Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (flyover), inayojengwa katika makutano ya Barabara za Mandela na Nyerere, kwenye eneo la Tazara juzi, Rais Magufuli aliita misaada ya wahisani ‘mkate wa masimango’ na kusema kuliko kula mkate huo ni bora kushindia muhogo.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuzungumzia misaada yenye masharti tangu Shirika la Changamoto ya Milenia (MCC) la Marekani, kusitisha msaada wa Dola za Marekani milioni 472.8 karibu Sh1 trilioni, zilizokuwa zitumike kuongeza kasi ya usambazaji umeme.
MCC ilisitisha msaada huo ikilalamikia uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliofanyika Machi 20, ukisusiwa na Chama cha Wananchi (CUF).
Akizungumzia kauli hiyo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema ni jambo jema kwa Watanzania kujitegemea, lakini kwa sasa haijawezekana moja kwa moja.
“Mimi nilishasema kwamba, jambo la kujitegemea ni jema, tunatakiwa kujifunza kujitegemea, lakini kwa sasa bado hatuna uwezo, tunatakiwa tujiandae,” alisema Msigwa na kuongeza:
“Hata bajeti iliyopita tulipunguza utegemezi kwa asilimia kadhaa. Hata mtoto mchanga anapozaliwa anaanza taratibu… kulikuwa na uzembe mwingi uliofanyika serikalini, unatakiwa kushughulikiwa.”
Alisema licha ya kuunga mkono dhana ya kujitegemea, Msigwa alionya tabia ya Serikali ya Magufuli kuwaghasi watumishi wa umma na watu wasio na hatia.
Naye mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema ni muhimu Rais Magufuli kuwa makini katika utekelezaji wa kauli yake hiyo.
“Inabidi awe makini sana jinsi anavyotekeleza mipango yake na jinsi anavyofanya kazi na wafadhili. Ni dhahiri kwamba kuna miradi bado inaendelea na hata hizo barabara nyingi alizosimamia yeye mwenyewe akiwa waziri zilikuwa zinafadhiliwa na wafadhili,” alisema Mbunda.
Alisema mbali na barabara, kuna miradi mingi inafadhiliwa na nchi wahisani ikiwamo ya umeme, hivyo inahitajika diplomasia ya uchumi ili kuendeleza uhusiano huo.
Kwa upande wake Profesa wa Siasa wa Chuo Kikuu cha Iringa, Gaudence Mpangala aliunga mkono dhana ya kujitegemea, lakini amekubaliana na sababu za Marekani kukatisha msaada kutokana na utata wa uchaguzi wa marudio wa Zanzibar.
Alisema misaada haina shida kwa sababu inachochea maendeleo, lakini tukio la Zanzibar limechafua taswira ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment