MKUU wa Wilaya ya Ukerewe, Mwanza, Joseph Mkilikiti ameagiza kila siku apelekewe taarifa ya vifo vya wagonjwa vinavyotokea vituo vya afya. Akizungumza katika kikao cha kamati ya afya ya msingi ya wilaya hiyo juzi, Mkilikiti alisema pia taarifa hiyo iwe na sababu za vifo ili kumwezesha kusimamia ipasavyo utoaji huduma kwa wagonjwa.
Alisema mara kwa mara anapokea taarifa toka zahanati, vituo vya afya na hata hospitali ya wilaya zinazohusisha baadhi ya vifo hasa vya akinamama na watoto kusababishwa na uzembe wa watumishi.
Sambamba na hilo, pia ameagiza kupewa taarifa ya uagizaji dawa pamoja na taarifa ya dawa na vifaa tiba zilizopo hasa katika hospitali ya wilaya, ili kumwezesha kufuatilia na kuondoa tatizo la upungufu wa dawa.
Maelekezo hayo yanatokana na taarifa iliyotolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Taitus Kaniki kuwa hali ya dawa na vifaa tiba ikiwemo dawa za kutibu wagonjwa wa kipindupindu zimeisha.
Alisema tatizo hilo limetokea baada ya Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Ziwa kushindwa kuleta dawa tangu ziagizwe miezi miwili na kusababisha kero kubwa wakati wa utoaji huduma.
Wakati huohuo, Mkilikiti amepiga marufuku uuzaji na unywaji wa pombe na michezo ya pool wakati wa saa za kazi ili kuwezesha kila mmoja kwa nafasi yake kufanya kazi za kuingiza kipato.
Aidha amezuia michezo ya bahati nasibu pamoja na wanafunzi kwenda kwenye kumbi za maonesho ya video na kuwataka watumie muda huo kujisomea ikiwa ni mkakati wa kuinua taaluma.
No comments:
Post a Comment