mazingira

mazingira
kwa pamoja tuyatunze mazingira

Monday, April 4, 2016

Saba matatani kwa fedha za mahindi ya msaada



WATENDAJI saba wa vijiji na kata katika Halmashauri ya wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wanatuhumiwa kutafuna fedha za mahindi ya msaada zaidi ya Sh mil 5.3, yaliyotolewa na Serikali.
Mahindi hayo yanaelezwa kutolewa mwaka 2012, 2013 na 2014 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Rostrika Turuka alisema kuwa, watendaji hao wamekuwa wakiagizwa kwa nyakati tofauti kuhakikisha wanarejesha fedha hizo zitumwe Ofisi ya Waziri Mkuu katika kitengo cha maafa, lakini wamekuwa wakikaidi.
Turuka aliwataja kuwa ni aliyekuwa Mtendaji wa kijiji cha Mwanzugi aliyesimamishwa kazi, Stanley Ngassa, Mtendaji kata ya Mbutu, Fabian Mwelele, Mtendaji wa Buchenjegele, Hussein Luziga na Mtendaji wa Kata ya Itundulu, Stephano Manundo.
Wengine ni pamoja na Mtendaji wa kijiji cha Kagongwa ambaye alishafukuzwa kazi, Rahel Stephano, Mtendaji wa kijiji cha Mwagala, Idd Kagusa na Mtendaji wa kijiji cha Ngulu, Mazazi Shija. Kwa pamoja wanadaiwa kutumia Sh 5,039,100 za mahindi ya msaada.
Alisema, kwa sasa kazi hiyo imekabidhiwa kwa Polisi wilayani humo kuhakikisha wanakamatwa na kulipa deni hilo na watakaokaidi watafikishwa mahakamani.
Mkuu wa Polisi wa wilaya, Costantine Mbogambi amethibitisha kupokea majina saba ya watendaji hao na kwamba ametoa mwezi mmoja wote wahakikishe wamelipa deni hilo.
Alisema wakiendelea kukaidi hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani. Baadhi ya watendaji kata na vijiji wakizungumza kwa nyakati tofauti pasipo kutaka kutajwa majina yao, walidai wako tayari kutafuta fedha hizo na kuzirejesha.

No comments:

Post a Comment