TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania vijana wenye umri chini ya miaka 17 `Serengeti Boys’ inatarajiwa kushiriki mashindano maalumu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 nchini India, yatakayozishirikisha nchi za Marekani, Malasyia na Korea Kusini na wenyeji mwezi ujao.
Taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Baraka Kizuguto iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa Chama cha Soka India (AIFF) kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17.
Ilisema mashindano hayo ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka kesho. “Nchi tano zitashiriki mashindano hayo yatakayofanyika katika mji wa Goa kuanzia Mei 15-25, 2016 ambapo michezo itachezwa kwa mfumo wa ligi kwa kila timu kucheza michezo minne, kabla ya mchezo wa mwisho wa fainali wa kumpata bingwa wa mashindano hayo,” ilisema taarifa hiyo.
Serengeti Boys imeshacheza michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa mpaka sasa, moja dhidi ya Burundi na miwili dhidi ya timu ya vijana wa Misri (The Pharaohs). Kwa mujibu wa Kizuguto, Serengeti Boys inatarajiwa kuingia kambini mwishoni mwa mwezi huu katika hosteli za TFF zilizopo Karume kujiandaa kwa safari ya India.
Serengeti Boys inanolewa na kocha Bakari Shime, akisaidiwa na Sebastian Mkomwa chini ya mshauri wa ufundi wa timu za vijana Kim Poulsen, ambapo Juni mwaka huu Serengeti Boys itacheza na Shelisheli mchezo wa kuwania kufuzu fainali za vijana za Afrika.
No comments:
Post a Comment