Ugiriki imeanza kuwarejesha Uturuki wahamiaji walioko nchini humo ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya ambayo yamekosolewa na makundi ya haki za binadamu
Kundi la kwanza la wahamiaji hao limewasili nchini Uturuki asubuhi ya leo. Isaac Gamba anaarifu zaidi katika taarifa ifuatayo. Boti ya kwanza iliyobeba wahamiaji waliokuwa nchini Ugiriki, imewasili asubuhi hii katika bandari ya Dikili nchini Uturuki, ikisindikizwa na walinzi wa pwani ya nchi hiyo.
Boti hiyo, Nazli Jale ni moja ya mbili zenye kupeperusha bendera ya Uturuki, ambazo zimeondoka alfajiri ya leo jumatatu tarehe 04.04.2016 katika kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos zikiwa zimewabeba wahamiaji 131.
Mabasi yatumika kuwarejesha wahamiaji Uturuki
Mabasi maalumu kwa ajili ya kuwabeba mamia ya wahamiaji hao kwa ajili ya kusafirishwa kupelekwa nchini Uturuki nayo pia yaliwasili katika bandari za Lesbos na Chios nchini Ugiriki mapema asubuhi. Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki Efkan Ala amesema nchi yake iko tayari kuwapokea watu 500 ingawa serikali ya ugiriki imetoa majina ya watu 400 tu . Hata hivyo idadi hiyo inaweza kubadilika.
Baadhi ya wahamiaji wawasilisha maombi ya hifadhi katika dakika za mwisho.
Chanzo cha kipolisi kutoka katika kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki ambacho kimekuwa njia kuu ya watu wanaotafuta hifadhi barani ulaya wakitokea nchini Uturuki kimesema kumekuwepo na harakati katika dakika za mwisho za maombi ya watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa barani ulaya miongoni mwa wahamiaji 3,300 walioko nchini humo.
" Tuna idadi ya zaidi ya watu 2,000 ambao tayari wameonesha nia ya kutafuta hifadhi ya kisiasa na tunahitaji kuona utaratibu unaofaa kwa ajili ya kushughulikia suala hilo'' amesema Boris Cheshirkov ambaye ni msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi katika kisiwa cha Lesbos, na kuongeza kuwa shughuli hiyo itafanyika kulingana na taratibu zinazohusiana na masuala ya hifadhi ya kisiasa nchini Ugiriki kwa wale ambao wanahitaji kuelezea juu ya kuwepo na haja ya kulindwa.(P.T)
No comments:
Post a Comment