mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Thursday, April 14, 2016

Walio ‘Benchi’ Kusubiri Rais Magufuli Awapangie Kazi Mpya Waongezeka



Uamuzi wa kutengua uteuzi wa makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wilaya na watumishi wengine waandamizi kwa maelezo kuwa watapangiwa kazi nyingine, inazidi kuongezeka baada ya Rais kumvua Anne Kilango ukuu wa mkoa na kuahidi kumpangia kazi nyingine.

Mpaka kufikia jana, makatibu wakuu sita na wakuu wa mikoa na wilaya kumi walikuwa wamevuliwa nyadhifa zao na kuelezwa na mamlaka zao za uteuzi kuwa watapangiwa kazi nyingine huku nafasi zao wakipewa watu wengine.

Utenguaji wa uteuzi wa makatibu wakuu sita na mkuu mmoja wa mkoa umefanywa na Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani Novemba 5, mwaka jana huku Jakaya Kikwete, aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Nne, akitengua uteuzi wa wakuu tisa wa wilaya na mikoa ambao mpaka sasa hawajapangiwa kazi nyingine.

Kitendo cha kuwaweka pembeni wateule hao wa Rais kimezua maswali mengi, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa ulipwaji wa stahiki mishahara na posho mbalimbali hasa kwa wale wanaokaa muda mrefu bila kupangiwa kazi nyingine.

Baadhi ya wachambuzi waliozungumzia suala hilo walisema licha ya mamlaka ya uteuzi ya watumishi hao kuwa chini ya rais, hoja ya kupangiwa majukumu mengine haraka kwa lengo la kuokoa fedha haikwepeki.

Kwa mujibu kwa kifungu cha 13 (6) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2014, mtumishi wa umma wa ngazi ya uteuzi wa Rais, akivuliwa wadhifa, mshahara wake wa mwezi utabaki kama ulivyo isipokuwa posho aliyokuwa akipokea wakati wa uteuzi itapangwa kulingana na matoleo ya ofisi kuu ya Utumishi wa Umma.

Pia kifungu cha 20 (1) cha kanuni hizo kinasema: “Iwapo mtumishi wa ngazi ya uteuzi wa Rais, atakuwa hayupo katika nafasi yake ya utumishi, nafasi yake itashikiliwa na mtumishi mwenye wadhifa sawa na wake au anayemfuatia kwa idhini ya Katibu Mkuu au mkuu wa taasisi au Katibu Mkuu Kiongozi kulingana na wadhifa wa anayeondoka.”

Hata hivyo, makatibu wakuu walioondolewa nafasi zao zilijazwa na wengine walioteuliwa na Rais Magufuli, huku wakuu wa wilaya na mikoa pia nafasi zao zikijazwa na wengine na hivyo kuwafanya wote kuendelea kusubiri majukumu mengine.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Angela Kairuki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, hakutaka kuzungumzia suala hilo.

“Mkuu wa utumishi wa umma ni Katibu Mkuu Kiongozi. Yeye ndiye atakuwa na nafasi nzuri ya kusema hilo, maana mimi nikisema nitakuwa kama naingilia.”

Jitihada za kumpata Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi hazikufanikiwa baada ya kutafutwa kwa wiki mbili mfululizo bila kupatikana.

Katibu mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi (Tucta), Nicolaus Mgaya alisema ni jambo linaloweza kuzua mjadala iwapo watumishi hao watakaa muda mrefu bila kupangiwa majukumu mengine.

“Kwanza wanalipwa fedha za umma bila kuwajibika popote. Ni vyema uteuzi wa mtu ukitenguliwa isichukue muda mrefu awe amepangiwa majukumu mengine,” alisema Mgaya.

“Inawezekana mtu akalipwa mpaka siku anastaafu akifikisha miaka 60. Na ikitokea hivyo na pia kama rais hajamstaafisha mtu huyo ana haki pia ya kulipwa na ataendelea kulipwa tu.”

