mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Monday, April 4, 2016

Chanjo saratani ya mlango wa kizazi kutolewa mwakani



SERIKALI inatarajia kuanza kutoa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa nchi nzima, kuanzia mwakani katika utaratibu wa kawaida wa utoaji wa huduma za chanjo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Ulisubisya Mpoki wakati akifungua mkutano wa tathmini ya huduma za chanjo nchini unaofanyika mjini hapa.
Alisema kutokana na maendeleo katika sayansi, chanjo mpya ya kuzuia magonjwa ya kichomi na kuhara kwa watoto na satarani ya shingo ya mlango wa kizazi zimepatikana, zingine ziko katika hatua ya majaribio zikiwemo za Ukimwi na malaria.
Dk Mpoki alisema pia kuwa utekelezaji wa mpango wa taifa wa chanjo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, umeweza kuvuka kiwango cha asilimia 90 kitaifa.
“Tumeweza kuzuia uingizwaji wa virusi pori vya ugonjwa wa polio kutoka katika nchi jirani hali inayothibitisha kuwa udhibiti wa ugonjwa wa polio nchini uko vizuri,” alisema Dk Mpoki.
Dk Mpoki alisema mwaka 2015 Tanzania ilipata cheti kuwa ni miongoni mwa nchi huru dhidi ya ugonjwa wa polio. Alisema kwa kushirikiana na huduma za chanjo, imeboresha na itaendelea kuboresha huduma ili kuhakikisha watoto wanapata chanjo zenye ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa.
Aliitaka mikoa na wilaya kuandaa mipango na mikakati yao katika maeneo muhimu ya chanjo kama vile utoaji wa huduma za mkoba, utaratibu wa kumfikia kila mtoto ili apate chanjo, upatikanaji wa mitungi ya gesi kwenye vituo, uhamasishaji jamii juu ya umuhimu wa huduma ya chanjo.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Christopher Kamugisha alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazofanya vizuri kwenye chanjo.
Alitaka juhudi zaidi ili kuweza kufikia watoto wote waliolengwa.
Alisema ili nchi iendelee kukubalika haina ugonjwa wa polio ni muhimu kuhakikisha ufuatiliaji wa magonjwa ya kupooza yanafuatiliwa na kufikia viwango vinavyokubalika.
Pia alisema Tanzania imefikia viwango vya kutokomeza surua ambapo mwaka jana ni mlipuko moja tu uliotokea dalili ambayo ni nzuri.
“Tanzania ni nchi pekee Afrika ambayo mikoa na wilaya imefikia lengo la kutunza chanjo kwa miezi mitatu”, alisema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Charles alisema mikutano ya kufanya tathimini ya huduma za chanjo nchini kila mwaka imesaidia kuinua kiwango cha chanjo hadi kufikia asilimia 97 kwa mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment