JAJI Mkuu, Mohamed Chande Othman amesema, Mahakama ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma itaanza kutoa huduma haraka iwezekanavyo mwaka huu ili kuwaondolea wananchi usumbufu kutafuta haki zao mbali.
Alisema hayo jana baada ya kuwasili katika mji mdogo wa Mbamba Bay wilayani hapa, akiwa katika ziara yake ya siku nne mkoani Ruvuma kukagua na kuangalia kazi za Mahakama. Wilaya ya Nyasa haina jengo la Mahakama ya wilaya tangu Serikali ilipoianzisha miaka saba iliyopita.
Hakimu Mkazi Mfawidhi aliyekuwepo hana ofisi, hali inayomlazimu wakati mwingine kusafiri zaidi ya kilometa 50 kuhudumia wananchi. Jaji Mkuu aliwataka wananchi na wadau wengine wa Mahakama wilayani humo kutoa ushirikiano kufanikisha malengo ya Mahakama kumaliza usikilizaji mashauri kwa wakati ili wanaotafuta haki kupitia chombo hicho waipate kwa wakati.
Alisema, "Kuchelewa kwa ujenzi wa mahakama ya wilaya kumetokana na ukosefu wa fedha". Hata hivyo, Serikali iliahidi kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya mahakama nchini zilizo katika hali mbaya.
Aliwataka Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Mkoa kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi ikiwemo kuharakisha usikilizaji wa mashauri yanayowasilishwa mbele yao . Alisema kwa kufanya hivyo, wataondoa dhana potofu inayowahusisha mahakimu na rushwa.
Alisema "Ni wajibu kwa kila hakimu kutenda haki kwa wananchi na kuzingatia weledi wakati wa kusikiliza mashauri na kutoa hukumu". Alisisitiza wajiepushe na vitendo ambavyo ni kinyume na viapo vyao vya utumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment