KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema kiwango bora kilichooneshwa na vijana wake ndiyo ilikuwa chachu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa kiporo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam juzi.
Ushindi huo uliirudisha Yanga kileleni baada ya kufikisha pointi 59.
Akizungumza na gazeti hili baada ya mchezo huo, Pluijm alisema kiwango ambacho kilioneshwa na vijana wake kilimshangaza na walistahili kupata ushindi licha ya kubadili mfumo mara mbili kutokana na wapinzani wao Mtibwa Sugar kuwabana vilivyo.
“Kiwango hiki sijakiona katika mechi tatu zilizopita, ikiwemo ile na Al Ahly ambayo tulipata sare ya 1-1, naamini hii ilitokana na kila mchezaji wangu kutambua umuhimu wa ushindi klabu inahitaji nini kipindi hiki ambacho msimu unaelekea mwishoni,”alisema Pluijm.
Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema kwa kiwango hicho kinamfanya aende Misri kuikabili Al Ahly kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa akiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri bila kujali ubora na rekodi waliyokuwa nayo wapinzani wao.
Kwa upande wake kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime alisema timu yake haikuwa na bahati katika mchezo huo baada ya kuonesha kiwango kizuri lakini wakapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Yanga.
Maxime alisema kuwa amekubali matokeo hayo ingawa anawapongeza vijana wake kwa kucheza kwa kiwango cha juu na kupoteza nafasi nyingi, kitu ambacho alidai kilisababishwa na kukosa bahati katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
“Tumekubali matokeo tumepoteza mchezo nawapongeza Yanga, kwa ushindi wao walicheza vizuri na walistahili ushindi na baada ya mchezo tunakwenda kupumzika kwa siku mbili tatu baada ya hapo tutaanza mazoezi kujiandaa na mechi zilizopo mbele yetu,” alisema Maxime.
Maxime alisema pamoja na kupoteza mechi mbili mfululizo, ana uhakika msimu huu wataweka rekodi kwa kumaliza ligi katika nafasi tatu za juu baada ya kupoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment