kuwasilishwa utafiti wa huduma za wodi za wazazi za Hospitali kuu ya Mnazimmoja. Picha na Makam Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Dkt. Ali Salum kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali kuu ya Mnazimmoja akimkabidhi cheti na zawadi Metroni Mkuu wa Hospitali hiyo kwa kushiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na Mradi wa PartoMa katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Tembo.
Wauguzi wa wodi ya wazazi katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja wakimpa zawadi ya mlango na kasha Dkt. Anna Maaloe kwa kazi nzuri aliyosimamia ya utafiti wa wodi za wazazi katika Hospitali ya Mnazimmoja. Picha na Makam Mshenga-Maelezo Zanzibar
Mradi wa PartoMa unaoshirikisha Chuo Kikuu cha Copenhagen nchini Denmark na Hospitali Kuu ya Mnazimmoja wenye lengo la kuongeza ufanisi na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa wodi za wazazi katika hospitali ya Mnazimmoja umeanza kuleta mafanikio makubwa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mradi wa PartoMa kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali Kanga Martenity Trust (KMT) iliyopo Hospitali ya Mnazimmoja umeonyesha vifo vinavyotokana na uzazi na vifo vya watoto wanaozaliwa vimepungua tokea kuanza kwa mradi huo mwaka mmoja uliopita.
Akiwasilisha utafiti uliofanywa na mradi wa PartoMa ambao uliwashirikisha madaktari, wakunga na wasaidizi wakunga katika wodi za wazazi, Dkt. Anna Maaloe amesema bado ni mapema kuthibitisha kuwa mafanikio hayo yanatokana moja kwa moja na kuwepo mradi huo lakini ufanisi na utaalamu wa wafanyakazi kwenye wodi za wazazi Hospitali ya Mnazimmoja umeongezeka.
Amesema Hospitali za rufaa, kama ya Mnazimmoja zinawajibu mkubwa wa kuwa na mafunzo ya mara kwa mara kwa wafanyakazi waliopo na wanaotegemewa siku za mbele na kuweka miongozo bora ili kuokoa maisha ya mzazi na mtoto pamoja na wagonjwa wa kawaida.
“Kwa kuliona hilo mradi wa PartoMa umekuwa ukiandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo madaktari na watendaji wa wodi za wazazi Hospitali Mnazimmoja siku moja kwa miezi mitatu baada ya saa za kazi na kuweka miongozo ambapo wafanyakazi wengi wamekuwa wakishiriki,” aliongeza Dkt. Anna.
Katika utafiti huo Dkt. Anna amesema imebainika kuwa wafanyakazi wengi wa Hospitali ya Mnazimmoja wamehamasika kuongeza elimu na ufanisi na hiyo inasaidia katika kuokoa maisha ya wananchi.
Hata hivyo amesema bado kunachangamoto katika kutoa huduma bora zaidi katika Hospitali ya Mnazimmoja ikiwemo uhaba wa wafanyakazi katika wodi za wazazi ukilinganisha na ongezeko kubwa la wazazi wanaotumia Hospitali hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Hoteli ya Tembo Forodhani, Mwenyekiti wa KMT Dkt. Mohammed Hafidh amesema utafiti huo ambao ni wa kwanza kufanywa na kuwashirikisha watafiti wa wazalendo Hospitali ya Mnazimmoja utasaidia kuwa na taarifa sahihi na za uhakika kwa maendeleo ya Hospitali hiyo.
Amesema lengo la utafiti huo ni kuwasaidia mama wajawazito kujifungua salama na kwa heshma na kuzuia vifo vya mama na mtoto ambavyo vinaweza kuzuilika.
Nae Dkt. Naufal Kassim amekiri kuwepo mtafartoMa na ameshauri madaktari kujipanga kufanya tafiti zaidi za afya na kuyatumia matokeo ya tafiti zilizopo kwa ukamilifu.
Katika hafla hiyo Dkt. Ali Salum kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja aliwakabidhi vyeti madaktari, wakunga na wasaidizi wakunga walioshiriki mafunzo ya kuwajngea uwezo baada ya saa za kazi bila malipo katika hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment