YANGA imejiweka kwenye wakati mgumu wa kusonga mbele kwenye mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Al Ahly ya Misri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kutokana na sare hiyo, Yanga itahitaji ushindi wa aina yoyote ama sare ya kuanzia mabao 2-2 kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa Misri wiki ijayo ili kusonga mbele hatua inayofuata.
Kwenye mchezo huo, Al Ahly walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa kwa kichwa na mchezaji Amri Gamal dakika ya 10 kutokana na mpira wa adhabu ndogo na mabeki wa Yanga kujisahau kuuokoa kabla ya kumkuta mfungaji.
Hata hivyo bao hilo lilidumu kwa dakika nane tu, kwani Yanga walisawazisha baada ya beki wa Al Ahly, Ahmed Hegazy kujifunga katika juhudi za kuokoa mpira wa krosi kutoka kwa winga wa Yanga, Isoufou Boubacar.
Kuingia kwa bao hilo kuliongeza kasi kwa Yanga kufanya mashambulizi ya mara kwa mara, lakini mabeki wa Al Ahly walikuwa imara kuzuia hatari zilizoelekezwa kwenye lango lao na washambuliaji Donald Ngoma na Amis Tambwe.
Kipindi cha pili kocha wa Yanga Hans van Pluijm alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Isoufou Boubacar na Amis Tambwe na kuwaingiza Geofrey Mwashiuya na Simon Msuva.
Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuonekana kuisaidia sana kwani hayakuweza kubadili sura ya mchezo huo.
Yanga ilipata pigo kwa kipa wake Ally Mustapha ’Barthez’ kuumia dakika ya 81 na Deogratius Munishi ’Dida’ kuingia badala yake.
Yanga; Ally Mustapha/ Deogratius Munishi, Juma Abdul, Hajji Mwinyi, Kelvin Yondani, Vincent Bossou, Salum Telela, Deus Kaseke, Thabani Kamusoko, Amis Tambwe/ Simon Msuva, Donald Ngoma na Isoufou Boubacar/Geofrey Mwashiuya.
Al Ahly; Sherif Ekramy, Mohamedi Hany, Sabry Raheel, Rami Rabea, Ahmedi Hegazy, Abdallah Said, Hossam Ghaly, Amri Gamal, Ramadhan Sobhi, Moaem Zakaria.
No comments:
Post a Comment