mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Sunday, April 10, 2016

Pingamizi la Bausi latupwa ZFA



KAMATI ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), imetupilia mbali pingamizi iliyowekwa na mgombea urais wa chama hicho, Salum Bausi aliyoikata dhidi ya mgombea mwenzake Ravia Idarous Faina.
Bausi alimuwekea pingamizi Raivia akitaka aondolewe kuwania nafasi hiyo kwa madai ya kujihusisha na siasa zaidi, kukiondolea chama uhusiano mzuri wa kimichezo na nchi nyingine na pia kukiweka chama hicho katika wakati mgumu wa kufutiwa uanachama na mashirikisho ya kimataifa.
Madai mengine ni pamoja na kuwepo shutuma za ubadhirifu wa fedha wa chama hicho na kuwepo kwa kesi ya jinai dhidi yake, sababu alizodai zinamuondolea sifa kuongoza ZFA.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Uchaguzi huo, Kibabu Haji Hassan, alisema kamati baada ya kupitia kwa kina pingamizi hilo, imebaini hakuna sababu ya kumuondoa Ravia asiwe mgombea kutokana na vipengele, ambavyo vimetumika havimo katika kanuni wala masharti ya kugombea.
“Tumepitia pingamizi na kuona sababu ambazo zimetolewa hazimo katika kanuni zetu za kuendesha uchaguzi wala masharti ya kugombea,” alisema.
Hata hivyo, katika hatua nyingine alisema kampeni zilifunguliwa rasmi jana na zinatarajia kumalizika Aprili 13 mwaka huu.
Aliwataka wagombea wote kupiga kampeni za kistaarabu bila ya kuchafuana wala kutoleana matusi. Uchaguzi wa ZFA Taifa unatarajiwa kufanyika April 14 mwaka huu mjini Unguja, ambapo nafasi zinazogombewa ni Rais na Makamu wa Rais Pemba na Unguja.
Waliojitokeza kuwania urais ni Ravia anayetetea nafasi hiyo na Bausi Wakati Makamu wa Rais Unguja ni Mohammed Masoud, Ali Salum Nassor Mkweche na Mzee Zam Ali, huku Makamu wa Rais Pemba ni Ali Mohammed anayechuana na Suwedi Hamad.

No comments:

Post a Comment