mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Thursday, March 10, 2016

Magufuli aitamani Vietnam


Rais John Magufuli akimkaribisha Rais wa Vietnam, Truong Tang Sang alipowasili kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam jana kwa mazungumzo akiwa kwenye ziara ya siku nne nchini. (Na Mpigapicha Wetu).
RAIS John Magufuli amesema anatamani mafanikio ya nchi ya Vietnam kiuchumi na kubainisha kuwa ziara ya Rais wa nchi hiyo, Truong Tang Sang nchini, ni fursa na changamoto kwa watanzania kujifunza mambo mengi, yatakayosaidia kukuza pia uchumi wa Tanzania.
Aidha amehamasisha Watanzania kuchangamkia fursa na rasilimali zilizopo nchini katika kujiinua na kuimarisha nchi yao kiuchumi. Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi tajiri kwa rasilimali na fursa nyingi, ingawa bado iko nyuma kimaendeleo. Kwa upande wake, Rais Sang amesema nchi yake na Tanzania zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya biashara, kilimo, viwanda na uvuvi lengo likiwa ni kuhakikisha nchi zote zinanufaika kwenye ushirikiano huo.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari na marais hao Ikulu Dar es Salaam jana, Dk John Magufuli alisema ni wakati sasa wa Tanzania kujifunza kutoka kwa nchi hiyo ya Vietnam ambayo pamoja na kukabiliwa na vita ya muda mrefu, imefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati. “Ukweli ni kwamba ziara ya Rais Sang nchini kwetu ni muhimu sana na imekuja kwa wakati muafaka.
Mwaka 1976 Rais wa Vietnam alikuja nchini na alichukua mbegu ya korosho na kuipeleka nchini kwake, na leo hii Vietnam ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kuzalisha korosho duniani,” alisema. Alitaja mafanikio mengine ya nchi hiyo ni pamoja na kuwa na uchumi wa kati, licha ya kukabiliwa na mapigano ya muda mrefu. Ilipata uhuru wake mwaka 1945 na ilidumu kwenye mapigano hadi Julai 2, mwaka 1976.
Alisema mwaka 1977 mapato ya kila raia wake yalikuwa ni dola 100, lakini sasa imefanikiwa kupandisha mapato hayo na sasa kila raia wa nchi hiyo mapato yake ni dola 2000 kwa mwaka na imepunguza kiwango cha umasikini kwa asilimia 50. “Sisi tangu mwaka 1960 bado tuko kwenye nchi masikini, kwa hiyo hii ni changamoto kwa nchi yetu. Tunatakiwa kujifunza kuondokana na hali hii.
Wao uzalishaji kwa mchele wanalima mara tatu kwa mwaka, sisi tunalima mara moja tu na inawezekana uzalishaji wetu ni mdogo sana,” alisema. Alisema nchi hiyo pamoja na kuchukua mbegu ya korosho nchini, ndio nchi inayoongoza kwa kuzalisha korosho duniani, wakati Tanzania ndio iliyotoa mbegu hiyo, zao hilo badala ya kuzalishwa kwa wingi ndio uzalishaji wake unafifia.
“Samaki sina uhakika kama walichukua huku, lakini leo hii Vietnam ni wazalishaji wa samaki wakubwa sana. Lakini kwa nchi yetu ambayo ina maziwa 21 na mito kila mahali na bahari lakini uzalishaji wa samaki uko chini…” “Tuna ng’ombe zaidi ya bilioni 22 hadi bilioni 23 nafikiri tunaweza kuwa wa pili barani Afrika baada ya Ethiopia, lakini ngozi zetu za viatu hapa tunaagiza nje.
Kwa hiyo kwa hili watanzania tunatakiwa tusiogope kujifunza kwa wale waliotutangulia ili na sisi nchi yetu iweze kufika mahali pazuri,” alisisitiza Dk Magufuli. Alisema ujio wa Rais Sang pamoja na ujumbe wake wa zaidi ya mawaziri takribani 20 na wafanyabiashara ni wakati pekee wa Watanzania na wa Vietnam, kuimarisha ushirikiano uliokuwepo kwa zaidi ya miaka 50 sasa kuhakikisha uhusiano unaleta maendeleo kwa pande zote.
“Ziara hii ni muafaka kwetu sisi watanzania kujenga uhusiano mzuri na nchi ya Vietnam ili kuweza kujifunza na sisi tuweze kufikia lengo letu la kuwa nchi ya kipato cha kati,” alisema. Pamoja na hayo, Rais Magufuli alisema katika mazungumzo yake na Rais wa Vietnam alipata mwaliko wa kutembelea nchi hiyo mwakani. “Kwa kweli mwaliko huu nimeupokea na ninajisikia kuthaminiwa na kuheshimiwa sana,” alisema.
Kwa upande wake, Rais Sang alisema anajisikia fahari kuona uhusiano kati ya Tanzania na nchi yake unaimarika. Alisisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaleta maendeleo ya dhati baina ya nchi hizo mbili. Alipongeza serikali kupambana dhidi ya umasikini kwa kusisitiza kuwa inafanya vizuri kiuchumi kwani ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.
“Kama rafiki wa karibu tunavutiwa na maendeleo yenu hasa katika kupambana na umasikini lakini pia ukuaji wa kasi wa uchumi wenu. Katika mazungumzo yetu na Rais Magufuli tumezungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kilimo, biashara na viwanda,” alisema rais huyo. Aidha, alisema uhusiano wa nchi hizo mbili ni wa muda mrefu, kwani pamoja na umbali wa kijiografia Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vietnam.
Alisema ziara hiyo ni moja ya njia za kudumisha na kuboresha zaidi uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili. Rais huyo alisema kwenye mazungumzo yake na Magufuli, wamekubaliana kushirikiana katika maeneo yatakayonufaisha nchi zote. Maeneo hayo ni kilimo, biashara, viwanda na mawasiliano. Pia walisaini mikataba ya kutowatoza kodi mara mbili wawekezaji na wafanyabiashara wanaowekeza katika nchi hizo.
Aidha Rais huyo alisema katika kikao chake na Rais Magufuli pamoja na mawaziri wa nchi zote mbili wamekubaliana kuanzisha tume ya pamoja itakayosimamia masuala ya uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili. Aidha marais hao walizungumzia masuala ya kimataifa ambapo wote kwa pamoja walikubaliana suala la kuhakikisha amani na utulivu linapewa kipaumbele na mataifa yote duniani.
“Tulikubaliana kuwa nchi zote zina wajibu wa kuhakikisha suala la amani linapewa kipaumbele, ikiwemo na mataifa ya kimataifa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha na kutuliza vurugu zinazoibuka katika nchi mbalimbali,” alisema. Alisisitiza kuwa amemwalika Rais Magufuli kutembelea Vietnam wakati wowote. Tayari Marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, walishafanya ziara katika nchi hiyo wakati wa utawala wao.
Rais Sang aliyeongozana na ujumbe wa watu 51 ataendelea kuwepo nchini kwa ajili ya kumalizia ziara yake katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kutembelea Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).

No comments:

Post a Comment