Alisema litakuwa jambo jema kama uteuzi mpya utafanyika haraka iwezekanavyo ili kuondoa sintofahamu iliyopo sasa kwa kuwa jambo hilo lisipotazamwa kwa kina, nchi itajikuta inawalipa mishahara watumishi wanaosubiri kupangiwa kazi nyingine.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala aliungana na Mgaya na kufafanua kuwa jambo hilo si sawa na linahitaji kukumbushwa mara kwa mara.

Alisema ili kuondokana na suala hilo, inapaswa watendaji hao kupangiwa majukumu mengine muda mfupi baada ya kuwekwa kando.

“Ninachokiona ni kama kila Serikali kutaka kuwa na watu wapya. Rais Magufuli ameingia madarakani na inaonekana wazi kuwa anataka kufanya kazi na watu wapya. Tazama makatibu wakuu waliowateua hivi karibuni na hata kitendo cha kumuondoa Sefue,” alisema Mpangala.

Utenguaji wa uteuzi

Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa akisimamisha, kutengua uteuzi na kutimua watumishi kadhaa waandamizi na kati ya aliotengua uteuzi wao, alisema kuwa atawapangia kazi nyingine.

Desemba 30, mwaka jana Rais Magufuli alifanya uteuzi wa makatibu wakuu na naibu 50 wa wizara, huku akiwaacha baadhi yao ambao alisema watapangiwa kazi nyingine.

Walioachwa ni pamoja na Dk Donnan Mmbando (Afya), Balozi Liberata Mulamula (Mambo ya Nje), Omari Chambo (Nishati na Madini), Jumanne Sagini (Tamisemi) na Joyce Mapunjo (Afrika Mashariki).

Katika orodha hiyo, yupo Balozi Ombeni Sefue, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, ambaye alikuwa mteule wa kwanza wa Rais Magufuli kuondolewa Ikulu akimpisha Balozi John Kijazi.

Rais alisema atampangia kazi nyingine Balozi Sefue, lakini hadi sasa bado haijatangazwa kazi aliyopangiwa.

Wengine ambao uteuzi wao ulitenguliwa ni aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka kupisha uchunguzi baada ya kutajwa kuhusika katika matumizi mabaya ya Sh13 bilioni kwenye Shirika la Reli Tanzania (TRL).

Mwinjaka alikuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya Katibu Mkuu kuondolewa na Rais Magufuli. Uteuzi wake ulitenguliwa wakati Dk Magufuli alipotimiza mwezi mmoja tangu awe Rais wa Awamu ya Tano.

Mbali na Rais Magufuli kuwaweka pembeni watumishi hao, Kikwete naye aliwaweka pembeni watumishi kadhaa kwa sababu tofauti.

Desemba 7, 2014 Kikwete aliteua wakuu wapya wa mikoa, akiwapandisha cheo wakuu wa wilaya na kuwaacha watatu akieleza kuwa watapangiwa kazi nyingine.

Walioachwa kwa ahadi ya kupangiwa kazi nyingine ni Dk Christine Ishengoma (Iringa) na Kanali Fabian Massawe (Kagera). Katika panga hilo pia alikuwepo Kanali Joseph Simbakalia aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ambaye tayari ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzi ya Nje (EPZA).

Pia Februari 19, 2015 Kikwete alihitimisha uteuzi wa nafasi za kisiasa za mkupuo kwa kuwang’oa wakuu wa wilaya 19, kuteua wapya 27, kuhamisha 64 na 42 wakibaki kwenye vituo vyao.

Katika kundi la wakuu wa wilaya 19 waliong’olewa, uteuzi wa wakuu 12 ulitenguliwa na saba ilielezwa kuwa watasubiri majukumu mapya.

Wakuu saba wa wilaya waliobadilishiwa majukumu ni Brigedia Jenerali Cosmas Kayombo, aliyekuwa Simanjiro, Kanali Ngemela Lubinga (Mlele), Juma Madaha (Ludewa), Mercy Silla (Mkuranga), Ahmed Kipozi (Bagamoyo) na Elinas Pallangyo (Rombo).    

No comments:

Post a Comment