BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limeitaka Klabu ya Yanga na nyingine ambazo hazijafanya uchaguzi kuanza mchakato ndani ya wiki hii. Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Mohammed Kiganja alisema jana Dar es Salaam kuwa mwisho wa kumaliza suala zima la uchaguzi huo likamilike hadi Juni 30, mwaka huu, uongozi mpya uwe madarakani.
Alisema katika uchaguzi wa Yanga Katiba inayopaswa kutumiwa ni ile ya mwaka 2010, ili wale watakaochaguliwa kuingia madarakani waingize vipengele vya mabadiliko ndani ya Katiba ya Yanga kama ambavyo wameelekezwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF).
Kauli ya Kiganja imekuja baada ya BMT, TFF na Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na Msajili Msaidizi wa Klabu na Vyama vya Michezo Ilala kukutana juzi kujadiliana juu ya uchaguzi wa Yanga na klabu nyingine.
“Juni Mosi mwaka 2014 Yanga kwa maelekezo ya TFF walifanya mkutano mkuu ili wafanye marekebisho ya katiba yao, lakini baada ya mkutano ule yale marekebisho hayakuingizwa kwenye Katiba ya Yanga hadi leo,”alisema.
Alisema mkutano huo ndio uliomuingiza Mwenyekiti wa Yanga madarakani, lakini kwa makubaliano kuwa Oktoba 2014, klabu hiyo ingefanya uchaguzi jambo ambalo hawakufanya wala kuingiza vipengele walivyoagizwa na TFF.
Kiganja alisema kwa mujibu wa sheria, Yanga haina uongozi wa kikatiba wala kisheria ambao kwa hali iliyopo ungeweza kuteua Kamati ya Uchaguzi kama kifungu F ibara ya 45 cha Katiba ya klabu hiyo kinavyoelekeza.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya kuundwa kwa BMT namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake namba sita ya mwaka 1971 na kanuni za msajili namba 442 za mwaka 1999, wanaagiza Yanga kufanya uchaguzi huo.
Pia, alisema kadi za wanachama wa Yanga katika uchaguzi huo zitumike zile zilizowahi kutumika katika uchaguzi uliopita, zenye saini ya Mwenyekiti wa Yanga na Katibu na si zile kadi za CRDB au Benki ya Posta.
Katibu huyo amesema TFF ndio watakaopanga tarehe ya uchaguzi na kuwaagiza kusimamia mchakato huo mzima ndani ya wiki hii. Baraza hilo limeiagiza TFF pia kuhakikisha klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania bara ukiondoa Simba na Coastal Union zote zifanye uchaguzi. “Kwenye kanuni za TFF wanatakiwa kuweka sheria kali zinazotekelezeka ili kudhibiti ujanjaujanja wa baadhi ya klabu kukwepa kufanya uchaguzi,” alisema.
No comments:
Post a Comment