mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Sunday, March 13, 2016

Esther Bulaya akamatwa, asafirishwa hadi Dar


Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya.

MBUNGE wa Bunda, Esther Bulaya (Chadema), amekamatwa usiku wa kuamkia jana mkoani Mwanza na kusafirishwa kwenda mkoani Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza Kuu la Chadema jijini hapa jana, Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe, alidai Esther alichukuliwa na Polisi ili asafirishwe kwenda Dar es Salaam kutokana na agizo la Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kwa mujibu wa madai ya Mbowe, kuitwa kwa Esther mjini Dar es Salaam na Spika Ndugai kunatokana na baadhi ya wabunge wa Chadema kuonesha msimamo wao baada ya kutolewa hoja ya kupunguzwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Shirika la Utangazaji (TBC) ndani ya Bunge lililopita.
Mbowe alidai kuwa hoja hiyo ya matangazo ya TBC ilipopelekwa bungeni, wabunge wote wa Chadema walikomaa na kutokukubaliana na msimamo wa Serikali. Baada ya hapo kwa mujibu wa madai hayo, baadhi ya wabunge wa Chadema waliitwa ndani ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, akiwemo Esther lakini hakwenda.
Mbowe amedai kuwa Esther hakutii mwito huo kwa kuwa wakati anaitwa katika Kamati hiyo iliyokuwa Dar es Salaam, alikuwa na kesi Musoma Mjini ambako ndiko alikokwenda kwa kuwa ilikuwa siku ya hukumu. Aliwataka viongozi wa chama hicho wasiogope vitisho vya Jeshi la Polisi pale wanapokuwa wanapigania haki za Watanzania.
“Kama wewe ni kiongozi wa chama hiki halafu unaogopa Polisi, aisee umepotea njia, Esther kwenda Polisi ni jukwaa lingine la Chadema la kuzungumza,” alisema. Katika hatua nyingine, Mbowe alisema Chadema itawashughulikia wanachama na viongozi wa chama hicho watakaokwenda kinyume na maadili ya chama hicho na kuongeza kuwa chama hicho hakitakuwa tayari kuvumilia viongozi wa aina hiyo.
Alisema kwa sasa Chadema inahitaji kujenga chama imara na utaratibu wa kukijenga chama hicho si lelemama na kwamba viongozi watakaporuhusu chama hicho kufa, maana yake ni kuirudisha nchi kwenye mfumo wa chama kimoja na hali hiyo ikitokea, Chadema itachukua miaka 25 kujenga chama imara.

No comments:

Post a Comment