WENGI wanachukulia sare ya Yanga ya bao 1-1 dhidi ya mabingwa mara nane wa Afrika, Al Ahly kwenye uwanja wa nyumbani sio matokeo mazuri sana kwa Yanga itakapokutana na timu hiyo kwenye Jiji la Alexandria, Misri leo, lakini kocha Abdallah Kibadeni anaamini Yanga inaweza kufanya vizuri.
Kwa matokeo hayo ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zaidi ya wiki moja iliyopita ni kama Yanga imefungwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwani wapinzani wao wana faida ya bao la ugenini.
Hata hivyo, katika soka sio sahihi sana kutokana na ukweli ulio wazi kwamba kama Al Ahly walifanikiwa kufunga bao Dar es Salaam na Yanga wana uwezo wa kufunga bao leo Alexandria, wakiwa na nidhamu ya mchezo basi wanaweza kuandika historia mpya kwenye mashindano hayo.
Hivyo, wawakilishi hao wa Tanzania watatakiwa kupata bao la mapema na huku wakicheza kwa tahadhari kubwa kutoruhusu wavu wao kuguswa kwa muda wote wa mchezo huo, kwani wakifanya hivyo ni kama watakuwa wametolewa tu kwenye mashindano hayo.
Kibadeni, mmoja wa makocha wakongwe soka nchini, ameyasema hayo kutokana na kumbukumbu nzuri ya namna alivyoiongoza Simba kuwafunga Al Ahly kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mwaka 1985 kwa mabao 2-1 ya Zamoyoni Mogella na kiungo Mtemi Ramadhani na lile la kufutia machozi la wageni likiwekwa kimiani na Mohammed El Khatibu ’Bibo’.
Kibadeni alikuwa na maneno ya busara kwa Yanga, ambao wana upinzani mkubwa na Simba ambayo kocha huyo amewahi kuifundisha mara nyingi na kupata mafanikio nayo makubwa.
Kibadeni anashauri wachezaji wa Yanga wajitume kwenye mchezo wa leo ili kusonga mbele. “Sare ya bao 1-1 ni kama Yanga wamefungwa tu, ingawa mechi bado iko wazi sana kwa timu zote mbili, hasa kwa Yanga wenyewe.
Muhimu wachezaji wakajua kuwa wana deni na hivyo wajitume kwenye dakika ya kwanza mpaka ya mwisho. “Wacheze soka la kushambulia ili kupata bao la mapema, wasijihami hata kidogo, lakini muhimu wajilinde vizuri pia ili wakati wanafanya mashambulizi kutoruhusu Al Ahly wasipate bao la mapema,” alisema Kibadeni.
Alisema kama Yanga watafanikiwa kuwadhibiti Al Ahly kuanzia dakika ya kwanza mpaka dakika ya 15 wasipate bao ni rahisi kwa Waarabu kuchanganyikiwa na Yanga kutumia nafasi hiyo kupata ushindi.
Maneno hayo ya Kibadeni yaliungwa mkono na nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay aliyesema Yanga haina budi kushambulia, lakini wakati huo kujilinda ili kutoruhusu Al Ahly kupata bao la mapema.
“Wanatakiwa kucheza soka la kushambulia kuanzia dakika ya mwanzo, lakini pia wacheze kwa tahadhari kubwa kutowapa nafasi ya kupata bao la mapema, lazima Al Ahly watacheza soka la kushambulia mwanzo mwisho, Yanga lazima wajue hilo,” alisema Mayay ambaye wakati wake Yanga ilikutana na Zamalek mwaka 2001.
Alisema uwepo wa kiungo Haruna Niyonzima, utaisaidia Yanga kwenye mchezo huo kwani ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kukaa na mpira na kutengeneza mazingira ya wenzake kucheza.
Kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, ambao Yanga walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0, kocha wa timu hiyo Hans Pluijm, alitumia mabeki watatu nyuma kwenye mfumo wa 3-5-2 lakini Mayay alishauri asitumie mfumo huo kwenye mechi ya leo.
“Alianza na mabeki watatu nyuma kwenye mfumo wa 3-5-2 na kumfanya beki Vincent Bossou kucheza kama kiungo mkabaji. “Lakini kwenye soka la kisasa kiungo mkabaji anapaswa kuanzisha mashambulizi kitu ambacho Bossou alishindwa kufanya.
Lakini baada ya kumtoa Yondani na kucheza na mabeki wawili wa kati walicheza vizuri na kushambulia,” alisema Mayay. Kwenye mchezo wa leo Yanga inaweza kuwa na nahodha wake Nadir Haroub ’Cannavaro’ na kiungo wake Haruna Niyonzima waliokosa mchezo uliopita, lakini habari njema ni kurejea kwa kipa wake Ally Mustapha ’Barthez’ aliyeumia dakika za mwisho za mchezo uliopita.
Yanga inahitaji kupata ushindi wa aina yoyote au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ya mashindano hayo.Katika michezo mingine inayofanyika leo, mabingwa wa Afrika, timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itashuka uwanjani mjini Lubumbashi kuivaa Wydad Casablanca ya Morocco ukiwa ni mchezo marudiano.
Mazembe anayochezea Mtanzania, Thomas Ulimwengu, inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 3-0 ili kusonga mbele baada ya kufungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza mwishoni mwa wiki mjini Casablanca.
No comments:
Post a Comment