MSHAMBULIAJI wa Yanga Donald Ngoma amewaomba mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho wakati Yanga itakapokuwa inapata ushindi dhidi ya Al Ahly mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na gazeti hili, mshambuliaji huyo aliyetua Yanga msimu huu akitokea timu ya Platinum ya Zimbabwe, alisema lengo lake ni kuona Yanga inapata ushindi mnono kesho.
Alisema anafurahi mashabiki wa Yanga wamempokea vizuri na namna ya kuwalipa ni kuwafanyia kazi itakayowapa furaha na mojawapo ni kuifunga Al Ahly kaba hawajakwenda kurudiana nchini Misri.
Pia amesema ndoto yake nyingine ni kuipa Yanga taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo ambalo anaamini linawezekana. Ngoma ambaye ameshaifungia Yanga mabao 15 mpaka sasa, alisema hata mabao yake anayofunga sasa hayatakuwa na maana kama Yanga haitashinda taji la Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara msimu huu.
“Hata haya mashindano ya kimataifa tunayoshiriki sasa ni kwa sababu wenzetu walishinda ubingwa msimu uliopita, na mimi lengo langu ni kushinda taji kwenye msimu wangu wa kwanza ili tuendelee kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao,”alisema Ngoma.
Alisema inawezekana kuitoa Ahly na kuingia hatua ya makundi, lakini lazima mashabiki wawaunge mkono kwa kujitokeza kwa wingi kuwashangilia. Wakati huohuo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro amesema wanataka kuifunga Al Ahly na waitoe mashindanoni na hiyo itakawa fursa yao ya kuibuka mabingwa.
“Lazima tuchukue ubingwa wa Afrika na uwezo tunao kwa sababu tuna wachezaji wazuri ambao ni tofauti na wale ambao tulikuwa nao msimu uliopita, tuna Donald Ngoma, Amis Tambwe, Mbuyu Twite, Isoufour Boubacar, Vicent Bosou na wengine ambao wameonesha ubora msimu huu,” alisema.
Muro alisema na ili kudhihirisha kauli hiyo wamejipanga kushinda mchezo wa nyumbani dhidi ya Al Ahly utakaochezwa kesho na pia wa marudiano utakaochezwa baadaye nchini Misri.
No comments:
Post a Comment