BOMBA LA MAJI LATAJWA
Habari zilizolifikia gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita na kutiliwa nguvu na hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea gereza hilo, zilieleza kwamba, kuna ‘mchongo’ unaofanywa na vigogo kadhaa wa unga kwa lengo la kumtorosha Shkuba, wakitumia kivuli cha mradi wa kuingiza bomba la maji gerezani hapo ambapo pengine hata wenye mradi huo hawajui lolote.
“Kuna bomba linachimbwa kuingia gerezani, wenyewe wanasema ni mradi wa kulipatia gereza hilo maji lakini kuna tetesi kwamba huenda bomba hilo ndiyo njia ya kutaka kumtolea Shkuba gerezani lakini wenye mradi hawana habari.
NJAMA ZAFANANISHWA
“Si unajua hata El Chapo (kigogo maarufu wa unga nchini Mexico), alitoroshwa kupitia bomba la chooni? Hakuna aliyejua kumbe wenzake ambao ni Mafia walikuwa wakilipigia hesabu bomba lile la chooni kuja kushtuka, El Chapo ameshatoka,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa jina.
Baada ya kupata taarifa hiyo, Uwazi lilianza kufuatilia kwa kina ili kujua kuhusu mradi huo lakini wakati uchunguzi ukiendelea, Waziri Mkuu Majaliwa naye alichezwa na machale na kuuzungumzia mradi huo.
Akiwa ziarani mkoani Lindi hivi karibuni, Waziri Majaliwa alimtahadharisha Mkuu wa Gereza la Lindi, Tusikile Mwaisabila kuwa makini na zabuni wanazotoa gerezani hapo, ikiwemo ya uwekwaji wa mabomba ya maji kwani inaweza kutumika kuwatorosha vigogo wa unga, akasisitiza kwamba ulinzi uimarishwe ili kuhakikisha hakuna kigogo wa unga atakayetoroka.
MSIKIE WAZIRI MKUU
“…hata hili bomba la maji linalopeleka maji gerezani lisije likawa ni njia, simamieni sana hili,” alisema waziri Majaliwa akimaanisha kuimarisha ulinzi katika gereza hilo kwa hofu kwamba watuhumiwa wa unga wasije wakatumia nafasi hiyo kutoroka.
WAZIRI KITWANGA
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Uwazi lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ili kumuuliza kuhusu kudaiwa kwamba mradi huo unaweza kutumika kutaka kumtorosha Shkuba ambapo alipopatikana kwa njia ya simu asubuhi na kusomewa maelezo hayo mwanzo hadi mwisho, alimsukumia mzigo Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, John Minja kwamba ndiye anayetakiwa kujibu kuhusu mradi huo na hali ya ulinzi gerezani hapo kufuatia uwepo wa watuhumiwa wa madawa ya kulevya.
“Sasa hilo tafadhali sana muulize Kamishna wa Jeshi la Magereza Tanzania, atakwambia nini kinaendelea,” alisema Waziri Kitwanga.
MSEMAJI WA MEGEREZA
Jitihada za kumpata Kamishna Minja ziligonga mwamba kutokana na simu yake kutopatikana hewani kila alipopigiwa lakini badala yake, alipatikana Msemaji wa Jeshi la Magereza Tanzania, Deodatus Kazinja ambaye kimsingi ndiye mwenye kujua mambo ya magereza yote nchini.
Katika mahojiano na Uwazi, Kazinja alikiri kuwepo kwa mradi huo lakini akaeleza kwamba wanafuatilia kwa kina kujua ni nani aliyepewa zabuni ya kuingiza mabomba ya maji gerezani hapo na lini na kuangalia kama kuna uhusiano wowote kati ya mzabuni huyo na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya walioko gerezani humo.
“Nitafuatilia, nipe muda nijue mradi ulianza lini na nani mwenye zabuni hiyo na uhusiano wake na madai hayo,” alisema Kazinja.
KAMISHNA MINJA KUWASILI
Habari za uhakika kutoka gerezani hapo zinaeleza kwamba siku yoyote kuanzia Jumapili iliyopita, Kamishna Minja angewasili kwenye gereza hilo ambapo pamoja na mambo mengine atafuatilia hali ya usalama wa gereza hilo pamoja na watuhumiwa wa unga waliopo mahabusu.
KIKAO KIZITO CHA GEREZA
Pia, taarifa zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zinasema kuwa, jana Jumatatu, baadhi ya vigogo wa gereza hilo walitarajia kukaa kikao kizito cha dharura kuangalia mustakabali mzima wa ulinzi gerezani hapo pamoja na madai kwamba, mradi huo wa kuingiza maji unaweza kutumika kutaka kumtorosha Shkuba na wenzake.
KAULI ILIYOWAHI KUTOKA
Wiki chache zilizopita, Kamishna Minja alipokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya jijini Dar alikaririwa akisema:
“Jeshi la Magereza limekuwa na changamoto ya uhaba wa fedha za kufanya ukarabati na upanuzi wa magereza za zamani ili yawe na miundombinu inayoendana na ongezeko la wafungwa na mahabusu.
“Mfano mzuri unapokuwa na mtu kama Shkuba ambaye ni hatari hata kwa nchi kama Marekani, imetulazimu kuongeza ulinzi katika Gereza la Lindi ambalo yupo mahabusu mpaka sasa.”
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umedhihirisha kwamba, tangu kauli hiyo ya waziri mkuu, ulinzi kwenye gereza hilo umeimarishwa maradufu ambapo askari wengi wameonekana wakirandaranda gerezani hapo kwa saa ishirini na nne kuhakikisha hakuna ‘figisufigisu’ yoyote inayoweza kutokea na kusababisha Shkuba na wenzake kutoroshwa.
Shkuba alinaswa saa sita usiku wa Februari 23, 2014 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar akijiandaa kwenda nchini Afrika Kusini na kuhusishwa na unga aina ya heroin kiasi cha kilo 211 yenye thamani ya shilingi bilioni 9.4 uliokamatwa Januari, mwaka huo mkoani Lindi.
Baada ya kukamatwa, alisafirishwa usiku huohuo kwenda Lindi chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo Februari 27, mwaka huo aliunganishwa na watuhumiwa wengine na kufikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kusini.
Watuhumiwa hao wengine ni pamoja na binti wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, Maureen Liyumba.
ULINZI KEKO, SEGEREA
Mbali na Gereza la Lindi, ulinzi umeimarishwa pia katika Magereza ya Keko na Segerea jijini Dar es Salaam ambako vigogo wengine wa unga wanashikiliwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vyetu makini kutoka katika Gereza la Keko zinaeleza kuwa, ulinzi ulianza kuimarishwa tangu mwaka jana baada ya magaidi kutishia kuvamia maeneo yote ya magereza yanayohifadhi wenzao wakiwemo wale waliohusika kupiga Kituo cha Polisi Stakishari, Dar.
Mkuu wa Gereza la Keko, Kibwana Sinashida alipohojiwa kuhusu hali ya usalama gerezani hapo, alisema imeimarishwa na hawana hofu katika hilo.
Kwa upande wa Gereza la Segerea, chanzo kilisema kuwa umeimarishwa kwani hata zana na vitendea kazi vya kisasa vipo vya kutosha.
No comments:
Post a Comment