mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Monday, April 18, 2016

Wasanii wa kike watakiwa kuhamasisha kupima afya


WASANII wa kike nchini wameaswa kutunga wimbo maalumu wa kuhamasisha vijana wa kike kujitokeza nchini kupima virusi vya Ukimwi kama sehemu ya kutekeleza wajibu wao kwa vitendo katika kuunga mkono kampeni ya kitaifa kwa wasichana wenye umri wa miaka 15-24 kwa kuwahamasisha wajitokeze kupima afya zao.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipozungumza kwenye hafla ya kuzindua kampeni ya kitaifa ya kupima virusi vya Ukimwi kwa wasichana iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya msingi Kakola wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Alisema wasanii wana nafasi kubwa kupitia shughuli zao za sanaa kuhamasisha na kuelimisha jamii kwa mambo ya msingi ya maendeleo ya nchi, likiwemo kuwahamasisha wasichana wajitokeze kupima afya zao.
Alimtaka Msanii wa kizazi kipya Supa Nyota Diva 2014, Hellen George ‘Ruby’ ambaye alitumbuiza katika hafla kuwatafuta wasanii wachanga wa kike nchini kutunga wimbo huo.
“Ruby hebu tukutane Dar es Salaam ili tuone ni namna gani tufanye ili wewe na wasanii wenzako wa kike mtunge wimbo maalum utakaotumika kwenye kampeni ya kuhamasisha wasichana kupima afya zao,”, alisema Ummy.
“Unajua Ruby akionekana nawasanii wenzake wa kike wakiwa wanaimba kwa kuwahamasisha wasichana na kwasababu watakuwa ni wasanii wa kike wenye umri mdogo wanaolingana na wao watawahamasisha sana wajitokeze kupima afya zao,”alisema.
Aidha aliwataka vijana wa kike na kiume nchini badala ya kutumia muda mwingi kwenye mtandao wa kijamii wa WhatsApp kwa kutuma ujumbe wa mapenzi, watumie ujumbe katika kuhamasishana kupima afya zao.
Kwenye hafla hiyo Ruby ambaye alipanda jukwaani mara kadhaa alikuwa kivutio kikubwa kwa watu waliohudhuria kwenye kampeni hiyo maalumu ya kitaifa ya kuhamasisha wasichana kupima virusivya Ukimwi.

No comments:

Post a Comment