KOCHA Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall amesema ni kama `waliporwa’ ushindi na Ndanda FC katika mchezo wa juzi baada ya wachezaji wake kushindwa kutimiza ipasavyo majukumu yao uwanjani. Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Azam FC ililazimishwa sare ya mabao 2-2.
Timu hiyo ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 kipindi cha kwanza cha mchezo huo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, lakini ilijikuta ikiondoka na pointi moja baada ya Ndanda kusawazisha mabao yote kipindi cha pili. Akizungumza juzi baada ya mchezo huo, Hall alisema wachezaji wake hawakujiamini mchezoni na walikosa ari ya kupambana ili kusaka ushindi.
“Hatukucheza vizuri kabisa, tulicheza vyema dakika 20 za mwanzo na baada ya hapo hatukuuonesha mchezo mzuri hasa kipindi cha pili, nadhani leo (juzi) wachezaji walikosa kujiamini na kutimiza majukumu yao uwanjani,” alisema.
Alisema kila mtu anajisikia furaha kulaumu waamuzi na wengine, lakini wakati huo wachezaji walishindwa kutimiza majukumu yao na hiyo imeonekana hata kwenye mechi zao mbili zilizopita.
Azam FC imefikisha pointi 52 na kubakia katika nafasi ya tatu, huku ikizidiwa pointi moja na Yanga inayoshika nafasi ya pili na pointi tano dhidi ya Simba iliyo kileleni, lakini imeizidi Yanga mchezo mmoja huku ikizidiwa mechi moja na Simba.
No comments:
Post a Comment