MAPISHI YA MWAMBAO VYAKULA VIKUU

Mchele kilo 1
Kuku mkubwa 1
Vitunguu maji kilo 2
Mayai 8
Samli kilo 1
Thomu gram 200
Tangawizi mbichi gram 50
Mdalasini gram 50
Hiliki gram 50
Bizari nzima kiasi
Siki kiasi
Mtindi painti 1
Tungule kilo 1
Zabibu nyeusi kiasi
1 Mkate kuku umwoshe umchemshe kwa maji na chumvi mpaka awive, kisha muepue.
2 Menya vitunguu uvioshe uvikate na uvigawe sehemu mbili. Sehemu moja uiweke, sehemu ya pili vikaange mpaka viwe vyekundu kama vya biriani. Kisha vichuje uitoe samli yote, vitie katika sinia uvitandaze ili vipoe kwa kupata upepo.
3 Chukua mdalasini, hiliki na bizari utwange pamoja, kisha uchunge unga laini. Saga thomu na tangawizi mbichi. Saga tungule.
4 Teleka sufuria tia samli ile ile iliyokaangiwa vitunguu halafu utie vile vitunguu vilivyobakia uvikaange. Vikianza kuiva tia viungo ulivyovitwanga na kuvisaga. (Bakisha vitunguu na viungo kidogo). Tia vipande vya kuku, mtindi siki na supu ya kuku iliyobakia katika sufuria. Acha ichemke nyama pamoja na vitu vyote mpaka libaki rojorojo.
5 Teleka maji, yakichemka tia chele. Ukiiva utoe uchuje yatoke maji yote.
6 Teleka tena sufuria utie samli kidogo utie na vile vitunguu ulivyovibakisha uvikaange. Tia mdalasini nzima, kaanga pamoja, tia na ule wali ukoroge koroge ili uchanganyike na viungo. Kisha ufunike upalie moto.
7 Chemsha mayai yote uyamenye.
8 Wali ukishakauka utaupakua, lakini lazima itabidi utumie kombe au sahani kubwa itakayoweza kuingia wali pamoja na vitu vyote. Kuupakua kwake kwanza utatia nusu ya wali katika hiyo sahani, baadae utatia masalo na nyama yote, na mayai, kisha utayafunika masalo kwa wali uliobakia. Mwisho utachukua vile vitunguu ulivyovikaanga na ukavitandaza ili vipo, utavimwaga juu ya wali.Kwani ni kwa sababu ya hivi vitunguu ndio maana ukaitwa wali wa asumini. Ukipenda utapamba chembe za zabibu juu yake. ZABIBU HIZO Ziroweke kwanza ili zivimbe.
WALI WA BIRIANI
Mchele kilo 1
Nyama kilo 1
Samli ½ kilo
Mbatata ½ kilo
Vitunguu maji kilo 1
Thomu gram 150
Tangawizi mbichi gram 150
Hiliki gram 50
Mdalasini gram 100
Mtindi painti 1
Siki kiasi
Majani ya nanaa fungu moja
Chumvi kiasi
Zaafarani kidogo (irowekwe kwa maji ya moto nusu kikombe cha kahawa)
Tungule ilosagwa
Tungule ya kopo
1 Menya vitunguu maji uvioshe uvikate. teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange bila ya kuvivuruga mpaka viwe vyekundu. Vichuje uvitoe halafu vitandaze katika sinia.
2 Twanga mdalasini na hiliki mpaka viwe laini kama unga. Menya thomu uitwange pamoja na tangawizi mbichi.
3 Kata nyama vipande vikubwa kisha tia chumvi na vitu ulivyovisaga (yaani tangawizi mbichi na thomu) vile vile tia unga unga wa mdalasini na hiliki pamoja na mtindi wa maji. Pika mpaka karibu nyama kuiva kabisa ndipo utie mbatata. Ukiona mbatata zimeshaiva tia siki.Usiache kukauka kabisa, bakiza rojorojo. Tia maji katika sufuria na chumvi yakichemka tia mchele. Acha utokote, angalia kiini cha wali ukiona umeshaiva uchuje.
4 Angalia sufuria ya nyama na rojo lake lisiwe limekauka kabisa, lazima ziwe na maji kidogo. Chukua vile vitunguu ulivyovikaanga vikapoa uvinyunyuzie juu ya masalo yote (usikoroge). Halafu utie mchele uliouchuja, nyunyuzia maji ya zaafarani juu ya wali wote halafu unyunyuzie samli ile uliyochuja kutoka kwenye vitunguu ulivyovikaanga ienee juu ya wali wote. Kisha funika upalie makaa.
5 Wali ukishakuwa tayari utaupakua. lakini unapotaka kuupakua lazima kwanza uutoe wali wote mweupe uutie katika chombo chengine, halafu uyakoroge masalo yachanganyike sawasawa kisha ndio uyatie juu ya wali katika kila sahani.
No comments:
Post a Comment