KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm, amewatetea wachezaji wake kwa kuonesha kiwango cha chini walipocheza na Mwadui FC juzi, na kusema hilo lilitokana na presha ya kuiengua Simba kileleni wakitumia michezo ya viporo.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Yanga ilishinda mabao 2-1, na kufikisha pointi 56, ikiwa ni moja pungufu dhidi ya vinara Simba wenye pointi 57.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo kumalizika, Pluijm alisema ulikuwa mgumu kwao na wapinzani wao Mwadui waliwabana hata kujikuta katika wakati mgumu, lakini amefurahishwa na ushindi walioupata kwani umezidi kurudisha matumaini yao ya kutetea taji lao la Ligi Kuu msimu huu.
“Angalau kipindi cha pili, lakini kipindi cha kwanza tulicheza vizuri kwa dakika 10, baada ya hapo tulicheza vibaya na kuwapa nafasi wapinzani wetu kucheza kwa kujiamini na kutushambulia hasa baada ya kupata bao la kusawazisha, lakini najua presha ya mechi za viporo ni kubwa na wachezaji wangu walicheza kwa hofu,” alisema Pluijm.
Alisema ameona upungufu uliojitokeza kwenye mchezo huo na wanajipanga katika siku mbili za mazoezi ili wasirudie kwenye mchezo wao wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kwa upande wake kocha wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo, ‘Julio’ amesema kipigo hicho wala hakimuumizi roho na kudai mwamuzi hakuwa akiwatendea haki.
Alidai kitendo cha beki wake Kulwa Mobby kutolewa nje kwa kadi nyekundu bila kosa la msingi kilikuwa ni cha kuidhoofisha timu yake na kwamba wapinzani wao walitumia mwanya huo kupata bao.
No comments:
Post a Comment