MBIO za kuwania taji la Ligi Kuu bara zimezidi kunoga huku mambo yakionekana kunyooka zaidi kwa mabingwa watetezi, Yanga, baada ya mechi za mwishoni mwa wiki iliyopita.
Sasa ni dhahiri Simba imejiweka kwenye wakati mgumu katika mbio hizo baada ya kupoteza kwa bao 1-0 mechi dhidi ya Toto Africans mwishoni mwa wiki iliyopita na hapo ndipo mambo yalipoinyookea Yanga.
Ushindi katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ungeiweka Simba kwenye ushindani mkubwa wa kuwania taji hilo linaloshikiliwa na Yanga, lakini sasa kipigo hicho kimeiacha timu hiyo kwenye mazingira magumu na kuifungulia Yanga milango ya mbio hizo.
Simba imebaki nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo na pointi zake 57 huku Yanga ikiwa kileleni na pointi 59 na mshindani mwingine wa taji hilo Azam ikiwa nafasi ya tatu na pointi 55.
Hasara kubwa kwa Simba ni kucheza mchezo mmoja zaidi, imecheza mara 25 huku Yanga na Azam zikicheza mechi 24, hivyo uwezo wa kuendelea kuvuna pointi baada ya kulingana mechi ni mkubwa.
Hasara zaidi inakuja kwa Simba kwenye mechi ilizosalia nazo. Mechi tano zote ngumu kwa wekundu hao wa Msimbazi na kwa hali timu ilivyo sasa matumaini ya ushindi moja kwa moja si makubwa.
Kwa hali ilivyo sasa, Simba inahitaji ushindi katika mechi zilizosalia lakini ikiomba Yanga na Azam zivurunde japo mechi mbili ili kurejesha matumaini ya kutwaa taji kwa angalau asilimia 95.
Hilo linatokana na uimara wa wapinzani hao, Yanga na Azam, hayo yasipotokea Simba itashuhudia mwaka mwingine unapita bila kushiriki michuano ya kimataifa.
Mei mosi Simba itacheza na Azam, mechi ambayo haitakuwa rahisi kwani Azam nayo itataka kushinda ili kujirudisha kwenye mbio za ubingwa,na siku zote Simba imekuwa ikipata tabu kupata matokeo mazuri kwa Azam.
Lakini pia hasara nyingine ni Simba kutokuwa na kocha wake Jackson Mayanja benchi pamoja na kumkosa mchezaji wake Hassan Kessy wanaotumikia adhabu ya kadi nyekundu walizopata kwenye mechi dhidi ya Toto.
Siku sita baadae Simba itacheza na Mwadui kabla ya kumenyana na Majimaji, Mtibwa Sugar na JKT Ruvu, mechi ambazo hakuna shaka ni ngumu kwa Simba.
Kwa upande wa Yanga mambo ni kama yanakwenda mteremko baada ya kubakiza mechi ‘nyepesi’, mechi dhidi ya timu ngumu zote imeshamaliza. Imebaki na Toto, Majimaji, Stand United, Mbeya City na Mgambo, uwezekano wa kushinda mechi hizo ni mkubwa kuliko kushindwa.
Kwa upande wa timu zilizo kwenye ukanda wa kushuka daraja timu tatu za Tanga zipo kwenye hali mbaya, Coastal Union inayoshika mkia ikiwa na pointi 22, kisha African Sports na Mgambo zenye pointi 23 kila moja.
Coastal Union na African Sports zimebakiwa na mechi tatu kila moja na Mgambo imebakiwa na mechi nne kumaliza msimu wa ligi, bado hali ngumu kwa timu hizo na nguvu ya ziada inahitajika kuzibakiza kwenye ligi msimu ujao.
No comments:
Post a Comment