mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Friday, March 11, 2016

VIETNAM NA TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO


vie6

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,  Balozi Augustine Mahiga amesema Tanzania na Vietnam zimeahidi kuendeleza  ushirikiano  katika nyanja mbalimbali kufutia makubaliano 
yaliyofanyika wakati wa ziara ya Rais wa Vietnam nchini.
Waziri Mahiga ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na waandishi wa habari wakati wa majumuisho ya ziara ya siku nne ya Rais wa Vietnam nchini Mheshimiwa Truong Tan Sang.
Akiwa ameongozana  na Waziri Habari na Mawasiliano wa Vietnman Nguyen Bal Son  ameyataja maeneo ambayo Tanzania na Vietnam zimekubaliana kushirikiana  kuwa ni uwekezaji wa  kilimo cha mpunga, uvuvi wa samaki wa ziwani na baharini na uanzishwaji wa viwanda vya kusindika mazao ya biashara.
“Tumekubaliana kushirikiana katika maeneo kadhaa ikiwemo kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kuongezeka kwa uwekezaji kutoka Vietnam kwani kwa sasa biashara inayofanyika kati ya Vietnam na Tanzania ni dola milioni 300 kwa mwaka, tumekubaliana ifikie dola bilioni 900  ifikapo mwaka 2020”
Aidha, maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na kufungua mahusiano ya mawasiliano na elimu, ambapo kutakua na fursa kwa wanafunzi wa Kitanzania kwenda kusoma nchini Vietnam, na wataalamu wa Vietnam kuja kufanya kazi pamoja na watanzania na kusema kuwa kampuni ya simu ya Halotel imefungua mlango kwa Vietnam kuwekeza nchini na kuongeza kuwa lengo la ushirikiano huu ni kuwa na uhusiano ulio sawa na kila mmoja anufaike na mahusiano hayo.
Hata hivyo, Mahiga amesema kuwa pamoja na maeneo  kadhaa waliyokubaliana jambo la msingi ni namna ambavyo nchi hizo zitatekeleza makubaliano hayo kwa kuwa na mawasiliano ya karibu  na kukutana  mara kwa mara baina ya watendaji wa Serikali hizo mbili.
Rais wa Vietnam Mhe. Truong Tang Sang, aliwasili nchini machi 8 mwaka huu, ambapo alikutana na Rais Mhe. John Magufuli na kufanya mazungumzo Ikulu na kutia saini mkataba wa kibiashara baina ya Tanzania na Vietnam.
Aidha, Rais Truong na ujumbe katika ziara yake ya siku nne nchini alikutana na Mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete, alizungumza na jukwaa la wafanyabiashara na viongozi wao, na  pia  alitembelea eneo la viwanda (EPZA) Ubungo jijini Dar es salaam.
Vilevile, alifanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein ambapo walikubaliana kuwa na mahusiano ya karibu na visiwa vya Zanzibar kwa ajili ya uwekezaji katika utalii na uvuvi wa samaki.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Vietnam Mhe. Nguyen Bal Son amesema nchi yake ina historia nzuri ya ushirikiano na mahusiano ya kidiplomasia ya muda mrefu yaliyo asisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hivyo wataendeleza uhusiano huo na Tanzania pamoja na kushirikiana ili kukuza uchumi wa nchi hizo.

No comments:

Post a Comment