mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Thursday, April 14, 2016

Lugumi atoroka nchini......Adaiwa kupanda ndege usiku wa manane, haijulikani alikokwenda



Mfanyabiashara  anayemiliki Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd, Said Lugumi, ametoroka nchi.

Lugumi ambaye anatajwa kuwa na ukwasi wa kupindukia katika kipindi kifupi, aliingia mkataba tata na Jeshi la Polisi mwaka 2011, kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Taarifa za kutoroka nchi kwa mfanyabiashara huyo, zilielezwa na baadhi ya maofisa wa vyombo vya dola, ambapo inadaiwa kuwa aliondoka nchini Jumatatu wiki hii, siku ambayo Jeshi la Polisi lilitakiwa kuwasilisha mkataba huo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa mujibu wa sheria.

Mfanyabiashara huyo ambaye amekuwa akitembea na msafara mkubwa wa magari ya kifahari, huku akilindwa na walinzi maalumu wa kukodi, ametoroka wakati vyombo vya dola vilikuwa vikimuwinda.

Utata wa Malipo
Pamoja na hali hiyo inaelezwa kuwa licha ya Lugumi kuingia mkataba na Jeshi la Polisi wa Sh bilioni 37, lakini bado alilipwa Sh bilioni 46 nje ya mkataba.

Katika mkataba huo, alilipwa kiasi Sh bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha za makubaliano ya mkataba, lakini hadi sasa mashine hizo zimefungwa katika vituo 14 pekee jijini Dar es Salaam ambavyo hata hivyo haijaainishwa maeneo vilipo.

Sakata hili lilibainika wiki iliyopita baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kukutana na maofisa wa jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Msafara wake Wapungua
Duru za ndani zinaeleza kuwa tangu Kamati ya Bunge ilipoibua sakata hilo na vyombo vya dola kuanza kuwahoji baadhi ya washirika wake katika biashara, msafara wa mfanyabishara huyo umepungua.

Chanzo kimoja kinasema kwa mara ya mwisho mfanyabiashara huyo alionekana eneo la Oysterbay jirani na Kanisa la St. Peter, huku akiwa na magari mawili badala ya saba hadi 10 kama ilivyokuwa awali.

Mtoa habari huyo alisema Lugumi aliopoonekana mwishoni mwa juma lililopita, alikuwa na magari mawili likiwamo Toyota GX V8 toleo la mwaka huu, ambalo lilikuwa limebeba walinzi wake, huku mwenyewe akiwa ndani ya gari la kifahari aina ya Escalade.

“Lugumi anaishi Mbweni na awali ilikuwa msafara wake ukipita magari husimamishwa ili kumpisha, na huwa na magari mengi kweli mithili ya kiongozi wa nchi, jamani kuna watu wamejua kuitafuna nchi hii, na sasa huenda unatimia usemi wa Rais Magufuli kuwa ni zamu yao kuishi kama mashetani na si kama malaika,” kilisema chanzo hicho.

Mkataba Wahamishwa
Sakata la mkataba huo wa Polisi na Lugumi limezidi kuchukua sura mpya baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kunyang’nywa hoja hiyo na badala yake kuhamishiwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Hatua hiyo inatokana na utata uliogubika mkataba huo ambao unawahusisha vigogo kadhaa wa Jeshi la Polisi pamoja na baadhi ya watendaji wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, huku ikidaiwa kuwa huenda ikawa njia ya ‘kulindwa’.

Kutokana na hali hiyo, hadi kufikia Jumatatu saa 10 jioni, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly, alisema kuwa kamati yao haijapokea taarifa yoyote kuhusu Kampuni ya Lugumi, ambapo kamati hiyo ililitaka Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba huo hadi kufikia leo.

Aeshi alisema wamemuomba Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, ili aweze kuwaandikia Polisi barua kwa ajili ya kuwasilisha mkataba huo.

“Tumelazimika kumwandikia barua Katibu wa Bunge ili awaandikie barua polisi walete mkabata huo ndani ya siku tatu kutoka leo (juzi) kama walivyotakiwa na kamati yetu,” alisema Hilaly.

Kauli ya Bunge
Alipotafutwa Mkuu wa Idara ya Habari, Elimu na Mawasiliano, Ofisi ya Bunge, Owen Mwandumbya, alisema kama kuna hoja iliyoibuliwa na Kamati ya PAC kisha ikapelekwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, itakuwa ni kwa ajili ya kupata ufafanuzi kuhusu matumizi ya fedha.

“Kama suala hilo lipo Mambo ya Nje, itakuwa si kwa hoja iliyoibuliwa na PAC na hakuna suala linaloshughulikiwa kama limeanzia PAC.

“Na kama litakuwa limekwenda huko ni kwa ajili ya kupata uelewa kuhusu matumizi ya fedha, na unajua hivi sasa hizi  kamati zipo katika maandalizi ya bajeti. Ila hoja kuhamishiwa kamati nyingine hutokana na maelekezo ya Spika wa Bunge. Kwa hoja hii ya PAC bado suala hilo lipo chini yao,” alisema Mwandumbya.

Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment